Tafuta

Kardinali Mario Zenari: Machafuko ya kisiasa na vita nchini Siria ni chanzo cha majanga yanayoendelea kuwaandama wananchi wa Siria. Kardinali Mario Zenari: Machafuko ya kisiasa na vita nchini Siria ni chanzo cha majanga yanayoendelea kuwaandama wananchi wa Siria. 

Vita Nchini Siria Ni Chanzo Cha Maafa Makubwa Kwa Watu!

Kardinali Zenari katika mahojiano na Vatican News anabainisha kwamba, miaka 10 ya vita nchini Siria imepelekea kuporomoka kwa masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii, kiasi kwamba, hata leo hii watu wengi wameanza kupoteza matumaini kwa Siria iliyo bora zaidi kwa leo na kwa kesho. Kuna haja ya kuanzisha mchakato wa kujikita katika kuwajengea wananchi wa Siria matumaini mapya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Vita nchini Siria ilifumuka rasmi tarehe 15 Machi 2011 na tangu wakati huo, zaidi ya wananchi milioni 12 hawana makazi ya kudumu; wengi wao wamelazimika kuikimbia nchi yao ili kutafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi, kutokana na kuandamwa na baa la njaa, umaskini na magonjwa. Mara nyingi Baba Mtakatifu Francisko anasema hii ni Vita ya Tatu ya Dunia inayopiganwa vipande vipande. Wananchi wa Siria wameshindwa kuaminiana kutokana na machafuko ya hali ya hewa kisiasa na mashambulizi ya mara kwa mara yanayojitokeza nchini humo ambayo kwa hakika yamekuwa ni chanzo cha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kardinali Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Siria ambaye amekuwemo nchini Siria kwa kipindi hiki chote cha vita na mauaji ya kimbari, anakaza kusema, kamwe hajakata tamaa ya matumaini na ujasiri wa kuendelea kutangaza na kushuhudia furaha, ari na mwako wa Kiinjili  nchini Siria. Kardinali Zenari katika mahojiano na Vatican News anabainisha kwamba, miaka 10 ya vita nchini Siria imepelekea kuporomoka kwa masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii, kiasi kwamba, hata leo hii watu wengi wameanza kupoteza matumaini kwa Siria iliyo bora zaidi kwa leo na kwa kesho.

Kuna haja ya kuanzisha mchakato wa kujikita katika kuwajengea wananchi wa Siria matumaini mapya. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hotuba yake kwa mabalozi na wawakilishi wa nchi zao mjini Vatican, Januari 2020 alisema kwamba, inasikitisha kuona maafa makubwa ya watu na mali zao nchini Siria yanaanza kuzoeleka na hatimaye, kukosa nafasi kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii. Hali tete ya Mashariki ya Kati kwa sasa ndiyo inayopewa kipaumbele cha kwanza. Wananchi wa Siria wanaendelea kupoteza maisha kutokana na aina mbalimbali za silaha: Kuna mabomu ya kurushwa na yale yanayotegwa ardhini, bila kusahau silaha za kinyuklia. Hakuna jambo linalosikitisha kuona kwamba, mtu anapoteza maisha na wala hakuna anayesikitika wala kujali. Makali ya vita yanaendelea kupungua, lakini watu wa Mungu wanakabiliana na umaskini mkubwa wa hali na kipato.

Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 80 % ya wananchi wote wa Siria ni maskini na haki zao msingi zinaendelea kusiginwa kutokana na baa la njaa, utapiamlo wa kutisha miongoni mwa watoto wa Siria pamoja na magonjwa mengine. Ni katika muktadha huu, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujielekeza zaidi katika ujenzi wa Siria mpya, kwa kuhakikisha kwamba, kiasi cha Euro bilioni 4 kinapatikana. Siria pia inahitaji kuanza mchakato wa diplomasia, amani, upatanisho na maridhiano kati ya watu wa Siria. Ili kuweza kufikia hatua hii, kuna haja pia kujenga na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuaminiana na kuheshimiana. Ikiwa kama demokrasia shirikishi itafufuliwa hapana shaka kwamba, hata uchumi wa Siria, utaweza kuanza kuboreka taratibu. Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya watu wanaendelea kunufaika kutokana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Kuna baadhi ya makampuni ya kigeni na kimataifa yanaendelea kujichotea mafuta ghafi kwa kiwango cha kutisha sana. Watu wanaotafuta mbao, wamekuwa wakikata miti kana kwamba “hiki ni kichwa cha mwendawazimu”. Kana kwamba, mambo yote haya hayatoshi, kuna baadhi ya makapuni makubwa makubwa ya kigeni yamekwapua maeneo makubwa ya ardhi kwa ajili ya mafao binafsi. Kardinali Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Siria,  anasema, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kusaidia kuboresha hali tete ya kisiasa na kivita nchini Siria kwanza kabisa kwa kuboresha hali ya magereza nchini Siria. Kuna wafungwa wanaoendelea kupoteza maisha yao wakiwa kifungoni. Kuna watu wamepotea katika hali na mazingira tete. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinabainishwa kwamba, kuna zaidi ya watu 10, 000 wamepotea katika mazingira ya kutatanisha na hawajulikani mahali walipo! Kati yao kuna Maaskofu wawili wa Aleppo pamoja na Mapadre watatu ambao kati yao yumo Padre Paolo Dall’Oglio, SJ., ambaye kwa muda wa miaka sita, hajulikani mahali alipo. Ujenzi mpya wa Siria hauna budi kwanza kabisa kupyaisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa wafungwa, watu waliotekwa nyara pamoja na wale wote waliopotea katika mazingira ya kutatanisha!

Umoja wa Mataifa, Kanisa pamoja na Mashirika mbalimbali ya kujitolea, yanaendelea kuwekeza sana katika mchakato unaopania kufufua uchumi na hali ya maisha ya wananchi wa Siria katika ujumla wao. Kuna zaidi ya watu milioni 11 wanaohitaji msaada wa dharura. Kumbe, kuna haja kwa Wasamaria wema kujitokeza zaidi kwa ajili ya kusaidia mchakato wa ujenzi mpya wa Siria kwa kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya hospitali, shule pamoja na nyumba za ibada. Kuna wanafunzi ambao hatima ya maisha yao kwa siku za usoni iko mashakani. Hali ngumu ya maisha inachagizwa pia na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Hali tete  Ukanda wa Mashariki ya Kati pamoja na mlipuko wa Lebanon ni kati ya mambo yanayoendelea pia kuwaathiri wananchi wa Siria. Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa ujenzi wa Siria mpya, kama kielelezo cha mshikamano wa upendo. Kanisa linataka kuwa ni sauti wa wanyonge, kwa kuwekeza zaidi katika huduma makini za afya, elimu, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu yanayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili.

Huu ni msingi wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali na ushuhuda wa uekumene wa damu na huduma kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko. Kuna haja ya kuganga na kutibu miili sanjari na kuboresha mahusiano na mafungamano ya kijamii. Ni katika muktadha huu, Kanisa linataka kusimama na kuwahudumia wananchi wote wa Siria bila ubaguzi. Hiki ndicho kiini cha diplomasia ya Vatican yaani: Utu, heshima, haki msingi, ustawi na maendeleo ya wote! Mateso na mahangaiko ya watoto wasiokuwa na hatia, wanawake na wazee ni jambo ambalo linatesa sana! Wakati wote huu, Baba Mtakatifu Francisko ameonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wa Mungu nchini Siria. Ni kielelezo cha ushuhuda wa Kanisa linalotangaza Injili ya matumaini kwa wale wote wanaoteseka, waliovunjika na kupondeka moyo. Baba Mtakatifu bado ametia nia ya kutembelea Siria mambo yatakapokuwa shwari!

Kardinali Zenari
22 September 2020, 08:11