Tafuta

Kardinali Pietro Parolin: Mkataba wa Muda Kati ya Vatican na Serikali ya China wa Tarehe 22 Septemba 2018 ni kwa ajili ya uteuzi wa Maaskofu mahalia peke yao! Kardinali Pietro Parolin: Mkataba wa Muda Kati ya Vatican na Serikali ya China wa Tarehe 22 Septemba 2018 ni kwa ajili ya uteuzi wa Maaskofu mahalia peke yao! 

Kardinali Pietro Parolin: Uteuzi Wa Maaskofu Katoliki Nchini China!

Kardinali Pietro Parolin katika hotuba yake elekezi katika Jubilei ya Miaka 150 ya P.I.M.E amegusia kuhusu: Mchakato wa majadiliano kati ya Vatican na China kama ulivyoasisiwa na Papa Pio XII; Upyaisho wa majadiliano pamoja na Uelewa potofu wa Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China wa tarehe 22 Septemba 2018 kuhusu uteuzi wa Maaskofu mahalia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Taasisi ya Kipapa Kwa Ajili ya Utume wa Kimisionari “Il Pontificio Istituto Missioni Estere (Kwa lugha ya Kilatin: Pontificium Institutum Pro Missionibus Exteris), P.I.M.E. inaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya maisha na utume wake nchini China. Kama kilele cha maadhimisho haya tarehe 3 Oktoba 2020 kumefanyika kongamano ambalo limepembua fursa, changamoto, matatizo yaliyopo nchini China hata katika mwanga wa janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID- 19. Imekuwa pia ni nafasi ya kutathmini maisha na utume wa Kanisa nchini China bila kusahahu uhusiano kati ya Vatican na Serikali ya China. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika hotuba yake elekezi amegusia kuhusu mchakato wa majadiliano kati ya Vatican na China kama ulivyoasisiwa na Papa Pio XII; Upyaisho wa majadiliano kati ya Vatican na China; Uelewa potofu wa Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China, uliotiwa saini tarehe 22 Septemba 2018 kuhusu uteuzi wa Maaskofu mahalia. Lengo mojawapo limefikiwa na kwamba, kuna alama ya matumaini kwa Wakristo nchini China. Kardinali Parolin anasema, historia ya Kanisa Katoliki nchini China inabebwa na Myesuit Matteo Ricci (Mattheus Riccius Maceratensis; 6 Oktoba 1552 – 11 Mei 1610), aliyejitahidi kuinjilisha China kunako karne ya 16 na baadaye Taasisi ya Kipapa Kwa Ajili ya Utume wa Kimisionari ikafuatia.

Tangu tarehe 17 Januari 1951, jitihada za majadiliano kati ya Vatican na Serikali ya China zilianza kuonekana kwa Serikali ya China kuamua kwamba, Mapadre na watawa wataendelea kuwa chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, lakini Kanisa lilitakiwa kuhakikisha kwamba, viongozi wa Kanisa kutoka nchini China wanaonesha uzalendo kwa nchi yao. Papa Pio XII akapitia Mkataba wa kwanza na kuufanyia marekebisho, lakini haukuweza kutekelezwa kutokana na hali tete iliyokuwepo wakati ule. Kulikuwa kuna vita nchini Korea na Vatican pamoja na China, hawakuelewana wala kuaminiana na matokeo yake ni mkataba huu haukuweza kutekelezwa hata kidogo na huo ukawa ni mwanzo wa kudhaniana vibaya kati ya Kanisa na Serikali ya China. Kardinali Parolin anakaza kusema, majadiliano mapya yalianza tena kujitokeza baada ya kutimia zaidi ya miaka 30 na hii ni dhamana na utume uliotekelezwa kunako mwaka 1980 na Kardinali Roger Etchegaray, aliyekuwa ni Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani. Hali ya kisiasa nchini China ilikuwa bado ni tete sana, kumbe, Vatican haikuweza kupata mafanikio yaliyokuwa yanatarajiwa.

Huu ni mchakato wa majadiliano ya kina ulioanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, ukaendelezwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na hatimaye, Papa Francisko akashuhudia matunda ya juhudi hizi katika ukweli na uwazi kwa kuwekwa saini Mkataba wa muda kunako mwaka 2018. Mkazo ni kuhusu shughuli za kichungaji na kitume, ili kuwawezesha waamini wa Kanisa Katoliki nchini China kuchangia kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mchakato huu pamoja na mambo mengine unapania kukoleza: imani na matumaini; umoja na mshikamano wa kidugu. Uteuzi wa Maaskofu kwa ushirikiano kati ya Vatican na Serikali ya China ni jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa nchini China na kwamba, huo ni mwanzo wa ushirikiano mpana zaidi kwa sasa na kwa siku za usoni. Kardinali Parolin anasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya waamini wametoa tafsiri potofu kuhusu mkataba huu, kwa kuuhusianisha na masuala ya kisiasa. Mkataba wa tarehe 22 Septemba 2018 ni kwa ajili ya uteuzi wa Maaskofu peke yake.

Vatican inatambua sana matatizo na changamoto katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini China na kwamba, si rahisi kuweza kuyatatua kwa mkupuo, kunahitajika uvumilivu. Ikumbukwe kwamba, uteuzi wa Maaskofu Jimbo ni kati ya matatizo ambayo Kanisa Katoliki nchini China limekua nayo kwa muda mrefu kama hata ambavyo Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alivyobainisha kunako mwaka 2007. Ni kutokana na Mkataba wa muda kati ya Vatican na China, leo hii, Maaskofu wote wa China wanaunda umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni katika mwono wa historia ya Kanisa Katoliki nchini China inayotaka umoja wa Maaskofu upewe kipaumbele cha pekee. Hata wale Maaskofu ambao hawakuwa na umoja kamili na Khalifa wa Mtakatifu Petro ni viongozi waliofundwa na kuundwa na wamisionari, waliowafahamu fika na utume wao kwa ajili ya watu wa Mungu. Maaskofu hawa wote waliokuwa wamewekwa wakfu bila idhini ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, wamekiri na kuomba msamaha na hatimaye, kujipatanisha na Baba Mtakatifu Francisko. Hiki ni kielelezo cha imani hai.

Ndiyo maana Vatican inaendelea kujibidiisha ili changamoto hii iweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa njia ya Mkataba kati ya Vatican na Serikali ya China. Lengo la Mkataba huu ni kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa, utakaowawezesha Wakristo kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, sanjari na kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni matumaini ya Kardinali Parolin kwamba, Mkataba huu utaendelea kufanya kazi bora zaidi, kuliko ulivyowekwa saini,  ili hatimaye, Kanisa liweze kuteuwa Maaskofu mahalia kwa ajili ya majimbo ambayo hadi sasa bado yako wazi! Lengo kuu ni utume na maisha ya Kanisa nchini China. Pole pole, waamini wa Kanisa Katoliki nchini China wanaanza kuelewa na mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho unaanza kushika kasi, ili kila mmoja aweze kutangaza na kushuhudia imani yake kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Majadiliano katika ukweli na uwazi, yawasaidie kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Mkataba huu unalenga pia kudumisha mchakato wa amani Kimataifa.

Maaskofu China: Uteuzi

 

 

13 October 2020, 14:40