Tafuta

Vatican News
Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2021: Dhana ya Sinodi Katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu mwelekeo wa kiekumene! Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2021: Dhana ya Sinodi Katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu mwelekeo wa kiekumene!  (Vatican Media)

Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo: Dhana ya Sinodi Kiekumene

Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2021 ni hija ya kiekumene inayosimika mizizi yake kwenye “Dhana ya Sinodi Katika Maisha na Utume wa Kanisa. Makanisa yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa mwaka 325. Dhana ya Sinodi kama changamoto ya kiekumene na umuhimu wa kumsikiliza Roho Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2021 ni “Kaeni katika pendo langu, ili mzae matunda”. Rej. Jn 15-5-9. Kristo Yesu ndiye Mzabibu wa kweli ni ufafanuzi unaotolewa katika Injili ya Yohane 15:1-17. Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo anasema, maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2021 ni hija ya kiekumene inayosimika mizizi yake kwenye “Dhana ya Sinodi Katika Maisha na Utume wa Kanisa. Makanisa yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa mwaka 325. Dhana ya Sinodi kama changamoto ya kiekumene; Umuhimu wa kumsikiliza Roho Mtakatifu mintarafu dhana ya Sinodi; Dhana ya Sinodi katika majadiliano ya kiekumene kati ya Wakatoliki na Waorthodox; Umuhimu wa upatanisho wa kiekumene kati ya dhana ya Sinodi na Ukuu wa viongozi wa Kanisa, Asili ya Ekaristi Takatifu katika dhana ya Sinodi na Ukuu wa viongozi wa Kanisa.

Kanuni ya Imani ya Nicea-Constantinopoli ni formula rasmi ambayo ilipitishwa na Mababa wa Mtaguso wa kwanza wa Nicea (325) ikakamilishwa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381) ili kubainisha imani sahihi ya Kanisa Katoliki dhidi ya uzushi, hasa wa Ario na wafuasi wake. Katika mazingira hayo, lengo kuu lilikuwa kwanza kabisa ni kumkiri Kristo Yesu kama Mungu kweli sawa na Baba, halafu kwamba Roho Mtakatifu anastahili kuabudiwa pamoja na Baba na Mwana (Utatu Mtakatifu). Mwaka 2025 Makanisa yataadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu kuadhimishwa kwa Mtaguso wa Nicea. Umoja wa Kanisa ulikuwa hatarini na hivyo pia kutishia amani na usalama hata katika masuala ya kisiasa. Tangu mwanzo, Mababa wa Kanisa wameonesha umuhimu wa Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Kanuni ya Imani ya Nicea-Costantinopoli ndiyo bado inayoyaunganisha Makanisa pamoja na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo. Hili ni tulio litakaloadhimishwa kiekumene.

KANUNI YA IMANI: Nasadiki kwa Mungu mmoja Baba mwenyezi, Muumba wa mbingu na dunia na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Nasadiki kwa Bwana mmoja, Yesu Kristo, Mwanae pekee wa Mungu, aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli, aliyezaliwa, bila kuumbwa, mwenye umungu mmoja na Baba: ambaye vitu vyote vimeumbwa naye. Alishuka kutoka mbinguni, kwa ajili yetu sisi wanadamu, na kwa ajili ya wokovu wetu. Akatwaa mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria, akawa mwanadamu. Akasulubiwa kwa ajili yetu sisi, kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato; akateswa, akafa, akazikwa, siku ya tatu akafufuka, kadiri ya Maandiko, akapaa mbinguni, amekaa kuume kwa Baba. Atakuja tena kwa utukufu, kuwahukumu wazima na wafu, nao ufalme wake hautakuwa na mwisho. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa, pamoja na Baba na Mwana: aliyenena kwa vinywa vya manabii. Nasadiki kwa Kanisa moja, takatifu, katoliki, la Mitume. Naungama ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi. Nangojea na ufufuko wa wafu, na uzima wa milele ijayo. Amina.

Dhana ya Sinodi kama changamoto ya kiekumene: Kardinali Kurt Koch anasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kukazia umuhimu wa watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ni kiini cha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Sinodi ya Kanisa si kama vikao vya Bunge, bali ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa wa kutaka kumsikiliza na kutembea kwa pamoja chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu kama sehemu ya mchakato wa utambulisho wa Kanisa na uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ndio ufafanuzi wa kina uliotolewa na Mtakatifu Paulo VI, Muasisi wa maadhimisho ya Sinodi mara baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Sinodi ni mwaliko kwa waamini kujidhaminisha chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, kwa kuonesha ujasiri wa kitume, unyenyekevu wa Kiinjili na Sala yenye imani, ili kumwachia Roho Mtakatifu kuwaongoza waamini na Kanisa zima kwa ujumla wake. Sinodi ni chombo cha uinjilishaji unaolisaidia Kanisa baada ya kutembea pamoja katika sala, tafakari na mang’amuzi mbali mbali waweze kufikia maamuzi kama ilivyokuwa kwa Mababa wa Mtaguso wa Efeso, walipofikia uamuzi kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu, “Theotokos”.

Mwelekeo wa Kanisa kwa sasa ni dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anakazia ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa; umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene; ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kielelezo cha imani tendaji! Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Juhudi za kichungaji na kitaalimungu zisaidie kuimarisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu majadiliano ya kiekumene, kwa kumpokea Roho Mtakatifu ili kuweza kujifunza mengi kutoka kwa wengine na kuvuna kile ambacho Roho Mtakatifu amepanda ndani yao, ambacho kimekusudiwa kuwa ni zawadi kwa wengine. Kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene na Kanisa la Kiorthodox, Wakatoliki wanaweza kujifunza zaidi maana ya urika wa kiaskofu pamoja na uzoefu wao wa Kisinodi, ili kumpatia nafasi Roho Mtakatifu aweze kuwaongoza katika ukweli na wema.

Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inapewa kipaumbele cha pekee katika majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox, hali inayojionesha katika ngazi kuu tatu; Kanisa mahalia, Kanisa la Kikanda na Kanisa la Kiulimwengu. Hapa mkazo ni kuhusu umoja wa Kanisa ndio changamoto kubwa inayopewa kipaumbele cha kwanza kama ilivyojionesha kwenye Tamko la Ravenna la Mwaka 2007. Tamko hili linagusia umuhimu wa huduma kwa watu wa Mungu. Kardinali Kurt Koch anasema, kuna haja ya kufanya upatanisho wa kiekumene kati ya dhana ya Sinodi na Maisha ya Mkuu wa Kanisa. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki bado ni changa sana ikilinganishwa na Waorthodox. Inawezakana kabisa kutambua dhamana na nafasi ya viongozi wakuu wa Makanisa. Maamuzi yaliyofanywa na Mtaguso wa NICEA wa Mwaka 325 na Mtaguzo wa Calcedonia wa Mwaka 541 ni muhimu sana katika masuala ya uongozi wa Kanisa kwa kutambua kati ya Maaskofu ni nani kiongozi wao mkuu, ili Mwenyezi Mungu aweze kutukuzwa na mwanadamu kutakatifuzwa kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Urika wa Maaskofu ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Kanisa la Kiorthodox kwa upande wake, litapaswa pia kutambua umuhimu wa Urika wa Maaskofu katika ngazi ya kiulimwengu. Maamuzi yaliyofikiwa kwenye Sinodi ya Makanisa ya Kiorthodox huko Creta, Ugiriki mwaka 2016 yanapaswa kuzingatiwa ili kutekeleza wazo la umoja wa Kanisa la Kiulimwengu, kwa kuwa na kiongozi mwenye mamlaka na wala si kiongozi wa heshima tu. Asili ya Fumbo la Ekaristi Takatifu katika dhana ya Sinodi na umuhimu wa wakuu wa Makanisa ni changamoto pevu katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Ukuu wa Askofu wa Roma unaweza kutambulika ikiwa kama chanzo cha tafakari hii, kitajikita katika Ekaristi Takatifu. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wake inapata chanzo na utimilifu wake katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Lengo ni kujenga na kudumisha umoja, ushiriki mkamilifu na hatimaye, kutekeleza utume kama kichocheo na kikolezo cha majadiliano ya kiekumene kutoka katika undani wake.

Waraka wa pamoja kuhusu “Sinodi na Ukuu wa Petro Karne ya kwanza; Kuelekea Uelewa wa pamoja katika Umoja wa Kanisa” ni matunda ya safari ndefu ya majadiliano ya kiekumene iliyotekelezwa na Kamati ya pamoja ya wanataalimungu wa Makanisa haya. Bado kuna mambo mengi anasema Baba Mtakatifu yanayopaswa kufanyiwa tafakari ya kina, lakini “Sinodi” na “Ukuu wa Petro karne ya kwanza” inaweza kuwa ni msingi unaoelekeza jinsi ya Ukuu unavyopaswa kutekelezwa ndani ya Kanisa wakati ambapo Makanisa ya Mashariki na Magharibi yatakapokuwa yamejipatanisha na kuungana kuwa ni Kanisa moja!

Kardinali Koch

 

 

19 January 2021, 15:53