Tafuta

Kardinali Pietro Parolin akiwa nchini Lebanon amesisitizia umuhimu wa kusali na kufunga; toba na wongofu wa ndani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Lebanon. Kardinali Pietro Parolin akiwa nchini Lebanon amesisitizia umuhimu wa kusali na kufunga; toba na wongofu wa ndani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Lebanon. 

Kardinali Pietro Parolin: Lebanon: Umoja na Mshikamano wa Kitaifa

Mateso ya wananchi wa Lebanon yawe ni sehemu ya toba na wongofu wa ndani. Yaimarishe misingi ya haki, amani na maridhiano ili kulinda utu na heshima ya binadamu. Iwe ni fursa ya kutaka kudumisha utawala bora unaowajibika katika misingi ya ukweli na uwazi, ili kudumisha umoja na udugu, kwa kuondokana na ghasia na vurugu. Watu watambue na kuheshimu haki na wajibu wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 3 Septemba 2020 ameshiriki kikamilifu katika mkesha wa Siku ya Kufunga na Kusali kwa ajili ya kuombea ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Lebanon. Hii ni siku maalum iliyotengwa na Baba Mtakatifu Francisko kama kielelezo cha umoja na mshikamano wa kidugu na watu wa Mungu nchini Lebanon. Imekuwa ni fursa ya kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliopoteza maisha, waliopata vilema vya kudumu pamoja na wale waliopoteza mali zao. Huu ni wakati wa kuanza upya kwa ari na moyo mkuu, kwa kujikita katika sala, imani na matumaini. Kardinali Pietro Parolin amekutana na kuzungumza na viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali kama kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu anayeongoza historia ya maisha ya mwanadamu; Mwenyezi Mungu anayependa binadamu wasaidiane na kuhudumiana.

Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko kwa Ijumaa tarehe 4 Septemba 2020 anakazia zaidi: Sala, Kufunga na Mshikamano kwa ajili ya Beirut na Lebanon katika ujumla wake. Watu wengi wameshiriki katika siku hii maalum, kielelezo kwamba, Lebanon, haijaachwa katika upweke, bali inazungukwa zaidi na watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Mateso na mahangaiko ya watu, yawe ni sehemu ya toba na wongofu wa ndani. Yaimarishe misingi ya haki, amani na maridhiano; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea utu na heshima ya binadamu. Iwe ni fursa ya kutaka kudumisha utawala bora zaidi unaowajibika katika misingi ya ukweli na uwazi, ili kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu, kwa kuondokana na ghasia na vurugu. Watu watambue na kuheshimu haki na wajibu wao.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani yaliyoongozwa na kauli mbiu “Siasa safi ni huduma ya amani”. Kwa muhtasari anakazia Injili ya amani kama sehemu ya utume wa Kanisa; Changamoto za siasa safi; Upendo na fadhila za kiutu kwa ajili ya siasa inayohudumia haki msingi na amani; vilema vya wanasiasa; umuhimu wa siasa safi inayowashirikisha vijana na kujengeana imani; anasema, kuna haja ya kukataa kishawishi cha vita na mbinu mkakati wa vitisho, kwa kuwekeza katika mradi mkubwa wa ujenzi wa amani. Kwa upande wake, Kardinali Parolin amewasihi watu wa Mungu nchini Lebanon kuwekeza zaidi miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Lebanon. Viongozi wa kidini na kiserikali, wahakikishe kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao barabara. Waimarishwe kwa umoja na mshikamano wa Kitaifa na Kimataifa kama mfano bora wa kuigwa!

Lebanon: Viongozi
05 September 2020, 08:56