Tafuta

UNESCO: Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa: Utu, heshima, haki msingi za binadamu, uraia, ekolojia, mshikamano na maendeleo fungamani ya binadamu. UNESCO: Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa: Utu, heshima, haki msingi za binadamu, uraia, ekolojia, mshikamano na maendeleo fungamani ya binadamu. 

UNESCO: Mkataba Wa Mfumo Mpya Wa Elimu Kimataifa 2020

UNESCO ina mpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kujipambanua katika mchakato wa ujenzi wa haki na amani duniani kwa njia ya mfumo mpya wa elimu pamoja na kutambua juhudi kubwa zinazotekelezwa na UNESCO hasa katika: Kusimamia utu, heshima na haki msingi za binadamu; uraia, ekolojia, mshikamano sanjari na maendeleo fungamani ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” ni mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko, ili kujenga mfumo wa elimu unaojikita katika msingi wa elimu fungamanishi. Lengo ni kuwasaidia vijana kujizatiti zaidi katika elimu fungamanishi inayowataka vijana wa kizazi kipya kuwa wasikivu, wajenzi wa haki, amani, umoja na udugu wa kibinadamu katika usawa! Baba Mtakatifu anakazia mfumo wa elimu itakayosaidia pia kuleta Mfumo Mpya wa Uchumi Duniani unaojikita katika wongofu wa kiekolojia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kimsingi mchakato wa mabadiliko katika mfumo wa elimu duniani unapaswa kuwahusisha watu wote ili kuunda “kijiji cha elimu”, mahali ambapo watu wote, kadiri ya dhamana zao, wanashiriki wajibu wa kuunda mtandao ambao ni wazi katika ujenzi wa mafungamano ya kibinadamu, kwani kila mtu anakuwa na wajibu wa kuchangia katika mchakato wa maboresho ya elimu!

Bi Audrey Azoulay, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa Mkutano wa Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education”, Alhamisi, tarehe 15 Oktoba 2020 uliokuwa unaadhimishwa kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran, kilichoko mjini Roma, amempongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kujipambanua katika mchakato wa ujenzi wa haki na amani duniani kwa njia ya mfumo mpya wa elimu pamoja na kutambua juhudi kubwa zinazotekelezwa na UNESCO hasa katika: Kusimamia utu, heshima na haki msingi za binadamu; uraia,  ekolojia, mshikamano sanjari na maendeleo fungamani ya binadamu. Elimu kimsingi ni kwa ajili ya mafao ya wengi na ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaoheshimu, kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko katika nyaraka zake mbali mbali.

Elimu isaidie mapambano dhidi ya ukosefu wa haki na usawa wa kijamii. Katika ulimwengu mamboleo, kuna zaidi ya wanafunzi bilioni 1.6 ambao wamenyimwa haki ya kupata elimu bora kutokana na ukosefu wa usawa wa kijamii. Nchi changa zaidi duniani zimeshindwa kuwekeza walau asilimia 40% katika maboresho ya sekta ya elimu katika nchi zao. Zaidi ya asilimia 80% ya wanafunzi kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara Barani Afrika hawana uwezo wa kutumia internet majumbani mwao. Haya ni matokeo ya utandawazi wa ubinafsi na uchoyo; vita, kinzani na mipasuko ya kijamii dhidi ya wakimbizi na wahamiaji duniani bila kuwasahau wanawake wanaonyanyasika chini ya mfumo dume! Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limedhihirisha udhaifu wa jamii nyingi duniani, kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika dhamana ya ujenzi wa mfumo mpya wa elimu kwa jamii kadiri ya matamanio ya Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa ambao kimsingi ni shirikishi na unamwambata mtu mzima: kiroho na kimwili. UNESCO imepewa dhamana na Jumuiya ya Kimataifa kuratibu elimu, utamaduni, michezo, tafiti za kisayansi pamoja na mawasiliano.

UNESCO inaunganisha nchi wanachama 193 na katika sera na mikakati yake, inapenda kujikita katika elimu shirikishi na maendeleo fungamani. Kumbe, Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” ni sehemu ya vinasaba vya UNESCO katika mchakato wa ujenzi wa historia, utu, haki, amani, lakini zaidi elimu. UNESCO inaunganisha wadau wa elimu 150 katika nchi wanachama 70, ili kuendeleza na kuunga mkono juhudi za elimu sehemu mbali mbali za dunia pale inapowezekana. Dhamana hii inatekelezwa kwa njia malengo ya muda mrefu na mfupi; kwa kuheshimu na kuthamini tofauti zinazojitokeza; ili kupambana na maamuzi mbele, ili kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu pamoja na ujenzi wa utamaduni wa amani na kuheshimiana. UNESCO pia inaendelea kutoa elimu juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kumbe, elimu bora ni amana, utajiri na mafao ya familia kubwa ya binadamu, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga kuanzia sasa hadi kufikia mwaka 2050 na kuendelea kama inavyofafanuliwa kwenye Mkataba wa Elimu kati ya Ethiopia na UNESCO.

Bi Audrey Azoulay, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO anasema, Shirika lake linaona fahari kubwa sana kuwa kati ya wadau wa Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” ambao umetiwa mkwaju, tarehe 15 Oktoba 2020. UNESCO inataka kujikita katika ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika: Usawa, mshikamano; utu na heshima ya binadamu kwa njia ya ushirikiano wa Kimataifa, kwa elimu kutoa mng’ao wa pekee katika mshikamano wa utu wa kibinadamu!

UNESCO Elimu

 

15 October 2020, 15:15