Tafuta

Vatican News
Mkataba wa Helsinki wa Mwaka 1975 ulitiwa mkwaju na Mataifa 35 baada ya kuhitimisha mkutano uliojadili usalama na ushirikiano kati ya Mataifa ya Bara la Ulaya, Mwaka 2020 unatimiza Miaka 45. Mkataba wa Helsinki wa Mwaka 1975 ulitiwa mkwaju na Mataifa 35 baada ya kuhitimisha mkutano uliojadili usalama na ushirikiano kati ya Mataifa ya Bara la Ulaya, Mwaka 2020 unatimiza Miaka 45.  (ANSA)

Kumbukumbu ya Miaka 45 ya Mkataba wa Helsinki 1975: Umuhimu wake!

Kwa mwaka 2020 Mkataba wa Helsinki wa Mwaka 1975, unaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 45 na mwaka mmoja tangu alipofariki dunia Kardinali Achille Silvestrini, yaani tarehe 29 Agosti 2019. Kardinali Achille Silvestrini alikuwa ni mwanadiplomasia wa hali ya juu kabisa, aliyeweza kuchangia uzoefu na mang’amuzi tangu mwaka 1953 hadi mwaka 1988. Ni mwanadiplomasia mahiri sana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkataba wa Helsinki wa Mwaka 1975, ulitiwa mkwaju na Mataifa 35 baada ya kuhitimishwa kwa mkutano uliojadili kuhusu masuala ya usalama na ushirikiano Barani Ulaya, uliofanyika mjini Helnsiki huko nchini Finland kati ya mwezi Julai na Agosti 1975. Huu ni mkutano uliolenga kuboresha mahusiano na mafungamano kati ya Ulaya ya Mashariki na Ulaya ya Magharibi kwa wakati huo. Kwa mwaka 2020 Mkataba wa Helsinki wa Mwaka 1975, unaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 45 na mwaka mmoja tangu alipofariki dunia Kardinali Achille Silvestrini, yaani tarehe 29 Agosti 2019. Kardinali Achille Silvestrini alikuwa ni mwanadiplomasia wa hali ya juu kabisa, aliyeweza kuchangia uzoefu na mang’amuzi tangu mwaka 1953 hadi mwaka 1988. Ni mwanadiplomasia anayekumbukwa sana kwa mchango mzito katika kipindi cha “Ostpolitik Vaticana”; yaani kipindi cha majadiliano kati ya Vatican na Nchi za Ulaya ya Mashariki zilizokuwa chini ya utawala wa Kikomunisti

Mkataba wa Helsinki wa Mwaka 1975 uliweka kanuni 10 ambazo zinafafanua mambo msingi katika uhusiano na ushirikiano yaani: Nchi zote zina mamlaka sawa, kuheshimu haki zilizo katika mamlaka husika; kutotumia nguvu; ukiukaji wa mipaka; uadilifu; utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani; kutokuingiliwa katika mambo ya ndani ya nchi; kuheshimu haki za binadamu pamoja na kudumisha; usawa na haki ya watu kudhibiti hatima ya maisha yao wenyewe; ushirikiano wa kimataifa; kutimiza majukumu ya kisheria ya kimataifa. Ni katika muktadha huu, Jumatatu tarehe 14 Septemba 2020 kumefanyika kongamano kuhusu maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 45 ya Mkataba wa Helsinki wa Mwaka 1975, na mwaka mmoja tangu alipofariki dunia Kardinali Achille Silvestrini, yaani tarehe 29 Agosti 2019.

Kongamano hili liliandaliwa na Ubalozi wa Italia mjini Vatican na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa Italia pamoja na Vatican. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika hotuba yake elekezi kuhusu mchango wa Kardinali Achille Silvestrini anasema, Kanisa lilionesha busara kubwa kwa kutofungamana na upande wowote hali ambayo ilichangia kwa kiasi kikubwa Urussi kuweza kurejesha imani na matumaini kwa Kanisa. Kwa mara ya kwanza Vatican iliweza kuhudhuria mkutano huu kama nchi mwanachama, ili kuchangia katika mchakato wa kanuni maadili, utu wema na uhuru wa kuabudu; mambo msingi katika ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya kijamii na kimataifa. Jumuiya ya Kimataifa ilipaswa kuzibainisha na hatimaye, kuzitambua haki msingi za binadamu.Na huu ulikuwa ni mchango mkubwa kutoka kwa Mtakatifu Paulo VI, sauti na mwono wa kinabii.

Hiki ni kipindi ambacho Kanisa lilikumbana na madhulumu makubwa, kiasi kwamba, utawala wa Kikomunisti, ulipania kufuta Ukristo katika baadhi ya Mataifa. Baadhi ya viongozi wakuu wa Kanisa wakakamatwa na kuwekwa kizuizini na huo ukawa ni mwanzo wa ushuhuda wa uvumilivu, ulioliwezesha Kanisa kufanya hija ya mateso katika baadhi ya Nchi za Ulaya ya Mashariki hususan: Hungaria, Czechoslovakia na Poland. Kanisa likasimama imara bila kufungamana na upande wowote wa kisiasa, kwa kuonesha uvumilivu, uwezo mkubwa, ujasiri na udumifu wa kuendeleza mchakato wa majadiliano tete kati ya Mataifa na hatimaye, matunda ya ushuhuda wa uvumilivu yakaonekana. Kardinali Pietro Parolin amekazia zaidi kanuni inayohusu haki msingi za binadamu zinazojumuisha uhuru wa kutoa mawazo, uhuru wa kidini pamoja na uhuru wa dhamiri.

Mkataba wa Helsinki wa Mwaka 1975 ukawa ni chemchemi ya: utu, heshima na haki msingi za binadamu, zilizopelekea hata kuanguka kwa utawala wa Kikomunisti hapo mwaka 1989. Hii ni sehemu ya mchango mkubwa uliotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwa kukazia pia majadiliano ya kidini na kiekumene. Uhuru wa kidhamiri, ukawa ni mchango mkubwa uliotolewa na Vatican kwenye mkutano wa Helsinki. Mtakatifu Yohane Paulo II alitambua fika kanuni kumi za Mkataba wa Helsinki wa Mwaka 1975 na alizitumia kudai uhuru wa kidini na hii ikawa ni changamoto ya Kimataifa. Huo ukawa ni mwanzo wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini Poland "Solidarność".

Hili ni Shirikisho ambalo limeleta mabadiliko makubwa ya kihistoria nchini Poland na Ulaya ya Kati katika ujumla wake. Kardinali Parolin anahitimisha kwa kusema, Miaka 1960 hadi mwaka 1970 imekuwa ni miaka ya mahusiano baridi na yenye woga kati ya Mataifa, lakini, Mataifa mengi yalionesha ujasiri wa kutaka kudumisha usalama na kuendeleza ushirikiano wa Kimataifa, kwa kudumisha misingi ya amani na haki msingi za binadamu. Huu ukawa ni mwanzo wa majadiliano katika ukweli na uwazi, silaha madhubuti katika mchakato wa ujenzi wa amani duniani, pamoja na kulinda haki msingi, utu na heshima ya binadamu.

Mkataba

 

15 September 2020, 14:43