Tafuta

Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW: Askofu mkuu Paul Richard Gallagher amefafanua historia, maana na umuhimu wake katika kukuza ulinzi na usalama duniani. Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW: Askofu mkuu Paul Richard Gallagher amefafanua historia, maana na umuhimu wake katika kukuza ulinzi na usalama duniani. 

Mkataba wa Kimataifa Kupinga Silaha za Nyuklia: Umuhimu Wake!

Utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za atomiki kwa ajili ya vita ni kinyume cha maadili na utu wema. Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW unalenga kujenga mazingira ya usalama, amani na utulivu bila ya kuwa na hofu ya mashambulizi ya silaha za maangamizi. Amani ya kweli inajengwa kwa njia ya majadiliano na mshikamano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe 20 Januari 2021 amesema kwamba Ijumaa tarehe 22 Januari 2021, Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW, ambao umeridhiwa na Mataifa zaidi 50 unaanza kutumika rasmi. Huu ni Mkataba wa Kimataifa unaopiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia. Hii inatokana na ukweli kwamba, matumizi ya silaha hizi hayana macho wala pazia, na hayawezi kuchagua wala kubagua! Katika kipindi kifupi tu, matumizi ya silaha hizi yanaweza kusababisha maafa makubwa na yatakayodumu kwa muda mrefu kwa binadamu na mazingira yake.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kutoa wito kwa Mataifa ambayo bado hayajaridhia Mkataba huu, kushiriki na kuendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba, dunia inakuwa ni mahali pa salama pasi na silaha za nyuklia, ili kuchangia katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa unaohitajika sana kwa wakati huu! Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika mahojiano maalum na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican anazungumzia kuhusu Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW, na historia yake, mchango wa Vatican, wito wa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na changamoto ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Baba Mtakatifu wakati wa hija yake ya kitume nchini Japan kuanzia tarehe 23 hadi 26 Novemba 2019, iliyopambwa na kauli mbiu: “Linda Maisha Yote”: Ujumbe unaoitaka familia ya Mungu katika ujumla wake, kusimama kidete kulinda: utu, haki na heshima ya binadamu dhidi ya vitisho vinavyohatarisha misingi ya amani na utulivu na hasa zaidi mapambano ya silaha, anasema, ili kuweza kuwa na amani ya kudumu, kuna haja kwa watu wote kuweka silaha zao chini, lakini zaidi zile silaha ya maangamizi. Hizi silaha za nyuklia zinazoweza kuleta maafa makubwa zaidi kwa miji na nchi mbali mbali duniani. Kwa mara nyingine Baba Mtakatifu anasema bila kupepesapepesa macho kwamba: utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za atomiki kwa ajili ya vita ni kinyume cha maadili na utu wema. Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW, unalenga kujenga mazingira ya usalama, amani na utulivu bila ya kuwa na hofu ya mashambulizi ya silaha za maangamizi.

Baada ya Jumuiya ya Kimataifa kushuhudia maafa makubwa yaliyotokana na matumizi ya silaha za maangamizi, kunako mwaka 1975 Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Kutengeneza, Kulimbikiza na Kutumia Silaha za Kibaiolojia na za Kemikali ulianza kutumika. Miaka ishirini baadaye, yaani tarehe 13 Januari 1993, ulizinduliwa mchakato wa kupiga rufuku maendeleo, utengenezaji na ulimbikizaji wa Silaha za Kemikali pamoja na matumizi yake na mkataba huo ukaridhiwa na nchi 193 hadi wakati huu. Hii ni Mikataba ya Kimataifa inayozitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuachana na sera na mikakati ya kutaka kutengeneza, kulimbikiza na kutumia silaha za maangamizi. Hii inatokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yanayoweza kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kumbe basi, Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW unadhibi kisheria matumizi yote ya silaha za maangamizi duniani na umeanza kutumika rasmi tarehe 22 Januari 2021.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko tangu mwanzo wa mchakato huu, ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwa ni chombo cha kisheria ili kudhibiti matumizi ya silaha za maangamizi duniani. Vatican inazisihi nchi ambazo hazijaridhia Mkataba huu, kufanya hivyo mapema iwezekanavyo ili kudumisha amani na utulivu duniani, huku utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa msukumo wa pekee! Hizi ni juhudi za Jumuiya ya Kimataifa kuona kwamba, ulimwengu unakuwa huru dhidi ya vitisho vya silaha za maangamizi kwa kujikita katika utamaduni wa kulinda uhai; kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano pamoja na utamaduni wa kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, ushuhuda wa “hibakusha” yaani wahanga wa mashambulizi ya mabomu ya nyuklia huko Hiroshima na Nagasaki utaendelea kuwa ni sauti inayotoa onyo kwa Jumuiya ya Kimataifa na kwa kizazi kijacho. Hapa kuna haja ya kujikita katika mchakato wa upatanaisho ya kitaifa, ili, hatimaye, kuweza kubinafsisha maneno ya Mzaburi yasemayo: “Kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu niseme sasa, “Amani ikae nawe”. Zab. 122: 8. Kumbukumbu hai sanjari na majadiliano katika ukweli na uwazi ni mambo msingi katika ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika misingi ya haki na udugu wa kibinadamu.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, anasema, ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 53 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2020 uliongozwa na kauli mbiu: Amani ni safari ya matumaini: Majadiliano, Upatanisho na Wongofu wa kiekolojia. Amani na utulivu wa Jumuiya ya Kimataifa, hauwezi kamwe kujengeka katika msingi wa vitisho na hofu ya maagamizi: Vunjilieni mbali hofu na vitisho! Baba Mtakatifu anakazia pamoja na mambo mengine: mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa unaosimikwa katika umoja wa familia kubwa ya binadamu. Watu wajenge utamaduni wa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja kwa kutambua kwamba, wote wanategemeana na kukamilishana. Huu ni mwaliko wa kutumia vyema uhuru wa kudhibiti na kusimamia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Karne ya 21 inakabiliwa na changamoto pevu zinazohitaji umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa kwa kuongozwa na kanuni ya auni. Kuna vitisho vingi dhidi ya amani na usalama kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, vitendo vya kigaidi, athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi, umaskini, ujinga na magonjwa ya milipuko yanayotishia usalama na maisha ya binadamu kama ilivyo kwa sasa ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030 ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani. Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora, kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama; nishati mbadala kwa gharama nafuu pamoja na uwepo wa mipango bora ya miji na makazi ya watu, ili kudumisha usalama na upatikanaji wa maendeleo fungamani ya binadamu.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kulinda mazingira pamoja na kudumisha amani duniani! Maambukizi makubwa ya ugonjwa Corona, COVID-19 ambayo yamesababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao ni changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher anaendelea kufafanua kwa kusema kwamba, watu wa Mungu watambue kwamba, amani na utulivu vinajengwa kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; mshikamano, umoja na udugu wa kibinadamu; haki, ustawi, maendeleo fungamani ya binadamu na mafao ya wengi. Huu ni mwaliko wa kuboresha miundombinu ya elimu, afya na ustawi wa jamii sanjari na watu kuaminiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja pamoja na kuwa na sera na mipango ya muda mrefu kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Francisko kwa kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kutambua, kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kuendelea kushirikiana na Mwenyezi Mungu katika kazi ya uumbaji na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa kuzingatia kanuni maumbile!

Mambo yote haya kimsingi ni changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema. Janga kubwa la Virusi vya Corona, COVID-19 pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi ni changamoto zinazoweza kutatuliwa ikiwa kama fedha inayotumika kutengenezea na kulimbikizia silaha za maangamizi itaelekezwa katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kutengeneza “Mfuko wa Mshikamano Kimataifa” kwa ajili ya kukoleza maendeleo fungamani katika Nchi Changa zaidi duniani!

Mkataba wa Kimataifa

 

22 January 2021, 15:58