Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya 94 ya Kimisionari Ulimwenguni Kwa Mwaka 2020: Mambo msingi kama yalivyofafanuliwa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu! Maadhimisho ya Siku ya 94 ya Kimisionari Ulimwenguni Kwa Mwaka 2020: Mambo msingi kama yalivyofafanuliwa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu! 

Maadhimisho Siku Ya 94 ya Kimisionari Duniani 2020: Utume!

Viongozi hawa wamefafanua kiini cha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika historia, maisha na wito wa kila mwamini katika ulimwengu mamboleo. Kazi mbali mbali za kimisionari zinazotekelezwa na Mashirika ya Kipapa katika utume wa Makanisa mahalia pamoja na Mfuko wa Dharura ulioanzishwa na Papa Francisko ili kupambana na Virusi vya Corona, COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 94 ya Kimisionari Ulimwenguni, Jumapili tarehe 18 Oktoba 2020 yanaongozwa na kauli mbiu: “Mimi hapa, nitume mimi” Isa. 6:8. Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, akiwa ameambatana na Askofu mkuu Giampietro Dal Toso, Katibu Mwambata, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa pamoja na Padre Tadeusz J. Nowak, OMI, Katiku mkuu wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za kimisionari, Ijumaa tarehe 16 Oktoba 2020 wamewasilisha Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 94 ya Kimisionari Ulimwenguni. Viongozi hawa wamefafanua kiini cha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika historia, maisha na wito wa kila mwamini katika ulimwengu mamboleo. Kazi mbali mbali za kimisionari zinazotekelezwa na Mashirika ya Kipapa katika maisha na utume wa Makanisa mahalia pamoja na Mfuko wa Dharura ulioanzishwa na Papa Francisko ili kupambana na Virusi vya Corona, COVID-19.

Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, anasema maadhimisho ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni ni chemchemi ya furaha na matumaini hata kama bado watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia wanapambana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Nimtume nani? Ni mwaliko kutoka kwenye moyo wa huruma wa Mwenyezi Mungu unaotoa changamoto kwa watu wa Mungu kushikamana, kushirikiana na kufarijiana kwa sababu wote wanasafiri katika boti moja. Katika muktadha huu,  waamini wanaitwa kutoka katika ubinafsi wao kwa ajili ya upendo kwa Mungu na jirani kama fursa makini ya kushirikishana, nafasi ya huduma pamoja na kuombeana. Maadhimisho ya Mpango Mkakati wa Kimisionari wa Mwezi Oktoba 2019 yaliongozwa na kaulimbiu: “Umebatizwa na umetumwa kutangaza Injili: Kanisa la Kristo katika Utume ulimwenguni kote”.

Sasa waamini wanapaswa kumwilisha wito huu katika uhalisia wa maisha yao kwa kusema, “Mimi hapa, nitume mimi” Isa. 6:8. Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu aliyetumwa na Baba yake wa mbinguni na kuongozwa na Roho Mtakatifu, vivyo hivyo, waamini pia wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia upendo wa Mungu kwa watu wote, lakini zaidi zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ndiyo maana halisi ya kufanya mapenzi ya Mungu kadiri ya Mpango wa ukombozi. Waamini hawana sababu ya kuogopa kwani utume wa Kanisa unasonga mbele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, changamoto na mwaliko wa kusikiliza kwa makini sauti ya Roho Mtakatifu na hatimaye, kumwachia nafasi ya kuweza kuwaongoza, kwa sababu hii ni nguvu salama na yenye uhakika! Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wote wanahamasishwa kujisikia kuwa ni wadau muhimu sana katika utume wa Kanisa na hivyo wanapaswa kujibu kwa uhakika na kusema“Mimi hapa, nitume mimi” Isa. 6:8.

Baba Mtakatifu anawachangamotisha waaamini  kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo; kutangaza Injili ya Wokovu unaoletwa na Kristo Yesu, ili kushiriki maisha ya Kimungu katika Roho Mtakatifu, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Utume wa Kanisa hauna budi kugusa na kuambata medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, ili hatimaye, kumwokoa mwanadamu na kutunza kazi ya uumbaji. Waamini wanapaswa kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaliko na changamoto ya kimisionari anayowapatia, ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, anasema, waamini wanaweza kushiriki utume huu kwa njia ya sala, sadaka na tafakari. Wanaweza kushiriki pia kwa hali na mali, ili kusaidia na kuenzi shughuli mbalimbali za kimisionari zinazotekelezwa kwa niaba ya Baba Mtakatifu na Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimisionari.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Giampietro Dal Toso, Katibu Mwambata, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa amegusia kuhusu Mfuko wa Dharura unaosimamiwa na kuratibiwa na Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa ulioanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya kuwasaidia watu wa Mungu, ambao wameathirika sana kutokana na maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Papa alichangia kiasi cha dola 750, 000 kama kianzio na anaendelea kuwaalika watu wa Mungu kuchangia katika Mfuko wa Dharura kupitia kwenye Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa katika nchi zao. Hiki ni kielelezo cha huruma na ukarimu unaojenga na kudumisha umoja na mshikamano na Makanisa mahalia katika kipindi hiki kigumu na chenye changamoto pevu katika maisha na utume wa Kanisa.

Msaada huu unatolewa kwa Makanisa mahalia kupitia miundo mbinu pamoja na taasisi mbali mbali za Kanisa. Hadi kufikia mwezi Oktoba 2020, jumla ya miradi 250 inayo gharimu kiasi cha dola za Kimarekani 473, 410 imepitishwa. Watu wa Mungu kutoka Hispania, Ufaransa, Korea ya Kusini wamechangia kwa kiasi kikubwa na hivyo kuwa ni mfano bora wa kuigwa. Nchi kama Rwanda na Bangaladesh nazo zimejitoa kadiri ya uwezo na nafasi zao. Fedha hii imetumika kwa namna ya pekee kwa ajili ya kuwasaidia watu walioathirika zaidi na Virusi vya Corona, COVID-19, elimu pamoja na kugharimia miradi mbali mbali ya shughuli za kichungaji kwenye Makanisa mahalia.

Wakati huo huo, Padre Tadeusz J. Nowak, OMI, Katiku mkuu wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za kimisionari “The Pontifical Mission Society” (Pontificium Opus a Propagatione Fidei) katika hotuba yake amegusia kuhusu mchango mkubwa unaotolewa na Mashirika haya kwa ajili ya kusaidia maisha na utume wa Makanisa mahalia katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili hususan katika huduma ya: elimu, afya, katekesi, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu. Mwaka 2020 una baraka na neema za pekee kwani Mtumishi wa Mungu Paulina Maria Jaricot (1799-1862), Muasisi wa Shirika la Kipapa la Kazi za kimisionari, tarehe 26 Mei 2020, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia uchapishwe waraka uliokubali muujiza uliopatikana kutokana na maombezi yake (Jaricot). Waraka huu ulifungua njia ya Paulina Maria Jaricot kutangazwa kuwa Mwenyeheri.

Propaganda Fide

 

 

17 October 2020, 15:49