Tafuta

Mapambano dhidi ya umaskini, uchafuzi na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote yanapania kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, utu na heshima yake! Mapambano dhidi ya umaskini, uchafuzi na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote yanapania kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, utu na heshima yake! 

Uharibifu Wa Mazingira Na Umaskini Ni Vikwazo Vya Maendeleo!

Ili kupata maendeleo fungamani ya binadamu, kuna umuhimu wa kujikita katika mapambano dhidi ya umaskini; kwa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Sanjari na juhudi zote hizi, kuna haja pia ya kupambana na ugaidi wa kimataifa ambao unakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu na uhuru wa kuabudu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ikiwa kweli Jumuiya ya Kimataifa inataka kufikia kiwango cha juu cha maendeleo fungamani ya binadamu, inapaswa kujikita zaidi katika mapambano dhidi ya umaskini duniani; kwa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Sanjari na juhudi zote hizi, kuna haja pia ya kupambana na ugaidi wa kimataifa ambao unakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu na uhuru wa kuabudu. Huu ni mchango uliotolewa na Askofu mkuu Gabriele Giordano Caccia, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, kwenye mkutano wa 75 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, uliofanyika tarehe 13 Oktoba 2020 huko New York, Marekani. Ameikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kwamba, watu wanategemeana na kukamilishana kama familia kubwa ya binadamu. Kumbe, kuna haja ya kufikiri na kutenda kama dunia moja yenye mradi mkubwa unaopaswa kutekelezwa kwa kuzingatia: Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030; Mkakati wa Sendai wa Kupunguza Madhara ya Maafa kuanzia mwaka 2015 – 2030 (Sendai Framework for Disaster Risk Reduction, 2015-2030) pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Paris wa Mabadiliko ya Tabianchi, Cop21 uliofanyika mjini Paris, nchini Ufaransa, kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2015.

Hii ni mikataba ambayo Jumuiya ya Kimataifa imeipitisha ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na majanga asilia. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuunganisha nguvu ili kupunguza kiwango cha uzalishaji wa hewa ya ukaa, inayosababisha ongezeko kubwa la joto duniani kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira. Juhudi zote hizi hazina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: utu, heshima na uhai wa binadamu; sera na mikakati bora ya uchumi fungamani pamoja na kudhibiti madhara yanayotokana na majanga asilia. Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa ni chanzo kikuu cha majanga ya mafuriko, maporomoko ya udongo, ongezeko la kina cha bahari pamoja na ukame wa kutisha. Kumbe, utekelezaji makini wa mikataba ya kimataifa utasaidia Jumuiya ya Kimataifa kuweza kupambana na majanga asilia ambayo yanaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika umaskini, njaa na magonjwa! Askofu mkuu Gabriele Giordano Caccia anaendelea kufafanua kwamba, majanga yameendelea kumwandama mwanadamu, kiasi hata cha kuharibu makazi, maendeleo ya kiuchumi na hasa katika sekta ya kilimo, kiasi cha kuvuruga mfumo mzima wa uhakika wa usalama wa chakula duniani.

Majanga yanaendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la maskini duniani na hasa kutoka katika Nchi zinazoendelea. Mchakato wa udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi ni dhamana ya haki, maadili na utu wema. Mchakato wa ulinzi wa mazingira hauna budi kusaidia kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu; kwa kupambana na umaskini wa hali na kipato, ili kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na mfumo bora zaidi wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa sasa na kwa kizazi kijacho! Vijana wa kizazi kipya hawana budi kujengewa uwezo wa kupambana na hali pamoja na mazingira yao kwa kuwapatia uwezo wa elimu bora zaidi. Wafundwe umuhimu wa kujikita katika ulinzi na utunzaji bora wa mazingira; kwa kuwathamini na kuwahudumia jirani zao ili mwisho wa siku waweze kuondokana na utamaduni wa kutojali mazingira wala kuwathamini watu wengine. Vatican hivi karibuni ilitia saini Itifaki ya Montreal ya Mwaka 1987.

Itifaki ya Montreal ya Mwaka 1987 “Montreal Protocol of 1987” ni Mkataba wa Kimataifa ulioridhiwa na Jumuiya ya Kimataifa ili kudhibiti uzalishaji na usambazaji wa bidhaa zenye kemikali zinazomong’onyoa tabaka la hewa ya ozoni angani,  ambayo ni muhimu sana katika kudhibiti kiwango cha mionzi ya jua inayotua ardhini. Ozoni ni hewa iliyoko kwenye angahewa ya juu, takribani kilometa 10 hadi 50 juu ya ardhi. Kazi yake kubwa ni kuchuja sehemu kubwa ya mnururisho wa mionzi kama “Ultraviolet B” isifike kwenye uso wa dunia. Itifaki hii pamoja na mambo mengine inapania kuhamasisha ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kuratibu shughuli mbali mbali za binadamu zinazotishia kuharibu tabaka la hewa ya ozoni angani na hivyo kuchochea kuongezeka kwa joto duniani. Itifaki imepata mafanikio makubwa katika Jumuiya ya Kimataifa kama sehemu ya mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kudhibiti uzalishaji wa hewa ya ukaa ambayo ina madhara makubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Itifaki imekuwa ikiboreshwa mara kwa mara kuendana na tafiti mbali mbali za sayansi na maendeleo ya teknolojia na kwa mara ya mwisho maboresho hayo yalifanyika mjini Kigali, Rwanda, kunako mwaka 2016. Takwimu zinaonesha kwamba,  kuna nchi 197 ambazo zimeridhia Itifaki ya Montreal ya Mwaka 1987 na Sudan ya Kusini ni nchi ya mwisho kuridhia Itifaki hii kunako mwaka 2012.

maendeleo

 

 

19 October 2020, 13:58