Tafuta

Vatican News
Jukwaa la Maonesho ya Sayansi Kimataifa kwa Mwaka 2020 (ESOF) limefunguliwa rasmi mjini Trieste, Italia kuanzia tarehe 2 Septemba hadi 6 Sept. 2020. Jukwaa la Maonesho ya Sayansi Kimataifa kwa Mwaka 2020 (ESOF) limefunguliwa rasmi mjini Trieste, Italia kuanzia tarehe 2 Septemba hadi 6 Sept. 2020.  (ANSA)

Jukwaa la Maonesho ya Sayansi Kimataifa Lazinduliwa Mjini Trieste

Jukwaa la Maonesho ya Kisayansi Kimataifa kwa Mwaka 2020 “EuroScience Open Forum (ESOF) 2020 ni tukio la maonesho ya kisayansi linaloadhimishwa kila baada ya miaka miwili na kwa mwaka 2020 linaadhimishwa kuanzia tarehe 2-6 Septemba, 2020 kwa kutambua kwamba, mji wa Trieste ulioko nchini Italia umeteuliwa kuwa ni Mji Mkuu wa Jumuiya ya Ulaya kwa Masuala ya Sayansi, 2020

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 2 Septemba 2020 kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amezindua rasmi Jukwaa la Maonesho ya Kisayansi Kimataifa kwa Mwaka 2020 “EuroScience Open Forum (ESOF) 2020. Hili ni tukio la maonesho ya kisayansi linaloadhimishwa kila baada ya miaka miwili na kwa mwaka 2020 linaadhimishwa kuanzia tarehe 2 Septemba hadi tarehe 6 Septemba 2020 kwa kutambua kwamba, mji wa Trieste umeteuliwa kuwa ni Mji Mkuu wa Jumuiya ya Ulaya kwa Masuala ya Sayansi. Zaidi ya matukio 150 yanayohusiana na mikutano na maonesho yanafanyika ili kukazia majadiliano  ya kina kati ya teknolojia, sayansi na masuala ya kisiasa. Kiini cha majadiliano yote haya ni maendeleo fungamani, mazingira na afya ya umma, hasa ukizingatia madhara makubwa yaliyoletwa na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Kardinali Pietro Parolin, amewashikirika wahusika mambo msingi yaliyomo kwenye Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Huu ni Waraka unaozungumzia kwa muhtasari mambo yanayotokea katika mazingira; Injili ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa ekolojia vinavyohusiana na watu; Ekolojia msingi; Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni elimu ya ekolojia na maisha ya kiroho. Kardinali Parolin ameyadadavua yote haya wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Kipindi cha Kazi ya Uumbaji kuanzia tarehe 1 Septemba hadi tarehe 4 Oktoba 2020. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko umepokelewa kwa mikono miwili kama kielelezo cha moyo wa shukrani, ikizingatiwa kwamba, mji wa Trieste umezungukwa na vituo vingi vya tafiti za kisayansi, pengine kuliko mji mwingine wowote nchini Italia anasema, Askofu Giampaolo Crepaldi wa Jimbo Katoliki la Trieste.

Mji huu umekuwa ni maabara ya imani na sayansi, kama utekelezaji wa changamoto iliyotolewa wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Jimbo Katoliki la Trieste. Kwa sasa kuna mchakato wa kuanzisha taasisi itakayofanya tafiti mahususi mintarafu kanuni maadili na utu wema, sayansi na taalimungu katika muktadha wa majadiliano ya kiekumene. ESOF inapania pamoja na mambo mengine kukoleza majadiliano kati ya sayansi, teknolojia,  jamii na masuala ya kisiasa. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika hotuba yake amekazia umuhimu wa tafiti zinazomhusu mwanadamu katika ukamilifu wake!

Trieste 2020
03 September 2020, 14:21