Tafuta

Angalisho kuhusu Maadhimisho ya Domenika ya Neno la Mungu kwa Mwaka 2021 Angalisho kuhusu Maadhimisho ya Domenika ya Neno la Mungu kwa Mwaka 2021 

Angalisho Kuhusu Maadhimisho ya Domenika ya Neno la Mungu 2021

Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti za Kanisa limetoa angalisho kuhusu Maadhimisho ya Domenika ya Neno la Mungu katika maisha ya Wakristo. Katika hija ya maisha yao hapa duniani, wanarutibishwa na Kristo Yesu kwa Neno la Sakramenti za Kanisa. Hivyo waamini wajenge utamaduni wa kupenda Biblia Takatifu, ili kuwasha nyoyo zao na moto wa Roho Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake Binafsi Motu Proprio: “APERUIT ILLIS”, iliyochapishwa kunako tatehe 30 Septemba 2019, alianzisha rasmi Maadhimisho ya Domenika ya Neno la Mungu, au Jumapili ya Neno la Mungu inayoadhimishwa Jumapili ya Tatu ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Maadhimisho haya ni matunda ya Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu na pia yana mwelekeo wa kiekumene, kwani huu ni wakati wa kuombea Umoja wa Wakristo. Kristo Yesu kabla ya kupaa kwenda mbinguni “Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na Maandiko” Lk. 24:45 Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Hati ya “Dei verbum” yaani “Neno la Mungu”, wanafafanua kwa kina maumbile na maana ya ufunuo; urithishaji wa ufunuo wa Mungu; Uvuvio wa Kimungu na ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu, Agano la Kale na Agano Jipya. Neno la Mungu ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa sanjari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Umoja wa Wakristo upate chimbuko lake kwa kusikiliza Neno la Mungu, linalofafanuliwa na wachungaji, kiasi kwamba, hata Mahubiri yanachukuliwa kuwa kama “Kisakramenti” muda muafaka wa kufafanua uzuri wa Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya waamini.

Makatekisita, wafundwe kikamilifu, ili wawasaidie waamini kukua katika imani kama ilivyokuwa kwa wale wafuasi wa Emmau, waliobahatika kufafanuliwa Maandiko Mtakatifu na Kristo Yesu alipokuwa anatembea pamoja nao njiani. Neno la Mungu lina utajiri mkubwa na amana ya kufundishia. Ni muhtasari ya maisha ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chemchemi ya imani na ukweli wa maisha na Fumbo la Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo. Neno la Mungu linafafanua historia ya wokovu, linabainisha maisha ya kiroho na kanuni ya Fumbo la Umwilisho. Baba Mtakatifu anawataka waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao! Neno la Mungu linatenda kazi ndani ya yule anayelisikiliza kwa makini, kiasi cha kumwajibisha kuwashirikisha wale wote anaokutana nao, ili kujenga na kudumisha umoja na mafungamano ya watoto wa Mungu.

Neno la Mungu ni chemchemi ya upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma kwa akina Lazaro wanaoendelea kuteseka sehemu mbali mbali za dunia hata katika ulimwengu mamboleo, changamoto na mwaliko wa “kufyekelea mbali ubinafsi na uchoyo”, ili kujenga na kudumisha umoja, ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, tukio la Yesu kugeuka sura mbele ya wafuasi wake, akaonekana akizungumza na Musa na Elia, ni ushuhuda wa utimilifu wa Sheria na Unabii. Maandalizi makini ya kupambana uso kwa uso na Kashfa ya Msalaba yaani: Mateso, Kifo na hatimaye, Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Katika mchakato mzima wa kusoma, kusikiliza, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya waamini, Bikira Maria anabaki kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kumwilisha Heri za Mlimani; muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu katika maisha yake.

Huu ni mwaliko wa kusikiliza Neno la Mungu na kulihifadhi katika sakafu ya nyoyo za waamini. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Barua hii binafsi “Motu Proprio” “Aperuit Illis” inayoanzisha “Domenika ya Neno la Mungu” itakayokuwa inaadhimishwa kuanzia sasa kila mwaka, Jumapili ya III ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa kwa kusema kwamba, Neno la Mungu li karibu sana “Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya.” (Kumb. 30:14). Ni katika muktadha huu, Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti za Kanisa limetoa angalisho kuhusu Maadhimisho ya Domenika ya Neno la Mungu katika maisha ya Wakristo. Katika hija ya maisha yao hapa duniani, wanarutibishwa na Kristo Yesu kwa Neno na Sakramenti za Kanisa. Hivyo waamini wajenge utamaduni wa kupenda Biblia Takatifu, ili kuwasha nyoyo zao na moto wa Roho Mtakatifu, vinginevyo watakuwa baridi na macho yao kugubikwa na upofu wa kila aina. Kristo Yesu ni kiini na utimilifu wa Maandiko Matakatifu. Maadhimisho ya Domenika ya Neno la Mungu yawasaidie waamini kufahamu mambo msingi yanayoyolizunguka Neno la Mungu linalotangazwa katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na Visakramenti vyake pamoja na Sala ya Kanisa.

Neno la Mungu katika vipindi mbalimbali vya Kanisa limepangwa ili kuwasaidia waamini kuweza kuisoma Biblia yote katika kipindi cha Miaka mitatu. Kumbe, maadhimisho ya Domenika ya Neno la Mungu yapewe uzito unaostahili kwa kuhakikisha kwamba, waamini wengi zaidi wanashiriki kikamilifu. Wahudumu wa Neno la Mungu ambao kimsingi ni Wakleri wahakikishe kwamba, kwa njia ya mahubiri yao yaliyoandaliwa kwa umakini mkubwa, wanawasaidia waamini kufafanua Neno la Mungu, kwa kutumia nyenzo zinazoshahuriwa na Mama Kanisa. Waamini wapewe nafasi ya kukaa kimya kidogo, ili kutafakari na hatimaye, kuzamisha ndani mwao yale waliyoyasikia.

Wakleri wajenge utamaduni wa kupenda kulisoma na kulitafakari Neno la Mungu. Mimbari ya Neno la Mungu ipewe heshima yake. Maadhimisho ya Domenika ya Neno la Mungu iwe ni fursa ya kufanya semina mbalimbali kama sehemu ya majiundo endelevu ya Maandiko Matakatifu: Zaburi na Tenzi zinazotumika katika Sala za Kanisa kwa Masifu ya Asubuhi na Jioni. Vitabu vya Liturujia viheshimiwe na kutumiwa kikamilifu. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume: "Scripturae Sacrae Affectus" Yaani “Waraka wa Kitume Juu ya Upendo Kwa Maandiko Matakatifu, Miaka 1600 Tangu Alipofariki Dunia Mtakatifu Jerome” anabainisha kwamba, Mtakatifu Jerome Padre na Mwalimu wa Kanisa aliyeweka Maandiko Matakatifu kuwa kiini cha maisha yake, awasaidie waamini kupyaisha ndani mwao ari, moyo na upendo wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Maandiko Matakatifu katika uhalisia wa maisha yao. Waamini wajenge utamaduni wa kujadiliana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Maandiko Matakatifu.

Katika Waraka huu, Baba Mtakatifu Francisko anachambua: Historia na mchango wa Mtakatifu Jerome katika Maandiko Matakatifu, Hekima ya Mtakatifu Jerome inayofumbatwa katika ushuhuda wake kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; Upendo kwa Maandiko Matakatifu, Masomo ya Maandiko Matakatifu yanayohitaji mwongozo makini ili kuweza kuyatafakari na hatimaye, kuyatafsiri na kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha ya mtu. Mchango wa Mtakatifu Jerome katika kutafsiri na kupanga Biblia ya Kilatini, Vulgata; Tafsiri yake kama sehemu ya utamadunisho. Mtakatifu Jerome na Kiti Kitakatifu cha Mtakatifu Petro. Mwaliko wa kupenda kile alichopenda Mtakatifu Jerome, yaani Maktaba ya Maandiko Matakatifu.

Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti za Kanisa katika Angalisho la Maadhimisho ya Domenika ya Neno la Mungu linasema kwamba, linapenda kukazia tena umuhimu wa Maandiko Matakatifu katika maisha ya waamini, umuhimu wa kupata mwangwi wa Maandiko Matakatifu katika maadhimisho ya Liturujia kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kina na Mwenyezi Mungu. Ikumbukwe kwamba, Neno la Mungu linatangazwa na kuadhimishwa kwa hali ya juu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu na hivyo linakuwa ni rutuba tosha ya maisha ya kiroho yanayowaimarisha Wakristo kujisadaka kama sehemu ya ushuhuda wa Injili katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku!

Domenika ya Neno la Mungu

 

19 December 2020, 16:32