Tafuta

Chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19: Angalisho kutoka Taasisi ya Kipapa ya Maisha kuhusu matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza kutokana na chanjo ya Virusi vya Corona, COVID-19. Chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19: Angalisho kutoka Taasisi ya Kipapa ya Maisha kuhusu matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza kutokana na chanjo ya Virusi vya Corona, COVID-19. 

Chanjo Dhidi ya Virus Vya COVID-19: Angalisho la Taasisi ya Maisha

Angalisho toka kwa Taasisi ya Kipapa ya Maisha: Matatizo na changamoto zinazotokana na mfumo mzima wa uzalishaji na usambazaji wa chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 na matokeo yake ni kukosekana kwa haki. Kuna haja ya kutafuta njia bora zaidi kwa ajili ya kutoa chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 kwa kuzingatia kanuni ya ukweli, uwazi na ushirikiano wa dhati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, chanjo ni sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu. Kwa njia hii, watu wanajenga udugu na ujirani mwema kwa njia ya chanjo, ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza, ili hatimaye, kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Huu ni utamaduni unaosababisha maafa na utengano! Ujirani mwema ni dhana inayopaswa kufanyiwa kazi, ili kujenga umoja na mafungamano ya kijamii, kitaifa na ndani ya Kanisa katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba, kifo laini pamoja na tabia ya kutowajali wala kuwathamini wengine, umeendelea kukuzwa kutokana na maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19. Maskini, wazee, wakimbizi na wahamiaji wameendelea kuteseka sana kutokana na ugonjwa wa Corona, COVID-19. Kumekuwepo na ongezeko la utoaji mimba kwa madai ya kuwepo na mimba zisizotarajiwa. Tatizo la utoaji mimba ni sehemu ya maisha adili linalogusa utu, heshima na haki msingi za binadamu na hatimaye, inakuwa ni changamoto ya maisha ya kidini kwa kuongozwa na dhamiri nyofu.

Haiwezekani kutumia utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba na kifo laini kuwa ni suluhu ya kumaliza matatizo na changamoto zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Chanjo ni lazima ithibitishwe kuwa salama na yenye ufanisi kwa idadi kubwa ya watu kabla ya kuidhinishwa na kuingizwa kwenye programu za chanjo sehemu mbalimbali za dunia. Ni katika muktadha huu, Taasisi ya Kipapa ya Maisha (Pontificia Academia Pro Vita) iliyoanzishwa tarehe 11 Februari 1994, katika angalisho lake inasema, mchakato wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 unakabiliwa na changamoto nyingi. Haya ni matatizo na changamoto zinazotokana na mfumo mzima wa uzalishaji na usambazaji wa chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 na matokeo yake ni kukosekana kwa haki. Kuna haja ya kutafuta njia bora zaidi kwa ajili ya kutoa chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 kwa kuzingatia kanuni ya ukweli, uwazi na ushirikiano wa dhati.

Chanjo ya Virusi vya Corona, COVID-19 kwa sasa inakabiliwa na matatizo pamoja na ushindani usiokuwa na tija wala mafao kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, “Urbi et Orbi” wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Noeli tarehe 25 Desemba 2020 aliwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumtafakari Mtoto Yesu aliyewawezesha kuwa ndugu wamoja. Baba Mtakatifu anasema, katika kipindi hiki cha historia ya mwanadamu, kimeguswa na kutikiswa kwa namna ya pekee kabisa na janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Hali hii imechangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa uchumi na hivyo kusababisha mwelekeo tenge katika jamii, hali inayodai ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu. Mwenyezi Mungu amewapatia Mwanaye wa pekee, Kristo Yesu, ili aweze kuwa ndugu yao.

Huu ni undugu unaofumbatwa katika upendo unaomwezesha mtu kukutana na jirani zake, licha ya tofauti zao msingi. Kwa njia hii, ataweza kuguswa na mateso na mahangaiko yake, tayari kumkaribia, ili kuweza kumhudumia kama alivyofanya yule Msamaria mwema. Haijalishi kama mtu huyu anatoka katika familia, kabila au dini yake, lakini ni ndugu yake. Mwelekeo huu ndio unaopaswa kuzingatiwa hata katika mahusiano na mafungamano kati ya watu na Mataifa. Haya ni maneno ya kinabii yanayopaswa kusikilizwa na hatimaye, utekelezwe kwa dhati. Nyota angavu ya Bethlehemu iwe ni chanzo cha matumaini mapya na ushirikiano wa Kimataifa, ili watu wengi zaidi waweze kupata chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 kwa kuondokana na uchoyo na utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko. Haki ya huduma bora ya afya, iwe ni kipimo cha upendo unaopaswa kushuhudiwa na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Huu ni wakati wa kushirikiana na kushikamana na wala si kufanya mashindano. Ni muda wa kutafuta suluhu ya kudumu, itakayowawezesha watu wengi zaidi kupata chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Maskini na wahitaji zaidi wapewe kipaumbele cha kwanza.

Hivi karibuni, Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu kwa kushirikiana na Taasisi ya Kipapa ya Maisha (Pontificia Academia Pro Vita), wamechapisha Waraka unaoonesha Umuhimu wa Chanjo na Chanjo Kama Sehemu ya Mafao ya Wengi. Waraka huu ulitoa angalisho dhidi ya chanjo zinazokumbatia utaifa, kwa baadhi ya Mataifa kutaka kuwa na chanjo zake binafsi, kwa kuhakikisha kwamba, zinapata kiasi kikubwa cha dawa ya chanjo kwa ajili ya wananchi wake. Hii ni hatari sana, kwani uzalishaji na usambazaji wa chanjo hii unaweza kujikuta unawanufaisha watu wachache peke yao na hivyo, kutawala soko la chanjo kwa kupanga bei wanayoitaka wao wenyewe hata kama ni kwa hasara ya watu wengi duniani. Uzalishaji mkubwa wa chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 unapaswa kujiekeza kwa kudumisha ushirikiano mwema kati ya Serikali, Makampuni yanayotengeza dawa pamoja na mashirika mbalimbali yanayojihusisha na afya ya binadamu, ili uzalishaji, usambazaji pamoja na utoaji wa chanjo hii uweze kufanyika kwa wakati mmoja sehemu mbali mbali za dunia.

Hii inatokana na ukweli kwamba, watu wanategemeana na kukamilishana. Huko nyuma, mwelekeo huu uliwezekana kwa kuzingatia tafiti mbalimbali. Katika mwelekeo huu pia, kuna haja ya kuanzisha mchakato utakaosaidia uzalishaji, usambazaji na huduma ya chanjo sehemu mbali mbali za dunia kwa kuzingatia kanuni ya auni “the subsidiarity principle”. Lengo ni kuhakikisha kwamba, chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 inawafikia watu wengi kwa wakati mmoja. Hii inatokana na wasi wasi kwamba, baadhi ya Mataifa yenye nguvu ya uchumi kununua kiasi kikubwa cha chanjo na hivyo kusababisha uhaba kwa baadhi ya Mataifa changa zaidi duniani. Mchakato wa ugavi wa chanjo dhidi ya Corona, COVID-19 unahitaji nyeno maalum zitakazotumika ili kufikia lengo linalokusudiwa, kwa kuwawezesha watu wengi zaidi kupata huduma hii. Serikali mbali mbali, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU), pamoja na Shirika la Afya Duniani, WHO yapaswa kuwajibika barabara kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa njia hii, watu wengi kutoka sehemu mbali mbali za dunia wataweza kujisikia kuwa ni sehemu ya familia kubwa ya binadamu!

Chanjo Corona
23 January 2021, 15:14