Tafuta

Dhamana na wajibu wa Kanisa katika sekta ya elimu: Kuwajengea vijana wa kizazi kipya leo na kesho yenye matumaini. Dhamana na wajibu wa Kanisa katika sekta ya elimu: Kuwajengea vijana wa kizazi kipya leo na kesho yenye matumaini. 

Dhamana ya Kanisa Katika Sekta ya Elimu: Matumaini Kwa Vijana!

Elimu maana yake ni mchakato unaowajengea watu matumaini ya kuondokana na ubinafsi wao; kwa kutambua, kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza, ili hatimaye, kujenga na kudumisha: utamaduni wa ukarimu, mshikamano, mafungamano ya kijamii na hofu ya Mungu. Upyaisho wa mfumo wa elimu utawasaidia kupambana na changamoto na kujenga matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa mkutano wa Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” hivi karibuni, alikazia pamoja na mambo mengine kuhusu: Janga la elimu duniani, maana ya elimu, umuhimu wa kupyaisha mfumo wa elimu duniani na hatimaye, mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika maboresho ya mfumo wa elimu. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi, COVID-19 limepelekea athari kubwa katika sekta ya afya, uchumi, jamii na elimu. Kulihitajika suluhu ya haraka ili wanafunzi waweze kuendelea na masomo yao, huku wakiwa wanaishi kwenye karantini majumbani mwao. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano yamewawezesha wanafunzi wengi kuendelea na masomo, lakini kuna umati mkubwa wa watoto na vijana umebaki nyuma kwa masomo na hili ni janga kubwa katika mfumo wa elimu duniani. Inakadiriwa kwamba, kuna watoto zaidi ya milioni 10 wako hatarini kutoendelea na masomo kutokana na kuyumba kwa uchumi kitaifa na kimataifa. Jambo la kusikitisha zaidi ni kuona kwamba, zaidi ya watoto milioni 250 wenye umri wa kwenda shuleni, hawataweza kupata fursa hii.

Changamoto zilizoibuliwa kwenye sekta ya afya zinapaswa kushughulikiwa kikamilifu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu pamoja na kukazia umuhimu wa kushirikiana na kushikamana katika udugu wa kibinadamu. Elimu maana yake ni mchakato unaowajengea wanafunzi matumaini ya kuondokana na ubinafsi wao; kwa kutambua, kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza, ili hatimaye, kujenga na kudumisha: utamaduni wa ukarimu, mshikamano, mafungamano ya kijamii sanjari na hofu ya Mungu. Upyaisho wa mfumo wa elimu katika ulimwengu mamboleo utawasaidia watu wa Mungu kupambana na changamoto zinazojitokeza kwa wakati huu, ili kujenga leo na kesho yenye matumaini. Elimu ni upendo unaowajibisha na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, ili kuondokana na ubinafsi unaopelekea watu kutokuthaminiana. Kuna haja ya kujenga umoja na mshikamano unaosimikwa katika kipaji cha kusikiliza, kujadiliana na maridhiano kati ya watu! Mabadiliko ya mfumo wa elimu duniani yanapaswa kuwahusisha wadau mbali mbali katika sekta ya elimu, ili kuondokana na ukosefu wa haki jamii; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili hatimaye, kuweza kupambana na umaskini pamoja na tabia ya watu kutowajali wengine.

Baba Mtakatifu anasema, huu ni mchakato fungamanishi unaopania kujenga madaraja yanayowakutanisha watu, ili kuondokana na upweke hasi, kwa kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini. Hali hii itawasaidia vijana wengi kuondokana na ugonjwa wa sonona; utumwa mamboleo, chuki, uhasama, matusi, ukatili pamoja na uonevu mitandaoni. Elimu ni nyenzo msingi inayomwezesha mwanadamu kuyasanifu mazingira yake na kwamba hii ni sehemu ya haki msingi za binadamu, kama ilivyobainishwa na Jumuiya ya Kimataifa kunako mwaka 2000. Haki ya elimu hupatikana kwa juhudi mbalimbali zinazopewa kipaumbele cha kwanza na jamii husika. Lengo ni kuiwezesha jamii kuuelewa ulimwengu kwa undani zaidi, kupata ujuzi, maarifa na stadi zitakazowezesha kuboresha na kudumisha uhai wa jamii sanjari na kukuza: utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Ni katika muktadha huu, Mama Kanisa ameendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika sekta ya elimu ili kuhakikisha kwamba, hata katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, wanafunzi bado wanaendelea kupata elimu kama haki yao msingi. Protokali za kuzuia maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 inapaswa kuzingatiwa kwa kutambua kwamba, shule ni mahali pa salama zaidi, ambapo wanafunzi wanaweza kukua na hatimaye kushiriki kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Yote haya yanabainishwa na Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu katika Jarida la habari za wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia hasa katika kipindi hiki maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Mama Kanisa anakumbusha kwamba, elimu ni sehemu ya haki msingi za binadamu, kumbe, kuna haja kwa wadau mbalimbali wa sekta ya elimu kushirikiana na kushikamana ili kuhakikisha kwamba, wanafunzi wanapata elimu bora na makini. Watoto wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la pekee. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watoto milioni 40 ambao ni wahanga wa utumwa mamboleo. Jumuiya ya Kimataifa katika ulimwengu mamboleo, inakabiliana na uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu kutokana na: vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kidini na kikabila. Kuna ongezeko kubwa la kiwango cha umaskini wa hali na kipato; uhalifu unaofanywa na magenge ya kitaifa na kimataifa pamoja na kuendelea kuibuka kwa mifumo mipya ya utumwa mamboleo pamoja na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake. Yote haya ni mambo yanayonyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Biashara ya binadamu na viungo vyake ni donda ndugu katika ulimwengu mamboleo.

Nchini Australia, Kanisa linaendelea kupambana na biashara haramu ya binadamu, kwa kuhakikisha kwamba, shule na mazingira ya kufundishia yanakuwa rafiki kwa wanafunzi. Watu wanahimizwa kususia bidhaa zinazozalishwa na makampuni ambayo yamekubuhu katika uvunjwaji wa haki msingi za binadamu, ili kuonesha kwamba, wanajali na kuguswa na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu. Kwa upande mwingine, Kanisa nchini Rwanda linaendelea kujielekeza katika ufundishaji wa elimu ya haki jamii na walengwa zaidi ni wakimbizi na wahamiaji kutoka DRC. Takwimu zinazonesha kwamba, mtu anaweza kuishi kwenye kambi ya wakimbizi au wahamiaji kwa zaidi ya miaka 17. Kumbe, haki elimu inapewa kipaumbele cha pekee sanjari na kuhakikisha kwamba, haki, ustawi na maendeleo ya vijana hawa yanazingatiwa, bila kusahau usawa katika mambo msingi. Walimu wanafundishwa namna ya kuwasaidia wanafunzi wenye matatizo makubwa darasani, ili kuwaundia mazingira ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Awamu ya tatu ya mkakati huu inayotekelezwa katika kipindi cha mwaka 2021 ni kuwawezesha wanafunzi, walimu na wazazi kujenga mafungamano ya kijamii, kwa kuhakikisha kwamba, wazazi wanahusishwa kikamilifu katika malezi, makuzi na majiundo ya watoto wao. Wayesuit nchini Kenya kwa kutumia Idara ya Huduma kwa Wakimbizi, “Jesuit Refugee Servives, Jrs, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ndani na nje ya Kenya, wanatoa ufadhili kwa wakimbizi vijana 21 kupata elimu ya juu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, elimu ni sehemu ya mchakato wa matumaini unaojielekeza tangu sasa kwa ajili ya kesho iliyo bora zaidi, kwa kuvunjilia mbali utandawazi usioguswa na mahangaiko ya wengine na badala yake kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu!

Haki Elimu

 

17 December 2020, 14:13