Tafuta

Vatican News
Caritas Internationalis imezindua kampeni ya Noeli kwa Mwaka 2020 kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa: chakula, malazi, usalama, utu na heshima ya binadamu. Caritas Internationalis imezindua kampeni ya Noeli kwa Mwaka 2020 kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa: chakula, malazi, usalama, utu na heshima ya binadamu.  (ANSA)

Caritas Internationalis: Kampeni ya Noeli kwa Mwaka 2020: Upendo

Caritas Internationalis, limezindua kampeni ya Kipindi cha Noeli kwa Mwaka 2020, kwa kuwataka wasamaria wema kuchangia jitihada za Caritas ili kuweza kutoa chakula, makazi na usalama kwa wakimbizi na wahamiaji kama sehemu ya unafishaji wa haki, afya na upendo kwa maskini na wahitaji zaidi. Kampeni ya Mwaka 2020 inajielekeza zaidi katika mapambano dhidi ya COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, limezindua kampeni ya Kipindi cha Noeli kwa Mwaka 2020,  kwa kuwataka wasamaria wema kuchangia jitihada za Caritas ili kuweza kutoa chakula, makazi na usalama kwa wakimbizi na wahamiaji kama sehemu ya unafsishaji wa haki, afya na upendo kwa maskini na wahitaji zaidi. Kampeni ya Mwaka 2020 inajielekeza zaidi katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Licha ya kusababisha maafa makubwa kwa watu, gonjwa hili hatari limekuwa pia ni chanzo cha ongezeko la kiwango cha umaskini na ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula duniani.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mahangaiko ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za duniani, ameanzisha Mfuko wa Dharura unaosimamiwa na kuratibiwa na Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kwa ajili ya kuwasaidia watu wa Mungu, ambao wameathirika sana kutokana na maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Caritas Internationalis ni mdau mkubwa katika kuchangia “Mfuko wa COVID-19 Response Fund”. Ni katika muktadha huu, Mashirika 38 ya Caritas kutoka sehemu mbalimbali za dunia yamekuwa mstari wa mbele kuwasaidia watu zaidi ya milioni 13.7 walioathirika zaidi na Virusi vya Corona, COVID-19.

Hawa ni watu kutoka Belarus, Ethiopia, Yordan, Rwanda, Iraq, Ugiriki, Nigeria, Pakistani, Lebanon, Ukraine pamoja na DRC. Caritas Internationalis imetekeleza miradi kadhaa ambayo imewasaidia watu wa Mungu kupata maji safi na salama; chakula pamoja na mahitaji msingi ya binadamu. Caritas imekuwa ni msaada mkubwa kwa wakimbizi na wahamiaji huko Afrika ya Kusini na Angola. Katika Kampeni hii ya Noeli kwa Mwaka 2020, Caritas inapenda kujielekeza zaidi  kugharimia miradi tisa inayotekelezwa huko Armenia, Burundi, Cambodia, Eritrea, Georgia, Haiti, Liberia, Msumbiji pamoja na Sierra Leone. Lengo ni kusaidia kugawa vifaa tiba kwa waathirika wa COVID-19, kutoa malazi salama kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na kuhakikisha kwamba, watoto wa wakulima vijijini wanaendelea na masomo kwa kutambua kwamba, walau asilimia 45% ya watoto wanaoishi vijijini katika Nchi zinazoendelea hawana uwezo wa kupata internet kwa ajili ya masomo.

Caritas Internationalis inasema Kampeni Noeli kwa Mwaka 2020 inapania kuwashirikisha watu wa Mungu furaha ya Noeli kwa kuhakikisha kwamba: haki, afya na upendo vinatawala katika akili na nyoyo za watu. Katika muktadha huu, Caritas inataka kuhakikisha kwamba, haki msingi za watu hawa zinalindwa na kuheshimiwa. Yaani hii ni haki ya kupata: chakula bora, maji safi na salama; makazi pamoja na elimu bora. Gonjwa hatari la COVID-19 limeanika udhaifu wa binadamu na kwamba, binadamu wanategemeana na kukamilishana. Kumbe, kuna haja ya kushikamana na kuwajibika kwa upendo, ili kutoa faraja kwa waathirika wa COVID-19. Kama Wasamaria wema, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuwa chemchemi ya faraja na upendo kwa watu wote waliopondeka na kuvunjika moyo. Wawe ni mwanga wa matumaini mapya kwa wote wanaotembea katika giza na hali ya kukata tamaa katika maisha. Huu ndio muujiza wa fadhila ya upendo!

Caritas Noeli 2020

 

 

 

16 December 2020, 14:21