Tafuta

Waraka wa Samaritanus Bonus: Yaani "Msamaria Mwema" Waraka Kuhusu Huduma Kwa Wagonjwa Mahututi na Walioko Kufani. Waraka wa Samaritanus Bonus: Yaani "Msamaria Mwema" Waraka Kuhusu Huduma Kwa Wagonjwa Mahututi na Walioko Kufani. 

Waraka wa Msamaria Mwema: Huduma Kwa Wagonjwa Mahututi

“Samaritanus Bonus” Yaani: “Msamaria Mwema”: Waraka Kuhusu Huduma Kwa Wagonjwa Mahututi na Walioko Kufani. Waraka huu umegawanyika katika sehemu kuu tano: Sehemu ya kwanza ni huduma ya upendo kwa jirani. Pili ni kuhusu mang’amuzi ya maisha mintarafu mateso sanjari na kutangaza Injili ya matumaini kwa watu wanaoteseka kimwili, kisaikolojia, kimaadili na kiroho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa tarehe 22 Septemba 2020 limechapishwa Waraka wa “Samaritanus Bonus” Yaani: “Msamaria Mwema”: Waraka Kuhusu Huduma Kwa Wagonjwa Mahututi na Walioko Kufani. Waraka huu umegawanyika katika sehemu kuu tano: Sehemu ya kwanza ni huduma ya upendo kwa jirani kwa kuzingatia kanuni maadili, ili kulinda maisha na kutomdhulu mtu. Sehemu ya pili ni kuhusu mang’amuzi ya maisha mintarafu mateso ya Kristo sanjari na kutangaza Injili ya matumaini kwa watu wanaoteseka kimwili, kisaikolojia, kimaadili na kiroho. Sehemu ya tatu ni kuhusu Moyo wa Msamaria Mwema Unaoona: Maisha ya binadamu ni matakatifu na zawadi yenye thamani kubwa, changamoto ni kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu. Sehemu ya nne ya Waraka huu inajihusisha zaidi na tamaduni ambazo ni kikwazo cha utakatifu wa maisha ya binadamu kwa kukumbatia utamaduni wa kifo unaojikita katika sera za utoaji mimba, kifolaini na msaada kwa watu wanaotaka kujinyonga. Sehemu ya tano inafafanua “Magisterium ya Kanisa” yaani “Mamlaka fundishi ya Kanisa kuhusu rufuku ya kifolaini na msaada kwa watu wanaotaka kujinyonga; kanuni maadili zinazoongoza huduma tete za kitabibu; huduma msingi za lishe na maji; huduma shufaa: (palliative care), wajibu wa familia na vituo vya kutunza wagonjwa.

Huduma ya utunzaji mimba na tiba kwa watoto wachanga; tiba ya kupunguza maumivu na hali ya kupoteza fahamu; hali ya mtu kutojitambua pamoja na utambuzi hafifu; dhamiri nyofu kwa wafanyakazi katika sekta ya afya na taasisi za afya zinazomililikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki. Sehemu hii inaendelea kufafanua kuhusu: Huduma za kichungaji na msaada wa Sakramenti za Kanisa. Mang’amuzi ya kichungaji kwa wagonjwa wanaoomba kifolaini au msaada wa kujinyonga. Mabadiliko katika mfumo wa elimu na majiundo makini kwa wafanyakazi katika sekta ya afya. Waraka wa “Samaritanus Bonus” Yaani: “Msamaria Mwema”: Waraka Kuhusu Huduma Kwa Wagonjwa Mahututi na Walioko Kufani unahitimishwa kwakuwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashuhuda wa upendo katika mateso. Kuna umuhimu wa kuheshimu, kulinda, kupenda na kuhudumia uhai, maisha ya kila mwanadamu sanjari na kuhakikisha kwamba, wagonjwa wanasindikizwa katika hatua mbalimbali za ugonjwa wao. Waraka huu, umeidhinishwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Juni 2020.

Sehemu ya kwanza ni huduma ya upendo kwa jirani kwa kuzingatia kanuni maadili, ili kulinda maisha na kutomdhulu mtu. Utakatifu na mateso ya mwanadamu ni sehemu ya fumbo la maisha ya mwanadamu linaloweza kueleweka tu kwa njia ya Ufunuo. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanahudumia Injili ya uhai katika hatua zake zote hadi pale mauti ya kawaida inapomfika mtu kadiri ya mapenzi ya Mungu. Kanuni maadili na utu wema ni mwongozo makini kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, ili kulinda maisha ya binadamu na kutomdhulu mtu. Hapa watu wanapaswa kuongozwa na kanuni ya dhahabu inayoratibu uhusiano na watu wengine kwamba, “Basi yoyote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo: maana hiyo ndiyo torati na manabii”. Mt. 7:12. Hii ni kanuni muhimu sana katika huduma ya afya inayopaswa kuboreshwa kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano kati ya: mgonjwa, wafanyakazi katika sekta ya afya, ndugu na jamaa ya mgonjwa, wanajumuiya ambao wanauhusiano wa karibu na mgonjwa. Sanaa ya matibabu, mchakato wa huduma pamoja na matibabu endelevu ni mambo msingi katika huduma ya afya na hasa zaidi kwa wagonjwa mahututi na wale ambao wako kufani.

Kristo Yesu anawaalika wafuasi wake kuwa ni Wasamaria wema kwa kuwekeza katika huduma ya tiba, ili kuokoa maisha ya watu, kielelezo cha upendo wa Mungu, ambaye kimsingi ni chanzo, maana na hatima ya maisha ya binadamu. Wajibu wa kimaadili, ukiongozwa na imani, uwasaidie watu kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, chanzo cha uhai. Kifo ni sehemu ya maisha ya mwanadamu na wanasayansi wanapaswa kutambua ukweli huu. Daima mgonjwa apewe tiba hata wale wenye magonjwa sugu na ya muda mrefu. Hii ni huduma ya tiba: kimwili, kisaikoljia, kijamii, kifamilia na katika maisha ya kiroho, kwa kuzingatia taalimungu ya maisha ya mwanadamu. Wadau mbalimbali wamsaidie mgonjwa kujiandaa kufa kifo chema, akiwa anasindikizwa na neema ya utakaso na upendo wa Mungu. Pale ambapo imani na matumaini vinakosekana wakati mgonjwa anapokaribia kifo kuna hatari ya kutumbukia katika kifolaini au msaada wa kutaka kujinyonga.

Sehemu ya pili ni kuhusu mang’amuzi ya maisha mintarafu mateso ya Kristo sanjari na kutangaza Injili ya matumaini kwa watu wanaoteseka kimwili, kisaikolojia, kimaadili na kiroho. Mama Kanisa anawaalika watoto wake kumwangalia Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani. Wagonjwa katika mateso yao, wanaonja pia upweke hasi, hali ya kukataliwa pamoja na kuteswa kutokana na maumivu, kiasi cha kudhani kwamba, hawana tena thamani wala ubora wowote kiasi kwamba, wamegeuka kuwa ni mzigo mzito usioweza kubebeka tena. Msalaba wa Kristo uwe ni tumaini kwa wale wote wanaoteseka: kimwili, kisaikolojia, kimaadili na kiroho. Wasindikizwe kwa uwepo, sala na maombezi ya Bikira Maria aliyethubutu kusimama chini ya Msalaba wa Kristo Yesu akatiwa shime na upendo wa Baba wa milele. Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kuwaacha waja wake katika upweke! Baada ya mateso na kifo cha Msalaba, kuna ufufuko na uzima wa milele, kielelezo cha imani ya Kanisa na upendo wa Mungu Baba. Huduma shufaa haziwezi kufua dafu, ikiwa kama mgonjwa ametumbukia katika kishawishi na hali ya kujikatia tamaa, mwaliko ni kuendelea kuandamana na Kristo Yesu Msalabani. Wale wote wanaomhudumia mgonjwa wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini, tayari kutangaza upendo wa Kristo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba. Hii ndiyo maana ya maisha ambayo Fumbo la kifo, kamwe haliwezi kuiondoa.

Sehemu ya tatu ni kuhusu Moyo wa Msamaria Mwema Unaoona: Hii ni huduma inayofumbatwa katika huruma na upendo kwa kutambua na kuheshimu Injili ya uhai kwani maisha ni matakatifu na zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Utambuzi huu unaweza kufanywa kwa akili ya kawaida. Ni katika muktadha huu, Mama Kanisa anapenda kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema na waamini wa dini mbalimbali duniani ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu tangu pale anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Maisha, utu na heshima ya binadamu ni kielelezo cha Fumbo la Utatu Mtakatifu. Maisha daima ni mazuri. Kumbe, huu ni mwaliko kwa watu wote kuheshimu na kuthamini utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mwenyezi Mungu ni chanzo na hatima ya maisha ya mwanadamu anayepaswa kuwajibika mbele yake. Thamani na utakatifu wa maisha ya binadamu yanaongozwa na kanuni maadili na sheria zote. Ni kinyume cha kanuni maadili na utu wema, kukatisha maisha ya mgonjwa hata kama mgonjwa mwenyewe ameonesha nia hii kwa uhuru kamili. Mwenyezi Mungu ndiye mwenye mamlaka halali ya kuondoa uhai wa binadamu. Ni kutokana na muktadha huu, utoaji mimba, kifolaini na tamaa ya mtu kutaka kujinyonga au kutoa sumu kwa jumuiya ni matendo yanayokwenda kinyume cha utashi wa Mwenyezi Mungu kwa binadamu.

Sehemu ya nne ya Waraka huu inajihusisha zaidi na tamaduni ambazo ni kikwazo cha utakatifu wa maisha ya binadamu. Utamaduni wa kifo unajenga dhana ya kuwakirimia watu “kifo chenye heshima”, kwa kujikita katika “ubora wa maisha” unaofungamanishwa na mfumo wa uchumi unaotaka kuwapatia watu ustawi, uzuri na furaha ya maisha. Lakini mwelekeo huu, unasahau mambo msingi katika maisha yaani: mafungamano ya kijamii, maisha ya kiroho na mwelekeo wa kidini katika maisha ya mwanadamu. Ni mtazamo wa maisha unaotaka kumuunda mtu ambaye ni mkamilifu bila hitilafu yoyote katika maisha na matokeo yake, ni watu kushindwa kutambua tunu ya maisha katika undani wake. Kikwazo cha pili ni huruma isiyokuwa na ukweli wowote kwa wagonjwa kwa kuwatakia kifolaini au kuwasaidia kujinyonga. Huruma ya kweli kama fadhila ni ile inayomkumbatia mgonjwa na kumsaidia katika shida na mahangaiko yake, kwa kumjali na kujitahidi kumwondolea maumivu!

Lakini si huruma ya machozi ya mamba! Kikwazo cha tatu ni ubinafsi, uchoyo, ukanimungu na unafsia unaotaka kumwondolea mwanadamu udhaifu, mapungufu ya kimwili na magonjwa. Ubinafsi ni kiini cha mtazamo huu tenge katika maisha ya binadamu. Pale wagonjwa wanaposhindwa kujitegemea na kujimudu binafsi, hapo ndipo ambapo ubinafsi unapoanza kutawala kwa kukazia haki ya kifolaini au msaada wa mtu kujinyonga, kwani hapa kipimo ni umuhimu wao katika mfumo mzima wa kiuchumi. Kama mgonjwa hawezi kuzalisha wala kutoa huduma, hana chake hapa duniani. Matokeo yake ni mshikamano na mafungamano ya kijamii kuteleleka; upendo wa Kimungu kutoweka na msaada wa kijamii kukosekana wakati mgonjwa anapokabiliana na changamoto na matatizo ya afya. Watu wanashindwa kuona na kutambua umuhimu wa maisha ya binadamu. Matokeo yake ni utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera na kifolaini na msaada wa kujinyonga, mwelekeo potofu sana katika huduma kwa wagonjwa mahututi na wale walioko kufani!

Sehemu ya tano inafafanua “Magisterium ya Kanisa” yaani “Mamlaka fundishi ya Kanisa: Mamlaka fundishi ya Kanisa inapiga rufuku kifolaini na huduma kwa watu wanaotaka kujinyonga hata katika nchi zile ambazo zoezi hili limeruhusiwa kisheria. Mama Kanisa anafundisha na kutamka kwamba, vitendo vyote hivi ni uhalifu dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Tunu ya maisha, hali ya mtu kujitegemea pamoja na kufanya maamuzi si sawa na ubora wa maisha katika ujumla wake. Kifolaini ni kinyume kabisa cha Sheria ya Mungu. Kwa wale wote wanaohusika na mchakato wote wa kifolaini watambue kwamba, wanatenda dhambi. Watunga sera na sheria ya kifolaini wanatuhumiwa kuwatumbukiza wengine katika kashfa na dhambi inayoendelea kuangamiza dhamiri na hata wakati mwingine miongoni mwa waamimi. Kila maisha ya mwanadamu yana tunu na utu sawa, yanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote. Waamini waongozwe na fadhila ya matumaini, kwa kutambua na kuthamini Injili ya uhai, ili kulinda maisha ya watu kwa kufurahia maana ya maisha. Ni dhana potofu ya kutoa huduma ya kifolaini kwa mgonjwa kwani hakuna haki ya mtu kujinyonga. Kifolaini pamoja na msaada wa kujinyonga ni kinyume cha haki msingi za binadamu. Haya ni matokeo ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani zao na ukosefu wa mshikamano wa upendo na udugu wa kibinadamu. Kuomba kifolaini peke yake ni dalili za mgonjwa ambaye anaelemewa na upweke hasi pamoja na machungu ya maisha.

Katika muktadha huu, Kanisa linaona umuhimu wa toba na wongofu wa ndani, ili mgonjwa aweze kujitakasa na hivyo kuambata na kukumbatia fadhila ya matumaini kwa kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu. Watu wasiue! Bali waoneshe uwepo na mshikamano na wale wanaoteseka na kuomboleza. Kanuni maadili zinazoongoza huduma tete za kitabibu zinapaswa kuhakikisha kwamba mgonjwa anapata matibabu msingi kama sehemu ya haki yake kwa kuondokana na kishawishi cha kutumbukia katika dhambi ya kifolaini na msaada kwa wale wanaotaka kujinyonga. Huduma msingi za lishe na maji zitolewe ikiwa kama hazisababishi madhara kwa mgonjwa; huduma shufaa: (palliative care), ni kielelezo cha huduma ya huruma na upendo inayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni kielelezo cha mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kuguswa na mahangaiko ya mgonjwa ili hatimaye, kumjengea mgonjwa matumaini kwa Mwenyezi Mungu anayeokoa. Wajibu wa familia na vituo vya kutunza wagonjwa ni muhimu sana kwa sababu familia ina wajibu wa kwanza wa kutoa huduma ya kiroho na kimwili kwa mgonjwa. Utu, heshima na haki msingi za mgonjwa zinapaswa kulindwa.

Huduma ya utunzaji mimba na tiba kwa watoto wachanga; tiba ya kupunguza maumivu na hali ya kupoteza fahamu; hali ya mtu kutojitambua pamoja na utambuzi hafifu; dhamiri nyofu kwa wafanyakazi katika sekta ya afya na taasisi za afya zinazomililikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki ni muhimu sana. Sehemu hii inaendelea kufafanua kuhusu: Huduma za kichungaji na msaada wa Sakramenti za Kanisa kwamba, ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo na chemchemi ya matumaini na faraja kwa mgonjwa. Ni wajibu wa Kanisa kumpatia mgonjwa Sakramenti za Uponyaji ambazo ni Kitubio na Mpako Mtakatifu. Hizi ni Sakramenti za uponyaji na wokovu. Mang’amuzi ya kichungaji kwa wagonjwa wanaoomba kifolaini au msaada wa kujinyonga. Mosi, mgonjwa anapaswa kuonesha majuto kamili, maungamo na kutimiza malipizi. Kwa mgonjwa aliyekuwa amejiandikisha kwenye vituo vya kifolaini, anapaswa kwanza kabisa kufuta jina lake huko kabla ya kupokea Sakramenti za Kanisa. Padre mtoa Sakramenti hizi anaweza kufanya mang’amuzi ya kichungaji na hatimaye, kufikia uamuzi wa busara zaidi.

Kanisa linaweza kuchelewesha kutoa maondoleo ya dhambi ili kumsaidia mwamini kutubu na kumwongokea Mungu. Hata hivyo, Kanisa litaendelea kuwa karibu na mgonjwa. Mabadiliko katika mfumo wa elimu na umuhimu wa majiundo makini kwa wafanyakazi katika sekta ya afya mintarafu maisha ya kiroho na kanuni maadili. Huduma hii itolewe kwa mgonjwa na kwa ndugu na jamaa ya mgonjwa. Wafanyakazi wa sekta ya afya katika hospitali zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki hawana budi kupewa miongozo ya Kanisa pamoja na majiundo endelevu, ili waweze kutoa huduma bora zaidi kwa wagonjwa wanaowahudumia, kwa kuwapatia matumaini, huku wakiendelea kuwasindikiza katika fumbo la maisha na neema wakati wanapoendelea kujiandaa kupokea fumbo la kifo katika maisha yao. Waraka wa “Samaritanus Bonus” Yaani: “Msamaria Mwema”: Waraka Kuhusu Huduma Kwa Wagonjwa Mahututi na Walioko Kufani unahitimishwa kwakuwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo katika mateso ya wagonjwa.

Kuna umuhimu wa kuheshimu, kulinda, kupenda na kuhudumia uhai, maisha ya kila mwanadamu sanjari na kuhakikisha kwamba, wagonjwa wanasindikizwa katika hatua mbalimbali za ugonjwa wao kama zilivyofafanuliwa katika Waraka huu. Ni muda wa kumwilisha huruma na mapendo katika matendo halisi. Ikumbukwe kwamba, matendo ya huruma ndicho kipimo cha hukumu ya mwisho! Waraka huu, umeidhinishwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Juni 2020 na kutolewa na Kardinali Luis Francisco Ladaria Ferrer, S.J., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na Askofu mkuu Giacomo Morandi, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa.

Samaritanus Bonus

 

22 September 2020, 12:00