Tafuta

Vatican News
Malekezo muhimu kuhusu Vyo Vikuu Katoliki na Taasisi Malekezo muhimu kuhusu Vyo Vikuu Katoliki na Taasisi 

Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki kuzindua maelekezo mapya matatu

Sheria zinahusu taasisi za elimu ya juu kuhusu mkusanyiko, ujumuishwaji, na ushirikiano. Kwa mujibu wa Katibu wake Askofu Mkuu Vincenzo Zani amesema ni kutaka kukabiliana na changamoto za leo na ili mfumo wa masomo ya Kanisa ufuate msukumo wa Kanisa kwa roho mpya ya utume wa kimisionari.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Katika Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki limefafanua kuhusu maelekezo mapya matatu  yanayohusu elimu. Hayo ni maelekezo matatu yanayozaliwa mara baada ya Katiba ya Kitume Veritatis Gaudium kuhusu Vyuo vikuu na Vyuo vya Kikanisa, iliyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko mnamo tarehe 8 Desemba 2017. Hati hizo zinakusudia kujibu hitaji la kufanya mtandao katika ukweli wa taasisi za elimu ya juu ya Kanisa linalotoka nje na la utume wa kimisionari.  Ni shughuli inayohitajika katika taaluma zinazozingatiwa kwenye masomo ya Kanisa pia kwa taasisi zenyewe. Ni maelekezo yanakusudia kutoa maendeleo ya Taasisi hizi na kwa usambazwaji wao rahisi katika sehemu mbali mbali za ulimwengu.

Nyaraka za Baraza la Kipapa la Elimu ya Katoliki zinazingatia maneno matatu muhimu kwanza kuhusu mkusanyiko, pili juu ya ujumuishaji na  tatu ushirikiano wa Taasisi nyingine. Ni mabadiliko matatu muhimu na ambayo lazima yote yawasilishwe kwa uamuzi wa makao makuu ya Vatican na yatolewe kupitia Hati ambayo ni halali kwa miaka 5 (ad quinquennium experimenti gratia), na ambayo inaweza kupyaishwa kila wakati kwa miaka mingine  5 au kufutwa. Maelezo hayo yataanza utumika siku ya kwanza ya mwaka wa masomo 2021-2022 au mwaka wa masomo wa 2022, kulingana na kalenda ya masomo ya kanda tofauti.

Kwa mujibu wa Katibu wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki Askofu Vincenzo Zani, ameelezea nini maana ya Tassisi za Masomo ya juu kuhusu mabadiliko hayo na kwamba: “Tuna zaidi ya taasisi 500 za Kanisa, 120 ni vyuo vya Kikanisa ambavyo ni vya Taalimungu , Falsasa, sheria ya kanoni au sheria ya Kanisa  na vitivo vingine,  vile vile  tuna taasisi karibu 400 zilizoshirikishwa, zilizojumuishwa na zinazoungana.  Inamaanisha nini?

Kwa kufafanua amesema “ Inamaanisha kuwa vitivo vya Kanisa vina mfumo wa masomo ambayo ni sawa na ule wa raia, ambapo ni kwamba, wamepangwa katika mizunguko mitatu ya masomo. Mzunguko wa kwanza huisha na jina la  Shahada ya kwanza (baccalaureato) ya pili Shahada ya uzamili (licenza) na tatu Shahada ya uzamivu(Dottorato). Kiukweli, tuna vyuo vikuu 120 lakini ulimwenguni kote tuna taasisi zingine zote ambazo zimeunganishwa au kujumuishwa au kuingizwa. Taasisi zinazohusiana zina mzunguko wa kwanza tu na badala yake Taasisi za jumla haziwezi kutoa shahada ya kwanza tu (Bacalaureato) bali pia shahada ya Uzamili (Licenza), wakati taasisi zilizojumuishwa, ambazo ni chache sana na ni maalum, hutoa tu mzunguko wa pili au wa tatu. Taasisi hizi zinarejea katika Vyuo vikuu, kwa maana hiyo viko  chini ya jukumu la vitivo, lakini kwa kupyaisha mfumo  mzima ulio mpya wa masomo, hatua kwa hatua tunakubali sheria pia kwa taasisi ambazo zimeunganishwa na vitivo”.

Askoufu Zani aidha amebainisha: “Uzuri ni kwamba kanuni hizi zilikuwa zimeandikwa kila wakati katika Kilatini na kwa wakati huu tunapaswa kutumia lugha zote za kisasa na juu ya yote tunapaswa kuzingatia kuongezeka kwa ubora katika taasisi. Hizi ni dalili halisi ambazo zinapaswa kutolewa kuhusu waalimu, sifa wanazopaswa kuwa nazo. Kwa kuwa taasisi zilizojumuishwa sehemu kubwa ni seminari kuu, kanuni pia zinafanya tofauti kuhusu malezi ya makuhani wa siku zijazo na wa kitawa. Uundaji wao unamaanisha kurejea katika Hati ya Ratio Fundamentalis, ya uwezo wa Baraza la Kipapa la Wakleri, na hivyo tunafuata masomo na kwa maana hiyo tunaelekeza kwa seminari ambapo inasemekana kuwa ni vizuri kuweka usimamizi na mafunzo yote ya semina mbali na masomo ambayo badala yake yanataja kuwa vitivo vya Kanisa.”

10 December 2020, 16:12