Tafuta

Kardinali Pietro Parolin: Uhuru wa kidini ni kati ya vipaumbele vya diplomasia ya Vatican sehemu mbali mbali za dunia. Kardinali Pietro Parolin: Uhuru wa kidini ni kati ya vipaumbele vya diplomasia ya Vatican sehemu mbali mbali za dunia. 

Uhuru wa Kidini Ni Kipaumbele Cha Diplomasia ya Vatican! Utu!

Msimamo wa Vatican kuhusu: Uhuru wa kidini ni kati ya vipaumbele vinavyotolewa na Vatican katika sera na mikakati yake ya diplomasia kimataifa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, uhuru wa kidini unapata chimbuko lake katika utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Uhuru wa kidini unakwenda sanjari na uhuru wa dhamiri na haki ya maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kutambua na kuheshimu haki msingi za binadamu ni hatua muhimu sana ya maendeleo fungamani ya binadamu, kwani mizizi ya haki za binadamu inafumbatwa katika hadhi, heshima na utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hizi ni haki za wote zisizoweza kukiukwa wala kutenguliwa. Ni za binadamu wote bila kujali: wakati, mahali au mhusika. Haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Haki ya kwanza kabisa ni uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi pale anapofariki dunia kadiri ya mpango wa Mungu. Mkazo umewekwa katika haki ya uhuru wa kidini inayofafanuliwa katika uhuru wa kuabudu. Hiki ni kiini cha haki msingi kinachofumbata haki nyingine zote. Kuheshimu na kuthamini haki hii ni alama ya maendeleo halisi ya binadamu katika medani mbali mbali za maisha!

Haki inakwenda sanjari na wajibu! Mama Kanisa anakazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa kuheshimu haki msingi za binadamu, kichocheo muhimu sana cha amani na utulivu miongoni mwa binadamu. Kanisa linapenda kusimama kidete: kulinda na kudumisha haki na amani sehemu mbali mbali za dunia kwa njia ya mwanga na chachu ya tunu msingi za Kiinjili! Uhuru wa kidini ni sehemu muhimu sana ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu lililopitishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1948. Mwamini anapaswa kukiri na kushuhudia imani yake inayomwilishwa katika matendo. Uhuru wa kidini ni kati ya mambo ambayo hayapewi tena kipaumbele cha pekee katika vyombo vya utekelezaji wa sheria na hata wakati mwingine kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii. Kuna haja ya kuwajulisha walimwengu kwamba, kuna nyanyaso na dhuluma za kidini zinazoendelea kutendeka sehemu mbali mbali za dunia, kinyume kabisa cha haki msingi za binadamu.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitamka “declarat” kwamba, binadamu anayo haki ya uhuru wa dini. Uhuru huo ndio huu, kwamba, kila binadamu lazima akingiwe na shurutisho la mtu mmoja mmoja, la makundi ya kijamii, au la mamlaka yoyote ya kibinadamu. Hivyo kwamba, katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubalika kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi au hadharani, peke yake au katika muungano na wengine. Haki ya uhuru wa dini msingi wake ni hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili. Haki hii ya binadamu ya uhuru wa dini yatakiwa kuzingatiwa katika sheria za jamii ili iwe haki ya raia. (Rej. DH, namba 2).  Uhuru wa kidini ni kati ya haki msingi za binadamu zinazopaswa kulindwa na kuendelezwa, kwa kuheshimu na kuthamini dhamiri ya mtu binafsi na Jamii katika ujumla wake. Hii ni haki inayojikita katika masuala ya kidini na uhuru wa kuabudu.

Uhuru wa kidini unafumbatwa katika mambo makuu matatu: Mosi, ni umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali; Pili, ni kulinda na kudumisha amani na utulivu kama chachu ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Tatu, ni kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi kama sehemu ya mbinu mkakati wa kuleta suluhu ya migogoro mingi duniani. Hivi karibuni, Callista Gingrich, Balozi wa Marekani mjini Vatican aliandaa kongamano la siku moja, lililowashirikisha Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano ya kimataifa mjini Vatican pamoja na Bwana Mike Pompeo, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani mintarafu uhuru wa kidini sehemu mbali mbali za dunia. Kongamano hili lilipambwa na kauli mbiu “Kuendeleza na kulinda uhuru wa kidini kimataifa kwa njia ya diplomasia:” Balozi Callista Gingrich katika hotuba yake elekezi amesema kwamba, uhuru wa kidini ni kati ya vipaumbele msingi vya Serikali ya Marekani kwa kushirikiana na Vatican.

Bwana Mike Pompeo, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani katika hotuba yake, amegusia kuhusu Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimisha kumbukumbu ya miaka 75 tangu kusitishwa kwa vita hii ambayo iliacha madonda makubwa katika historia ya maisha ya mwanadamu. Watu wengi wasiokuwa na hatia walikamatwa na kuuwawa kikatili chini ya utawala wa Kinazi. Mtakatifu Yohane Paulo II atambukwa sana kwa mchango wake wa kuamsha dhamiri nyofu na hivyo kupelekea kuanguka kwa “Pazia la Nyuma”, yaani utawala wa Kikomunisti. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani ameishutumu Serikali ya China kwa kuvunja uhuru wa kidini. Amesema ni dhamana ya kimaadili kwa viongozi wa Kikristo na ushuhuda wa kanuni maadili na utu wema unaopaswa kutolewa kama njia ya kupambana na madhulumu na nyanyaso za kidini sehemu mbali mbali za dunia.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican amekazia kuhusu umuhimu wa dini katika kulinda na kudumisha: haki msingi, amani; usalama na maridhiano kati ya watu wa Mungu. Ni katika muktadha huu, uhuru wa kidini ni kati ya vipaumbele vinavyotolewa na Vatican katika sera na mikakati yake ya diplomasia kimataifa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, uhuru wa kidini unapata chimbuko lake katika utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Uhuru wa kidini unakwenda sanjari na uhuru wa dhamiri na haki ya maisha. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican alihitimisha kongamano hili kwa kukazia uhuru binafsi unaozingatia mipaka na kumwajibisha mtu. Uhuru bila mipaka ni hatari sana kwa mahusiano na mafungamano ya kijamii.

Matokeo yake ni kuibuka kwa watu wanaodai uhuru, lakini wao wenyewe wanashindwa kuheshimu uhuru wa jirani zao na matokeo yake ustawi, maendeleo na mafao ya wengi vinakuwa hatarini. Uhuru binafsi usiokuwa na mipaka ni kielelezo cha ubinafsi wa hali ya juu kabisa, ni uhuru unaokwenda kinyume cha matakwa ya Mwenyezi Mungu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uhuru wa kidini ni mchakato unaomwezesha mwamini kutafuta na kuambata ukweli na imani kwa Mwenyezi Mungu, Muumba wa vyote vinavyoonekana na visivyoonekana.

Uhuru wa Kidini
10 October 2020, 14:35