Tafuta

2020.07.01 ASKOFU MKUU PAUL GALLAGHER 2020.07.01 ASKOFU MKUU PAUL GALLAGHER 

Gallagher kwa UN:Haki za binadamu lazima zilindwe na kuheshimiwa

Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican,kwa njia ya video amehutumia Umoja wa Mataifa akisisitizia kuhusu asili ya haki za bindamu kwamba lazima ziheshimiwe hata katika mahusiano ya hatua za kudhibiti janga corona linaloendelea.

Na Sr. Angela. Rwezaula – Vatican.

Katika fursa ya kikao cha 46 za Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa, (UN), Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican, kwa njia ya video ametoa hotuba yake akianza kuwafikishia salamu kutoka kwa Papa Fracisko na kutoa shukurani kwa kupewa fursa hiyo ya kuhutubia katika kikao hicho. Askofu Mkuu katika hotuba hiyo amesema mwaka umepita ambao covid-19 imeleta madhara katika maisha na kupoteza wengi, huku ikiacha bado mashaka ya uchumi, kijamii na mfumo wa kiafya. Imekuwa changamoto yauwajibikaji kwa wote katika kulinda na kuhamasisha haki za binadamu ulimwenguni, wakati huo huo hata kusisitizia umuhimu wao. Kama jumuiya ya ulimwengu, “tunahitaji kugundua tena msingi wa haki za binadamu ili kuzitekeleza kwa mtindo halisi”.  Utangulizi wa Azimio la Ulimwenguni la Haki za Binadamu amesema ulitangaza kwamba: “kutambuliwa kwa hadhi asili ya watu wote wa familia ya wanadamu na haki sawa na isiyoweza kutengwa ni msingi wa uhuru, haki, na amani. 

Malengo ya haki za binadamu bado yako mbali

Mkataba wa UN hivyo hivyo unasisitiza imani yake katika misingi ya haki za binadamu, katika utu na thamani ya mwanadamu, katika haki sawa za wanaume na wanawake, na ya mataifa makubwa na madogo”. Askofu Mkuu ameongeza kusema: “Nyaraka hizi mbili zinatambua ukweli ambao unategemea hitaji la makubaliano, na umewekwa kwa wakati, utamaduni, au muktadha; yaani kwamba kila mtu amejaliwa ubinadamu na kwa ulimwengu wote. Kwa bahati mbaya, kujitolea kwa dhati ni rahisi kutamka kuliko kufanikisha na kutekeleza. Kwa maana hiyo Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu (UDHR) unathibitisha kwamba kutambuliwa kwa hadhi na haki sawa na zisizoweza kutengwa za washiriki wote wa familia ya wanadamu ni msingi wa uhuru, haki, na amani ulimwenguni. Lazima tukubali hata hivyo kwamba malengo haya bado yako mbali kutambuliwa, kuheshimiwa, kulindwa na kukuzwa katika kila hali”, amesisitiza Askofu Mkuu.

Haki za binadamu zinategemea msingi wa ndani lazima kuhamasisha

Kwa hakika, kuhamasisha haki msingi za kibinadamu kweli kunategemea msingi ambao hupatikana ndani mwake. Mazoezi yoyote au mfumo ambao ungeshughulikia haki katika mtindo wa kufikirika, ni hatari ya kudhoofisha sababu zake, kutengwa na maadili yaliyokuwepo na ya ulimwengu wote. Katika muktadha kama huu wa haki ambazo hazina maadili, taasisi za haki za binadamu zinaweza kuathiriwa na mitindo iliyopo, maono au itikadi zilizopo, na inaweza kuweka majukumu au adhabu ambazo hazijawahi kufikiriwa na vyama vya serikali, ambayo wakati mwingine vinaweza kupingana na maadili waliyopaswa kuhamasishwa. Wanaweza hata kudhani kuunda haki zinazoitwa mpya ambazo hazina msingi na hivyo kuachana na kusudi lao la kutumikia hadhi ya binadamu.

Watu wengi wamejikua katika mazingira magumu kutokana na covid-19

Katikati ya janga la sasa la covid-19, hatua kadhaa zilizowekwa na mamlaka kuhakikisha afya ya umma pia inazingatia utekelezwaji wa haki za binadamu. Idadi ya watu wanaojikuta katika mazingira magumu, kama wazee, wahamiaji, wakimbizi, watu asilia, wakimbizi wa ndani, na watoto wameathiriwa vibaya na shida ya sasa. Upungufu wowote juu ya utekelezaji wa haki za binadamu katika ulinzi wa afya ya umma lazima utokane na hali ya ulazima mkubwa. Vizingiti kama hivyo lazima viwe sawa na hali hiyo, kwa kwa namna ya kutofanya ubaguzi, na kutumia wakati hakuna njia nyingine zinazopatikana. Katika suala hili Vatican inarudia kubainisha  juu ya udharura wa kulinda haki ya uhuru wa mawazo, dhamiri, na dini. Kwa namna ya pekee imani ya kidini na kiekelezo chake, inajikita katika kiini cha hadhi ya mwanadamu katika dhamiri yake.

Uhuru wa kidini unahitaji ushirikiano na sera za kisiasa

Ili kuheshimu thamani ya asili ya haki hii, uhuru wa kweli wa kidini unahitaji mamlaka ya kisiasa kushirikiana na viongozi wa dini, na mashirika ya kidini, na asasi za kiraia, ambazo zimejitoa kuhamasisha uhuru wa dini na dhamiri. Jibu la ulimwengu kwa janga la covid-19 linafunua wazi uelewa huu thabiti wa uhuru wa kidini unavyoharibiwa. Vatican inapenda kusisitiza kwamba, kama inavyotambuliwa katika vyombo vingi vya haki za binadamu, uhuru wa dini pia unalinda ushuhuda wake wa umma na maoni, wote mmoja mmoja na kwa pamoja, hadharani na kwa faragha, katika aina tofauti za ibada, maadhimisho na mafundisho.

Ili kufanikiwa lazima tuhame kutoka kile kinachotugawanya

Kwa kuhitimisha Askofu Mkuu Ghallagher amesema “li kupambana vyema na matokeo ya mizozo mbalimbali lazima tuwe tayari kuhama zaidi kutoka kile kichotugawanya. Kwa sababu hiyo mwaliko wa Baba Mtakatifu Francisko, uliooneshwa katika barua yake ya hivi karibuni ya ‘Fratelli tutti’ yaani ‘Wote ni ndugu’ na ambayo, ni ya umuhimu, “kwamba katika wakati wetu huu, kwa kutambua utu wa kila mwanadamu, tunaweza kuchangia kuzaliwa upya kwa matakwa ya ulimwengu wa udugu. Mgogoro wa sasa unatupatia fursa ya kipekee ya kukaribia pande nyingi kama kielelezo cha hali mpya ya uwajibikaji wa ulimwengu, mshikamano unaowekwa katika haki na kupatikana kwa amani na umoja ndani ya familia ya wanadamu, ambao ni mpango wa Mungu kwa ulimwengu wetu. Vatican itaendelea kushirikiana hadi mwisho”.

23 February 2021, 15:09