Tafuta

Vatican News
Baraza la Makanisa Ulimwenguni Kwa Kushirikiana na  Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini wameandaa Waraka wa pamoja: Huduma kwa ulimwengu uliojeruhiwa katika mshikamano wa kidini. Baraza la Makanisa Ulimwenguni Kwa Kushirikiana na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini wameandaa Waraka wa pamoja: Huduma kwa ulimwengu uliojeruhiwa katika mshikamano wa kidini.  (AFP or licensors)

Mshikamano wa Makanisa Katika Huduma Dhidi ya Virusi COVID-19

WCC kwa kushirikiana na PCID wameandika hati kuhusu: “Huduma kwa Ulimwengu Uliojeruhiwa katika Mshikamano wa Kidini: Mwaliko wa Kikristo Kutafakari na Kutenda Wakati wa COVID-19”. Huu ni msingi wa Kikristo mintarafu mshikamano katika mchakato wa kuganga na kuponya madonda ambayo yameujeruhi ulimwengu. Tafakari hii ni msaada wa kupambana na Virusi vya COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, PCID, yameandika hati ya pamoja inayoongozwa na kauli mbiu “Serving a Wounded World” yaani: “Huduma kwa Ulimwengu Uliojeruhiwa katika Mshikamano wa Kidini: Mwaliko wa Kikristo Kutafakari na Kutenda Wakati wa COVID-19”. Huu ni msingi wa Kikristo mintarafu mshikamano katika mchakato wa kuganga na kuponya madonda ambayo yameujeruhi ulimwengu. Tafakari hii ni msaada mkubwa unaopania kuunganisha nguvu za waamini kutoka katika dini mbali mbali, ili kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Huu ni wakati muafaka wa kutafakari madhara makubwa yaliyosababishwa na COVID-19 na kuanza kujipanga vizuri ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza baada ya janga hili. Hati hii imegawanyika katika sehemu kuu saba: Utangulizi, Kipeo cha wakati huu, Mshikamano unaosimikwa katika matumaini; Msingi wa mshikamano wa kidini, Kanuni, Mapendekezo na hatimaye ni hitimisho la hati hii.

Utangulizi: Kimsingi, hati hii inawahamasisha Wakristo kutambua maana ya kupenda na kuwahudumia jirani zao ambao wameathirika kutokana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona. Huduma hii inapaswa kusimikwa katika mshikamano kwa kushirikiana na waamini wa dini mbali mbali duniani kadiri ya imani na mapokeo yao. Changamoto mamboleo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 ni mwaliko wa kutambua umuhimu wa kushirikiana na kushikamana kiekumene na kidini, kama ilivyokuwa kwa yule Msamaria mwema. Mambo makuu mawili yanapewa kipaumbele cha kwanza yaani “Huduma na Mshikamano” ili kuwapenda na kuwahudumia jirani. Hii ni changamoto ya kuvuka kikwazo cha maamuzi mbele na hivyo kutambua kwamba, hata waamini wa dini nyingine wanaweza kuwasaidia Wakristo kutambua maana ya kweli ya huduma na mshikamano wa dhati.

Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 ni changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali kuvunjilia mbali tabia ya waamini kutovumiliana, ili kujenga jamii inayosimikwa katika maridhiano. Ni mwaliko wa kuondokana na mifumo yote ya ubaguzi, kwa kutambua na kuheshimu: utu na haki msingi za binadamu. Ni muda wa kujenga na kudumisha mahusiano ya dhati kwa kuunga mkono sera na mikakati ya uchumi shirikishi, ili kuondokana pia na mifumo mbali mbali inayosababisha ukosefu wa haki jamii, ili hatimaye, kujenga na kuimarisha ekolojia fungamani. Mchakato wa kuganga na kuponya madonda ambayo yamesababishwa na Virusi vya Corona, COVID, usaidie kuimarisha imani, upendo na mshikamano kwa waathirika wa gonjwa hili hatari.

Kipeo cha wakati huu: Janga la COVID-19 limeushtukiza ulimwengu ambao bado ulikuwa haujajiandaa kikamilifu na matokeo yake, kumekuwepo na madhara makubwa kwa watu kupoteza maisha yao. Lakini wengi wameathirika kisaikolojia, kiuchumi, kisiasa, kidini na kwamba, waamini wengi walipokonywa muda wa ibada za hadhara. Watu wengi wameandamwa na kifo pamoja na machungu yake, zaidi sana kwa kushindwa kuwapatia wapendwa wao buriani kama ilivyokuwa kawaida. Balaa la njaa ulimwenguni linaendelea kuongezeka maradufu. Kumekuwepo na ongezeko la vitendo vya ukatili majumbani na ongezeko la mimba za utotoni. Watu wengi wamekumbwa na upweke hasi, hali ya kukata tamaa sanjari na ukosefu wa usalama kutokana na kulazimika kukaa kwenye karantini kwa muda mrefu.

Gonjwa hili hatari halibagui wala kuchagua hali na matabaka ya watu. Limeonesha pengo kubwa kati ya matajiri na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Wazee, wagonjwa na maskini ni watu waliopapaswa na kuguswa sana na Corona, COVID-19. Wakimbizi, wahamiaji na wafungwa wameathirika vibaya sana. Huu ni muda muafaka wa kusikiliza na kujibu kilio cha Mama Dunia na kilio cha maskini duniani, kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Hapa kuna haja ya kufanya wongofu wa kiekolojia, ili kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Kutokana na udhaifu uliooneshwa na binadamu wakati aliposhambuliwa na gonjwa hatari la Virusi vya Corona, COVID-19, watu wengi wameguswa sana na huduma za kishujaa zilizotolewa na wadau mbali mbali katika huduma ya afya. Injili ya upendo na mshikamano imeshamiri sana kwa ajili ya kuwahudumia wazee, wagonjwa na maskini: kiroho na kimwili, kwa kutambua kwamba, watu wote wanaunda familia kubwa ya binadamu na wote wanaishi na kupata hifadhi katika dunia mama, nyumba ya wote.

Binadamu wote wanategemeana na kukamilishana, ndiyo maana hakuna mtu atakayejiokoa mwenyewe. Huu ni wakati muafaka wa kugundua tena umuhimu wa upendo na mshikamano, ili kujipanga vyema zaidi baada ya janga la homa kali ya mapafu inayosabishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Majadiliano ya kidini yanaweza kusaidia sana katika mchakato wa ujenzi wa mshikamano wa kidini, kwa kuheshimiana na kuwa wazi kwa wengine, ili kukuza mshikamano miongoni mwa watu wa imani pamoja na wenye mapenzi mema. Njia hii yamshikamano inaongozwa na matumaini yanayobubujika kutoka katika dini zao mbali mbali. Mshikamano unaosimikwa katika matumaini. Watu wote wana matumaini na ndoto zao na kwamba, matumaini yanausaidia utashi wa mwanadamu kuendelea kuishi hata nyakati za shida na majaribu makubwa. Wakristo wanahamasishwa kushirikiana na kushikamana na waamini wa dini mbali mbali duniani ili kuweza kunafsisha matumaini kwa ajili ya umoja wa ulimwengu ambao unasimikwa katika haki na amani.

Waaamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa kufanya kazi na watu wote wenye mapenzi mema, ili kujenga ulimwengu ulio bora zaidi. Matumaini ni fadhila muhimu sana ya Kimungu. Leo hii, kuna haja ya kushirikishana kanuni maadili, utu wema na tunu msingi za maisha ya kiroho, ili kuwapatia watu matumaini baada ya kukabiliana na madhara makubwa ambayo yamesababishwa na janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Waamini wa dini mbali mbali wanaweza kuchangia ujenzi wa jamii mpya yenye mwono wa umoja wa familia ya binadamu pamoja na urithi wa kanuni maadili ambazo zinapatikana miongoni mwa binadamu wote. Waamini wote wanapaswa kuwajibika mintarafu kanuni maadili na huduma ili kuganga na kuponya ulimwengu ambao umejeruhiwa kwa Virusi vya Corona, COVID-19. Huduma hii inapaswa kuanza kunafasishwa katika familia, miji, mataifa na hadi kufikia ulimwengu mzima.

Msingi wa mshikamano wa kidini kadiri ya Wakristo unabubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hii inatokana na utambuzi kwamba, binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, Mwenyezi Mungu anao mpango wake juu yao. Wote wanaunganishwa na upendo na utu wao kama binadamu, hivyo wanapaswa kupendana na kuhudumiana kama watoto wa familia kubwa ya binadamu. Kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema, upendo na huduma yao, vinapaswa kuvuka mipaka yote, ili kuwagusa na kuwaambata, watu wote walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano. Imani na matumaini ya Wakristo yanabubujika kutoka kwa Kristo Yesu aliyeganga na kuponya madonda ya dhambi kwa njia ya Fumbo la Msalaba, kielelezo cha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa na huruma, upendo na ukarimu kwa jirani zao.

Kwa njia ya watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali, waamini wanamwona Kristo Yesu anayeteseka kati yao; Kristo anayependa kuhudumiwa. Mshikamano wa dhati ni chachu muhimu sana inayoweza kuleta mabadiliko katika maisha ya mwanadamu. Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kielelezo makini kwamba, upendo una nguvu zaidi kuliko madonda na kifo kinachomwandama mwanadamu. Mshikamano unawawezesha waamini kujenga na kudumisha umoja unaobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu anayewaunganisha na waamini wengine. Karama na mapaji ya Roho Mtakatifu yawawezeshe kuwanyanyua watu. Waamini watakirimiwa matunda ya Roho Mtakatifu ambayo ni: upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Kwa njia ya Roho Mtakatifu wanaweza kusulubisha mawazo mabaya na tamaa zake. Wala hakuna mashiko kwa kujisifu bure, kwa kuchokozana na kuhusudiana. Roho Mtakatifu anawatuma kwenda kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Habari Njema ya Wokovu na mikono ya Kristo Yesu, anayewahudumia wale wote wanaoteseka!

Kanuni: Ili Wakristo waweze kushirikiana na kushikamana na waamini wa dini mbali mbali duniani, wanapaswa kuzingatia kanuni zifuatazo: Unyenyekevu na unyofu wa moyo katika kuhudumia. Heshima, nidhamu na usawa kwa wote. Kama Jumuiya ya waamini wanahimizwa kuwa na huruma na mapendo, daima wakitafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini wajenge na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi, tayari kujifunza pia kutoka kwa wengine. Wajenge moyo wa toba, wongofu wa ndani na upyaisho wa maisha. Waamini waoneshe daima moyo wa shukrani na ukarimu kwa Mwenyezi Mungu na jirani zao. Mwishoni, wajitahidi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo, ili kuweza kunafsisha upendo wa Kristo katika huduma.

Mapendekezo na hatimaye ni hitimisho la hati hii. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, PCID, katika hati ya pamoja inayoongozwa na kauli mbiu “Huduma kwa Ulimwengu Uliojeruhiwa katika Mshikamano wa Kidini: Mwaliko wa Kikristo Kutafakari na Kutenda Wakati wa COVID-19” wanawahimiza Wakristo kutafuta njia ya kuweza kushuhudia Ukristo wao kwa kuwa ni vyombo na sauti ya wanyonge. Wajitahidi kujenga na kudumisha utamaduni unaowashirikisha na kuwapatia watu fursa ya kusherehekea karama mbali mbali walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Huu ni wakati wa kuboresha mshikamano wa upendo kwa njia ya tasaufi makini. Wakristo waendelee kujikita katika majiundo yao: kiroho na kimwili; kwa kuwa na ufahamu mpana zaidi, ili kumhudumia mwanadamu kwa kushirikiana na wengine.

Wakristo wajenge ari na moyo wa kushirikiana na vijana wa kizazi kipya; kwa kuendelea kupanua wigo wa majadiliano yanayowalenga watu wote bila ubaguzi. Waamini wathubutu kuanzisha miradi yenye kukoleza mshikamano wa kidini na kiekumene, jambo linalowaunganisha wote. Kwa njia hii, wataweza kuwa kweli ni mashuhuda wa haki, amani, mshikamano na mafungamano ya watu. Watu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kristo Yesu, awe ni nguvu inayowawezesha waamini kuwapenda na kuwahudumia watu walioathirika kwa Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa waamini kufungua nyoyo zao kwa ajili ya majadiliano; na mikono yao kwa ajili ya upendo na mshikamano, kwa pamoja wataweza kujenga ulimwengu unaoganga, unaoponya na kusimikwa kwenye matumaini.

Hati ya Pamoja WCC

 

23 September 2020, 15:22