Tafuta

Kardinali Leonardo Sandri tarehe 16 Februari 2021 amemweka wakfu Monsinyo Dominique Mathieu kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Teheran-Ispahah lililoko nchini Iran: Shuhuda wa Uinjilishaji, amani na majadiliano. Kardinali Leonardo Sandri tarehe 16 Februari 2021 amemweka wakfu Monsinyo Dominique Mathieu kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Teheran-Ispahah lililoko nchini Iran: Shuhuda wa Uinjilishaji, amani na majadiliano. 

Askofu mkuu Dominique Mathieu Jimbo Kuu la Teheran! Shuhuda!

Askofu mkuu mpya Dominique Mathieu wa Jimbo kuu laTeherani amekumbushwa kwamba, ameteuliwa na sasa anatumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Atapaswa kuwa ni shuhuda na chombo cha amani inayobubujika kutoka ndani mwake. Asimamie imani, maadili na utu wema pamoja na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu anapaswa kuwa ni mtu wa sala, kiongozi anayejipambanua kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa maneno, lakini zaidi kwa njia yaa maisha adili na matakatifu. Ni kiongozi wa maisha ya kiroho anayepaswa kuwa kweli ni mchungaji mwema, anayejipambanua pia kutokana na harufu ya kondoo wake, kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Kanisa linahitaji viongozi wakweli na waadilifu; watu wanaoweza kujitosa kimasomaso kwa ajili ya watu wa Mungu waliokabidhiwa kwao. Kanisa mahalia linamhitaji Askofu ambaye ni shuhuda wa mateso, kifo ufufuko wa Kristo, chemchemi ya matumaini mapya. Askofu awe ni mtu mnyenyekevu na jasiri, atakaye pandikiza mbegu ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Askofu awe ni mtu mwenye uwezo wa kuunganisha nguvu na rasilimali iliyopo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika jimbo husika. Kimsingi haya ndiyo mambo msingi ambayo yanapaswa kuoneshwa na Askofu au wale wanaotamani kufikia utimilifu wa Daraja Takatifu ya Upadre ambalo kimsingi limegawanyika katika madaraja makuu matatu: Uaskofu, Upadre na Ushemasi, kadiri ya Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Tarehe 16 Februari 2021, Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki ambaye pia ni Makamu wa Dekano wa Baraza la Makardinali, amemweka wakfu Monsinyo Dominique Mathieu, ofm Conv., kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Teheran-Ispahah kwa ajili ya waamini wa Madhehebu ya Kilatini nchini Iran. Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la “Santi XII Apostoli” lililoko mjini Roma. Askofu mkuu mpya Dominique Mathieu, amekumbushwa kwamba, ameteuliwa na sasa anatumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Atapaswa kuwa ni shuhuda na chombo cha amani inayobubujika kutoka katika undani wake. Asimamie imani, maadili na utu wema pamoja na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene. Kristo Yesu kabla ya kupaa mbinguni, aliwahakikishia Mitume wake kwamba, wakisha kumpokea Roho Mtakatifu, watakuwa mashahidi wake katika Yerusalemu na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi!

Kumbe, Askofu mkuu Dominique Mathieu, ofm Conv., hana sababu ya kuogopa kwamba, yeye bado ni mdogo, kwa sababu Mwenyezi Mungu amemteua, akamtakasa akiwa bado tumboni mwa Mama yake ili aweze kuwa Mhudumu wa Habari Njema ya Wokovu. Jambo la msingi ni kutambua kwamba, wito wa Daraja Takatifu ya Upadre inayopata utimilifu wake katika Uaskofu ni zawadi na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Katika kipindi cha Mwaka 2019 Baba Mtakatifu Francisko alifanya hija ya kitume nchini Morocco na Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu ambako kuna idadi kubwa ya waaamini wa dini ya Kiislam. Lengo lilikuwa ni kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, ili waamini wa dini hizi mbili waweze kufahamiana, kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipokutana na Sultan Al Malik al- Kamil kunako mwaka 1219. Baba Mtakatifu Francisko anasema majadiliano ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya waamini wa dini mbali mbali duniani.

Ni majadiliano ambayo yanafumbatwa katika utu na tunu msingi za maisha ya binadamu, ili kujenga na kudumisha leo na kesho iliyo bora zaidi inayosimikwa katika amani ya kweli.Jambo la msingi ni waamini kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani kwa njia ya majadiliano katika ukweli, uwazi, haki na usawa! Umoja, udugu wa kibinadamu na usawa ni nyenzo madhubuti dhidi ya vitendo vya kigaidi na misimamo mikali ya kiimani. Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Dominique Mathieu, ofm Conv., anatumwa nchini Iran kuwa ni chombo na shuhuda wa Injili, huku akijitahidi kufuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi katika maisha na utume wake. Akiwa nchini Iran atapaswa pia kujenga na kudumisha uekumene wa maisha unaofumbatwa katika uekumene wa damu na hatimaye, uekumene wa utakatifu.

Haya ni mambo msingi yanayoshuhudiwa na Wakristo katika umoja, udugu na upendo kama kikolezo cha ujenzi wa Ufalme wa Mungu na Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa kwa njia ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na maisha ya kitume. Uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile watahamasisha na kutekeleza umoja wa Wakristo na udugu kati yao.

Askofu mkuu DM
18 February 2021, 15:39