Tafuta

Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo limetuma salam za pongezi kwa Patriaki Porfirije Peric, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Pec, Belgrade Karlovci. Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo limetuma salam za pongezi kwa Patriaki Porfirije Peric, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Pec, Belgrade Karlovci. 

Majadiliano ya Kiekumene: Wakristo wa Serbia na Wakatoliki!

Ni sala ya Kardinali Kurt Koch kwamba, Roho Mtakatifu atamkirimia neema, baraka na mapaji kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Serbia, ili kwa pamoja waamini wa Kanisa la Kiorthodox na Kikatoliki waweze kuwa ni mashuhuda wa Injili. Waamini wa Makanisa haya watambue kwamba, Yesu ni Mzabibu wa kweli na wao ni matawi yake. Umoja wa Kanisa

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mchakato wa majadiliano ya kiekumene unafumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo anasema kwa mwelekeo huu, mashuhuda wa imani, tayari wamekwisha jenga umoja wa Kanisa kwa njia ya kumwaga damu yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni katika muktadha huu, Kardinali Kurt Koch amemwandikia Patriaki Porfirije (Peric), “Порфирије” Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Pec, Belgrade Karlovci ujumbe wa matashi mema, heri na baraka baada ya kuchaguliwa kuwa Patriaki wa Kanisa la Kiorthodox la Serbia. Ni sala yake kwamba, Roho Mtakatifu atamkirimia neema, baraka na mapaji kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Serbia, ili kwa pamoja waamini wa Kanisa la Kiorthodox na Kikatoliki waweze kuwa ni mashuhuda wa Injili.

Waamini wa Makanisa haya watambue kwamba, Kristo Yesu ni Mzabibu wa kweli na wao ni matawi yake. Wakikaa katika pendo lake na kuzishika Amri zake watazaa matunda na matunda yao yatapata kudumu. Rej. Yn. 15: 1-17. Kristo Yesu katika Sala yake ya Kikuhani alisali akisema “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi.” Yn. 17:21-23. Kardinali Kurt Koch anaombea umoja na mshikamano wa kidugu, ili uendelee kuzaa matunda yaliyoanzishwa na watangulizi wake, ili kuimarisha mchakato wa umoja na ushirikiano kati ya Makanisa haya mawili. Ni matumaini ya Kardinali Kurt Koch kwamba wataendelea kufanya kazi kwa umoja katika medani mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa na hata katika masuala ya elimu na utamaduni kwani hatima ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene ni utekelezaji wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu, ili wafuasi wake wote wawe wamoja.

Patriaki Porfirije (Peric), Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Pec, Belgrade Karlovci alizaliwa tarehe 22 Julai 1961 huko mjini Becej, Kaskazini mwa Nchi ya Serbia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kimonaki tarehe 21 Aprili 1985 akawekwa wakfu kuwa Mmonaki. Tarehe 21 Novemba 1990 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 13 Juni 1999 akawekwa wakfu kuwa Askofu. Na kati ya Mwaka 2014 hadi mwaka 2021 alikuwa ni Patriaki wa Zagreb na Ljubljana huko Serbia. Sinodi ya Maaskofu wa Serbia ikamchagua kuwa Askofu mkuu wa wa Jimbo kuu la Pec, Belgrade Karlovci na kusimikwa rasmi tarehe 19 Februari 2021.

Kardinali Kurt Koch
23 February 2021, 15:34