Tafuta

2020.11.16 Kardinali  Raúl Eduardo Vela Chiriboga 2020.11.16 Kardinali Raúl Eduardo Vela Chiriboga 

Papa atuma salam za rambi rambi kufuatia na kifo cha Kard. Vela Chiriboga

Jumanne tarehe 17 Novemba 2020,Papa Francisko ametuma salamu za rambi rambi kufuatia kifo cha Kardinali Raúl Eduardo Vela Chiriboga,mwenye umri wa miaka 86,aliyekuwa Askofu Mstaafu wa Jimbo Kuu katoliki la Quito nchini Ecuador..Anamkumbuka kwa jitihada zake za kichungaji katika Kanisa hilo na kumwombea avikwe taji la utukufu usioisha.Misa ya mazishi imefanyika tarehe 17 Novemba katika Kanisa Kuu ya Quito.

Na Sr. Angela Rwezaula- Vatican

Tarehe 15 Novemba 20200, Kardinali Raúl Eduardo Vela Chiriboga, aliyekuwa Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo kuu Katoliki la Quito, amefariki dunia. Alikuwa na miaka 86, ambapo Baraza la Maaskofu mahalia wametoa taarifa, huku wakiomba waamni wasali kwa ajili ya roho ya marehemu na kutaja kifungu cha Injili ya Matayo kuhusu “mtumishi mwema na mwaminifu wa Bwana (Mt 25, 23). Kufuatia na kifo hicho Papa Francisko ametuma telegram ya salam za rambi rambi kwa Askofu Mkuu Alfredo José Espinoza Mateus, S.D.B. wa jimbo Kuu la Quito, akionesha masikitiko  ya kuondokewa na mtumishi wa Mungu huyo huku akimwomba Askofu Mkuu Espinosa amfikishie salam zake za rambi rambi kwa wanafamilia wa marehemu na jumuiya nzima ya Kanisa. Papa amekumbuka juu ya shughuli za kichungaji alizotenda katika uzima wake kwa miaka mingi na uaminifu wake kwenye huduma ya Mungu na kwa Kanisa. Anaiombea roho ya marehemu ipumzike kwa amani ili Bwana aweze kumvisha taji la utukufu usioishai. Kwa waamini wote wa Mungu anawabariki kwa Baraka ya Kitume kama ishara yamatumaini kikristo katika Bwana mfufuka.

Misa ya Mazishi ya marehemu Askofu Mkuu imefanyika tarehe 17 Novemba saa 4.00 katika Kanisa kuu la Quito nchini Equador. Marehemu Kardinali Raúl Eduardo alizaliwa tarehe 1 Januari 1934 akiwa ni mtoto wa tano kati ya tisa na baada ya kumaliza diploma ya masomo ya juu katika Taasisi ya Kisalesiano, mji wake, alijiunga katika Seminari Kuu ya Quito mnamo mwaka 1951. Aliendelea na mafunzo yake ya kitaalimungu, kichungaji na kiliturujia hata nje ya nchi ya Ecuador, kwa namna ya pekee katika miji wa  Bogotá, Colombia, Madrid, Uhisania na Buenos Aire nchini Argentina

Alipewa daraja la upadre mnamo tarehe 28 Julai 1957 na mwisho wa miaka ya 60 akawa mkurugenzi wa Caritas ya Riobamba. Alishirikiana  na huduma ya kichungaji kwa ajili ya watu asilia na kuunda taasisi ya Fatima kwa ajili ya elimu kwa vijana. Kunako mwaka 1968 akateuliwa kuwa katibu msaidizi wa Baraza la maaskofu nchini Equador, miaka miwili baadaye akawa katibu Mkuu. Baada ya kuwa Askofu msaidizi wa Guayaquil kunako tarehe 20 Aprili 1972,aliwekwa wakfu wa kiaskofu tarehe 21 Mei mwaka huo huo na wakati tarehe 29 Aprili 1975 akachaguliwa kuwa Askofu wa Azogues. Mnamo Februari 1979 alishiriki kama mwakilishi wa Kanisa la Equador katika Mkutano mkuu wa Mabaraza ya Maaskofu wa Amerika ya Kusini, uliofanyika huko Puebla ya  los Angeles, na wakati mwaka  1981 hadi 1988 alikuwa mjumbe katika Baraza la Maaskofu wa Amerika ya Kusini (Celam).

Tarehe 21 Machi 2003 aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Quito mahali ambapo alianzisha mpango ambao ulikuwa unawajibisha maparokia yote kujikita katika elimu ya vijana. Amekuwa na umakini zaidi katika mafunzo ya vijana makuhani, hasa kwa kuanzisha kozi maalum kwa ajili ya makuhani wapya. Alifungua pia kliniki inayotoa huduma kwa mapadre. Tarehe  11 Septemba 2011 akiwa na umri wa miaka 76 aliwakilisha maombi ya kung’atuka katika huduma za kichungaji kwenye jimbo kuu la quito na tarehe 20 Novemba mwaka huo huo Papa mstaafu Benedikto VI akamteua kuwa katika Baraza la Makardinali na kupewa Kanisa la Mama wa njia mjini Roma. Mwaka 2013 alishiriki katika uchaguzi wa Papa Francisko.

17 November 2020, 14:23