Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Monsinyo Mark Gerard Milles kuwa Balozi Mpya wa Vatican nchini Benin. Baba Mtakatifu Francisko amemteua Monsinyo Mark Gerard Milles kuwa Balozi Mpya wa Vatican nchini Benin. 

Askofu mkuu Mark Gerard Miles, Balozi wa Vatican Nchini Benin

Askofu mkuu mteule Mark G. Miles alizaliwa tarehe 13 Mei 1967 huko Gibralta, nchini Uingereza. Historia inaonesha kwamba, Askofu mkuu mteule Mark Gerard Miles anakuwa ni Balozi na Askofu mkuu wa kwanza kutoka katika eneo hili la Gibralta. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 14 Septemba 1996 akapewa daraja Takatifu ya Upadre! Matendo makuu ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Monsinyo Mark Gerard Miles, kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Benin na kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu mteule Mark Gerard Miles alizaliwa tarehe 13 Mei 1967 huko Gibralta, nchini Uingereza. Historia inaonesha kwamba, Askofu mkuu mteule Mark Gerard Miles anakuwa ni Balozi na Askofu mkuu wa kwanza kutoka katika eneo hili la Gibralta. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 14 Septemba 1996 akapewa daraja Takatifu ya Upadre. Hii ilikuwa ni Sikukuu ya Kutukuka kwa Fumbo la Msalaba, chombo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu! Ni ishara ya neema, sala, msamaha, upatanisho na matumaini.

Ni kutokana na maana hii mpya, Mama Kanisa anaona fahari kuu kuimba sifa kuu za Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Msalaba unaendelea kumfunza mwamini kwamba, hakuna mapendo kamili yasiyokuwa na mateso na matumaini ya uzima wa milele. Baada ya Mwaka 1996 Askofu mkuu mteule Mark Gerard Miles akaanza maandalizi ya kujiunga na Taasisi ya Kipapa ya Diplomasia ya Kanisa na hatimaye akajipatia Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa. Katika maisha na utume wake wa Kidiplomasia, alipangiwa huko Ucuador, Hungaria na Vatican katika Idara ya masuala ya jumla kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican.

Wakati wa hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Ufilippin na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2015, ndiye aliyekuwa anatafsiri hotuba za Baba Mtakatifu mubashara, kutoka katika lugha ya Kihispania kwenda katika lugha ya Kiingereza, kiasi cha kuwaacha wasikilizaji wengi wakiwa wameshika tama kutokana na umahiri wake! Tarehe 31 Agosti 2019 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwa Nchi za Amerika “Organization of American States, OAS”. Na hatimaye, tarehe 5 Februari 2021, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Benin na kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu.

Benin
08 February 2021, 14:33