Tafuta

Mama Kanisa katika Sherehe ya Tokeo la Bwana anaadhimisha pia sikukuu ya Utoto Mtakatifu. Kauli mbiu kwa Mwaka 2021: Tunogeshe Udugu wa Kibinadamu! Mama Kanisa katika Sherehe ya Tokeo la Bwana anaadhimisha pia sikukuu ya Utoto Mtakatifu. Kauli mbiu kwa Mwaka 2021: Tunogeshe Udugu wa Kibinadamu! 

Sikukuu ya Utoto Mtakatifu: Tunogeshe Udugu wa Kibinadamu!

Maadhimisho ya Siku ya Utoto Mtakatifu ni changamoto kwa wazazi na walezi kuwajengea watoto wao ari na moyo wa kimissionari ili, hatimaye, waweze kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watoto wenzao sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, watoto yatima; wanaokumbana na magonjwa, njaa, ujinga na umaskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Tokeo la Bwana ni Siku ambayo pia Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Utoto Mtakatifu. Maadhimisho ya Mwaka 2021 yanaongozwa na kauli mbiu “Tunogeshe udugu wa kibinadamu”. Mwaka 2020 - 2021 umetawaliwa sana na athari za janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kumbe, watoto wengi hawakuweza kukusanya fedha kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenzao ambao wanashida zaidi kuliko wao! Lakini wamejitahidi kadiri walivyoweza. Siku hii ilianzishwa na Papa Pio wa XII kunako mwaka 1950, aliyetaka kuwaona waamini na watu wote wenye mapenzi mema wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi ya watoto wao kama Kristo Yesu, alivyowapatia nafasi ya pekee katika maisha na utume wake. Watoto wanapaswa kujifunza na kujenga: utamaduni wa upendo na mshikamano wa kidugu, kwa kujaliana, kusaidiana na kusali pamoja. Haya ni mambo msingi katika malezi na makuzi yao kwa sasa na kwa siku za usoni, ili kujenga na kudumisha umoja na upendo wa udugu wa kibinadamu.

Shirika la Utoto Mtakatifu lilianzishwa kunako mwaka 1843 na Askofu Toussaint de Forbin Janson wa Jimbo Katoliki la Nancy. Maadhimisho ya Siku ya Utoto Mtakatifu ni changamoto na mwaliko kwa wazazi na walezi kuwajengea watoto wao ari na moyo wa kimissionari ili, hatimaye, waweze kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watoto wenzao sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, watoto yatima; watoto wanaokumbana na magonjwa, njaa, ujinga na umaskini. Hata katika umaskini wao, watoto wanaweza kuchangia ustawi na maendeleo ya watoto wenzao sehemu mbali mbali za dunia ndiyo maana kauli mbiu ya mwaka 2021 inasema, “tunogeshe udugu wa kibinadamu”.

Madhara ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, yamechangia kuporomoka kwa mchango unaokusanywa na watoto wakati wa Sherehe za Noeli. Watoto hata katika changamoto zote hizi, bado wanaweza kusaidiwa kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimissionari, kwa kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano. Kwa njia hii watoto wamesaidia kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kuwapatia watoto wenzao mahitaji msingi kama vile: chakula, elimu, makazi na huduma bora ya afya.

Utoto Mtakatifu

 

 

05 January 2021, 15:44