Tafuta

Kamati ya Wataalam wanaotathmini mikakati ya udhibiti wa fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya kigaidi MONEYVAL, imehitimisha ukaguzi wa mfumo wa fedha mjini Vatican. Kamati ya Wataalam wanaotathmini mikakati ya udhibiti wa fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya kigaidi MONEYVAL, imehitimisha ukaguzi wa mfumo wa fedha mjini Vatican. 

Kamati ya Moneyval Yahitimisha Ukaguzi wa Mfumo Wa Fedha Vatican

Moneyval ambayo ni Kamati ya wataalam wa udhibiti wa fedha haramu, tarehe 13 Oktoba 2020 imehitimisha ziara ya ukaguzi kuhusiana na vitendo vya utakatishaji wa fedha haramu pamoja na ufadhili wa vitendo vya kigaidi kwenye vyombo vya fedha mjini Vatican. Ziara hii ya kikazi imefanyika katika hali ya maelewano na ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wakuu wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kamati ya Wataalam wanaotathmini mikakati ya udhibiti wa fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya kigaidi kutoka Umoja wa Ulaya, EU., Moneyval, tarehe 13 Oktoba 2020 imehitimisha ziara ya ukaguzi kuhusiana na vitendo vya utakatishaji wa fedha haramu pamoja na ufadhili wa vitendo vya kigaidi  kwenye vyombo vya fedha mjini Vatican. Ziara hii ya kikazi imefanyika katika hali ya maelewano na ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wakuu wa Vatican. Taarifa kwa vyombo vya habari kutoka kwa Kamati ya Moneyval inaonesha kwamba, Vatican imepiga hatua kubwa katika mchakato wa kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya kigaidi. Taarifa rasmi itatolewa kwenye mkutano mkuu wa Kamati ya Moneyval unaotarajiwa kufanyika mapema mwaka 2021 kwa kufuata taratibu za ndani za Kamati hii. Viongozi wakuu wa Vatican wamefurahishwa na kutoa shukrani zao za dhati kwa wakaguzi na wajumbe wa Kamati ya Moneyval.

Itakumbukwa kwamba, katika ulimwengu halisi utakatishaji fedha “Money Laundering” ni kitendo cha ‘kusafisha’ kiwango kikubwa cha fedha haramu iliyopatikana kwa kuuza dawa za kulevya, mihadarati au fedha zinazotokana na vitendo vya uharamia. Fedha hii iliyopatikana kwa njia haramu ikiingizwa kwenye mzunguko wa fedha, mtuhumiwa anaweza kuhusishwa na kosa la kutakatisha fedha. Utakatishaji fedha ni tendo la kihalifu linaloathiri mzunguko wa fedha na uchumi wa nchi husika. Fedha zinazopatikana kwenye matukio ya kihalifu hujulikana kama ‘pesa chafu’ hivyo utakatishaji huzisafisha fedha hizo ili zionekane ni za halali. Moneyval ni Kamati ya Wataalam wanaotathmini mikakati ya udhibiti wa fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya kigaidi kutoka Umoja wa Ulaya, EU.

Kamati ya Monevyval hivi karibuni imetembelea mjini Vatican na kukutana na Baba Mtakatifu Francisko, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican pamoja na waandamizi wao, kama sehemu ya utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa kunako mwaka 2019. Kwa mara ya kwanza Moneyval ilitembelea na kufanya ukaguzi wa mfumo wa fedha mjini Vatican kunako mwaka 2012. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwenye Kamati ya Moneyval, ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kuondokana na tabia ya watu kupenda kuabudu sana fedha na hivyo kuigeuza kuwa kama miungu wadogo na matokeo yake ni kuangamia kwa uchumi, hali inayoathiri pia utu na heshima ya binadamu, unyonyaji, ukosefu wa usawa katika mfumo huu pamoja na tabia ya kutowajali binadamu wengine. Fedha inayopatikana katika mazingira kama haya ni chafu na ina matone ya damu. Fedha hii haramu imekuwa ikitumika pia kwa ajili ya kugharimia vitendo vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia kutokana na uchu wa madaraka, mali na utajiri wa haraka haraka.

Baba Mtakatifu katika Waraka wake wa Kitume: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”,  anasema kwamba, huu ni wakati wa kuwekeza katika mchakato wa sera na mikakati ya maendeleo fungamani kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi, kwa kuhakikisha kwamba, biashara haramu ya silaha duniani pamoja na vita vinakoma, kwani vita ni mama wa majanga makubwa ya binadamu! Upigaji rufuku wa silaha za kinyuklia ni changamoto ya kimaadili na dhamana ya kiutu kwa kukazia kanuni maadili zinazoendeleza amani duniani; ushirikiano katika ulinzi na usalama. Rasilimali fedha inayowekezwa kwenye utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za maangamizi ielewekezwe katika Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na baa la njaa duniani, ili kuwawezesha watu kupata maisha bora zaidi. Kumbe, sera na mikakati inayopania kudhibiti utakatishaji wa fedha na ufadhili wa vitendo vya kigaidi inalenga kuangalia kwa umakini mkubwa mzunguko wa fedha duniani na pale inapowezekana kuingilia kati kama sehemu ya mchakato wa kupambana na vitendo vya kigaidi. Uchumi wa dunia hauna budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu! Fedha inapaswa kumhudumia mwanadamu na wala si kinyume chake. Vatican katika masuala ya fedha na uchumi, itaendelea kujielekeza zaidi katika sera za ukweli na uwazi zinazosimamiwa na Mamlaka ya Habari za Kifedha mjini Vatican, AIF, “Financial Information Authority”.

Kwa upande wake, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican alipokutana na kuzungumza Kamati ya Wataalam wanaotathmini mikakati ya udhibiti wa fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya kigaidi kutoka Umoja wa Ulaya, Moneyval, EU., amedadavua kuhusu sera, mikakati na sheria zinazotumika mjini Vatican kama sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha ukweli, uwazi na uaminifu wa matumizi ya fedha ya Kanisa sanjari na ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya uchumi na fedha. Ni katika muktadha huu, Vatican imeamua kujiunga na Kamati ya Wataalam wanaotathmini mikakati ya udhibiti wa fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya kigaidi kutoka Umoja wa Ulaya, Moneyval. Vatican inaendelea kuimarisha miundombinu ya fedha, ili kupambana na uwezekano wa kutakatisha fedha pamoja na kugharimia vitendo vya kigaidi. Kumbe, Vatican inaupatia uzito wa juu wa mapendekezo yatakayotolewa na Kamati ya Moneyval kama amana na utajiri ili kuendelea kuimarika katika masuala ya fedha na uchumi kwa kuzingatia, sheria, taratibu, kanuni, lakini zaidi maadili na utu wema.

Wanachama wa Kamati hii wanapenda kuona kwamba, rasilimali fedha waliyo nayo inatumika kuleta ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa upande wa Vatican ni kutaka kuhakikisha kwamba, rasilimali fedha ya Kanisa inatumika hasa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo; na kwamba, fedha ya Kanisa inatumika katika mchakato wa uinjilishaji na ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Ni katika muktadha huu, Vatican inapenda kukazia zaidi dhamana na wajibu wa kimaadili katika shughuli za uwekezaji, fedha na uchumi. Fedha inapaswa kutumika kwa ajili ya huduma kwa mahitaji msingi ya binadamu na wale si kinyume chake!

Moneyval
15 October 2020, 14:48