Tafuta

Ratiba elekezi ya utume wa Baba Mtakatifu Francisko kati ya tarehe 24 hadi 25 Januari inaonesha kwamba, mkutano wake na mabalozi na wawakilishi mbalimbali umefutwa kwa sasa! Ratiba elekezi ya utume wa Baba Mtakatifu Francisko kati ya tarehe 24 hadi 25 Januari inaonesha kwamba, mkutano wake na mabalozi na wawakilishi mbalimbali umefutwa kwa sasa! 

Mabadiliko Katika Ratiba Elekezi ya Papa Francisko 24-25 Januari 2021

Ratiba elekezi ilikuwa inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 25 Januari 2021 alikuwa amepanga kukutana na kuzungumza na Mabalozi na wawakilishi wa nchi na Jumuiya za Kimataifa hapa mjini Vatican, lakini zoezi hili limeahirishwa hadi wakati mwingine. Masifu ya Jioni Kufunga Sherehe ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo yataongozwa na Kardinali Kurt Koch.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, amesema kwamba kutokana na sababu zilizoko nje ya uwezo wa Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu, tarehe 25 Januari 2021 kuanzia saa 11:30 jioni kwa saa za Ulaya, hataweza kuongoza Ibada ya Masifu ya Jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, Nje ya Kuta za Roma. Na badala yake, amemteua Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo kuongoza Ibada hii. Itakumbukwa kwamba, hii ni sehemu ya sherehe ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa sanjari na kufunga Juma la 54 la Kuombea Umoja wa Wakristo. Kauli mbiu ambayo imeongoza maadhimisho haya ni “Kaeni katika pendo langu, ili mzae matunda”. Rej. Jn. 15-5-9. Kristo Yesu ndiye Mzabibu wa kweli ni ufafanuzi unaotolewa katika Injili ya Yohane 15:1-17. Hili ni tukio linalohudhuriwa na viongozi wa Makanisa na madhehebu mbali mbali ya Kikristo wanaoishi hapa Roma. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujiunga katika sala hii kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo.

Ratiba elekezi ilikuwa inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 25 Januari 2021 alikuwa amepanga kukutana na kuzungumza na Mabalozi na wawakilishi wa nchi na Jumuiya za Kimataifa hapa mjini Vatican, lakini zoezi hili limeahirishwa hadi wakati mwingine. Hii ni fursa kwa Baba Mtakatifu kutoa dira na mwelekeo wa maisha na utume wa Kanisa katika kipindi cha Mwaka mzima wa 2021, huku akionesha vipaumbele vya Vatican katika kipindi cha mwaka mzima. Baba Mtakatifu Francisko hakuweza kushiriki wala kuongoza Ibada ya Misa Takatifu, Dominika ya Neno la Mungu, Jumapili tarehe 24 Januari 2021 na badala yake, ameongoza Askofu mkuu Salvatore Rino Fischella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya, ambaye pia amesoma mahubiri yaliyokuwa yameandaliwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Ibada hii ya Misa Takatifu. Jumapili tarehe 24 Januari 2021 maarufu kama Dominika ya Neno la Mungu, Baba Mtakatifu ameongoza Tafakari ya Neno la Mungu pamoja na Sala ya Malaika wa Bwana.

Ratiba Elekezi
24 January 2021, 16:29