Tafuta

Vatican News
Bi Asia Bibi Bi Asia Bibi   (AFP or licensors)

Asia Bibi:Lazima kukomesha ndoa za utotoni!

Bi Asia Bibi ni mwanamke wa Pakistan katika mahojiano kwa njia ya video na Mkurugenzi wa Shirika la Kipapa la Kanisa Hitaji anamshukuru Papa kwa ukaribu wake na msaada wa imani.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Asia Bibi amefanya mahojiano yanaogusa sana kwa njia ya video na Alessandro Monteduro mkurugenzi wa Shirika la Kipapa la Kanisa hitaji (ACS),ambaye ameelezea maneno yake ya  nguvu hasa akiomba kukomesha janga la ndoa za utotoni. Bi Asia asili ya Pakistan ni ishala ya mateso kutokana na mateso ya wakristo ambaye amebainisha juu ya janga kubwa la wanawake wengi wadogo sana nchini Pakistan waliotekwa nyara, waliolazimishwa kubadili dini zao, waliolazimishwa kuolewa kwa nguvu wakiwa wadogo.  Hata hivyo inatosha kutaja majina mawili kati ya wengi: Huma Younus na Maira Shahbaz, ambao kwa sasa ni wanaharakati wa kuhamasisha kukomesha janga hili kwa upande Shirika la Kipapa la Kanisa Hitaji ACS.

Kutoka taarifa iliyotolewa na Shirika la Kanisa Hitaji, kwa mujibu wa Asia Bibi ameomba mamlaka kuu ya Pakistan kuwasaidia wasichana hao kwa sababu hasiwepo hata mmoja anayeteseka. Vile vile Asia hakukosa kuomba kuwa nchini Pakistan iweze kuhakikishia kwa wote uhuru wa kidini hasa kwa wale walio wachache wapate ulinzi wa usalama wao, akikimbusha kuwa mwanzilishi wa nchi ya Pakistan Ali Jinnah, alikuwa akisisitiza kwamba uhuru wa dini na maoni ya kujieleza lazima yahakikishiwe ulinzi kwa wazalendo wote.

Katika mahojiano hayo na ambayo yametangazwa katika jukwaa la YouTube ya ACS, Italia, Asia Bibi kwa mara nyingine tena ameelezea shukrani zake kwa Papa Francisko. “Mimi nina rosari mbili nilizopewa na Baba Mtakatifu, moja ilibaki Pakistan na moja ninayo na kila siku ninasari Rosari kwa ajili ya imani na kwa ajili ya wanaoteswa nchini Pakistan. Ninamshukuru Baba Mtakatifu Francisko na Papa Benedikto ambao waliingilia kati kwa ajili yangu na shukrani kwenu Shirika la Kipapa la Kanisa Hitaji (ACS) na watu wengi wa Italia ambao walisali kwa ajili yangu”.  Monteduro, kwa niaba ya Shirika la Kipapa la Kanisa Hitaji (ACS), alimkaribisha Asia Bibi na familia yake mjini Roma, mwaliko ambao ulipokelewa kwa haraka na furaha ya matumaini ya kuweza kukutana na Baba Mtakatifu na ambaye alisema anawaimarisha katika imani yao.

Ikumbuke Mwanamke huyo Asia  Bibi ambaye mwaka 2010 alihukumiwa kunyongwa na Mahakama nchini Pakistan, alijikuta akiachiwa huru baada ya kukata rufaa juu ya hukumu hiyo. Hasa baada ya kundi la wanaharakati na wanasheria kupinga hukumu hiyo kwa zaidi ya miaka mitano. Hatua hiyo ya mahakama ilizua gumzo nchini humo, ambapo maelfu ya watu wenye itikadi  kali waliaandama kwa wingi mwezi Novemba 2018 wakitaka mwanamama huyo anyongwe. Shukrani kwa Mungu mwenyezi, Bi Asia Bibi ameweza kutoka nchini mwake na kukaribishwa nchini Canada.

09 September 2020, 16:03