Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 9 Januari 2021 amepokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Guzman Carriquiry Lecour, Balozi wa Uruguay mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 9 Januari 2021 amepokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Guzman Carriquiry Lecour, Balozi wa Uruguay mjini Vatican. 

Balozi Guzmàn Miguel wa Uruguay Awasilisha Hati za Utambulisho!

Balozi Guzmán Miguel Carriquiry Lecour ni kati ya waamini walei, ambao kwa miaka mingi wamekabidhiwa dhamana maalum katika maisha na utume wa Kanisa. Ameiwakilisha Vatican kwenye mikutano mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa kuhusu familia, dhamana na wajibu wa waamini walei. Amechangia mawazo katika maadhimisho ya Sinodi na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki duniani

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 9 Januari 2021 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Guzmán Miguel Carriquiry Lecour, Balozi mpya wa Uruguay mjini Vatican. Baadaye amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na huo ukawa ni mwanzo wa utume wake wa kidiplomasia mjini Vatican, baada ya kuteuliwa na Serikali ya Uruguay mwezi Julai 2020 kuwa Balozi mpya wa Uruguay mjini Vatican. Balozi Guzmán Miguel Carriquiry Lecour si mgeni sana mjini Vatican kwani tangu mwaka 1971 hadi mwaka 2019 amekuwa akifanya utume wake mjini Vatican kwenye Baraza la Kipapa la Walei wakati huo!

Itakumbukwa kwamba, Balozi Guzmán Miguel Carriquiry Lecour alizaliwa kunako tarehe 20 Aprili 1944 huko Montevideo, Uruguay, ameoa na kubahatika kupata watoto wanne. Kunako mwaka 1970 alitunukiwa shahada ya Uzamivu katika sheria na mwaka 1971 akaandikishwa rasmi kwenye Chama cha Wanasheria wa Uruguay. Kati ya Mwaka 1967 hadi mwaka 1970 aliteuliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Uruguay kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Mawasiliano Jamii nchini Uruguay. Ni mwandishi wa vitabu aliyebobea sana! Kati ya Mwaka 1971 hadi mwaka 1974, Mtakatifu Paulo VI alimteuwa kuwa mtalaam wa kisayansi katika Baraza la Kipapa la Walei.

Kati ya Mwaka 1974 hadi mwaka 1977 aliteuliwa kuwa kati ya viongozi waandamizi wa Baraza la Kipapa la Walei. Kati ya mwaka 1977 hadi mwaka 1982 aliteuliwa kuwa mkuu wa Ofisi, Baraza la Kipapa la Walei. Kati ya mwaka 1982 hadi mwaka 2011 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Katibu mkuu msaidizi, Baraza la Kipapa la Walei. Kati ya Mwaka 2011 hadi mwaka 2014 akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini. Baadaye kati ya mwaka 2014 hadi mwaka 2019 akateuliwa kuwa Makamu wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini.

Na tarehe 9 Januari 2021 amewasilisha hati zake za utambulisho kwa Baba Mtakatifu Francisko kama Balozi mpya wa Uruguay mjini Vatican. Balozi Guzmán Miguel Carriquiry Lecour ni kati ya waamini walei, ambao kwa miaka mingi wamekabidhiwa dhamana maalum katika maisha na utume wa Kanisa. Ameiwakilisha Vatican kwenye mikutano mbalimbali ya Kimataifa kuhusu familia. Amechangia mawazo katika maadhimisho ya Sinodi maalum, Mabaraza pamoja na Mashirikisho ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki hasa Amerika ya Kusini sanjari na kushiriki katika maandalizi ya Maadhimisho ya Siku za Vijana Ulimwenguni tangu kuasisiwa kwake na Mtakatifu Yohane Paulo II.

Balozi Uruguay
09 January 2021, 15:03