Tafuta

Vatican News
Waraka: Maagizo Wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa: Kardinali Stella: Parokia ya Kitovu cha toba, wongofu na uinjilishaji wa kina. Waraka: Maagizo Wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa: Kardinali Stella: Parokia ya Kitovu cha toba, wongofu na uinjilishaji wa kina.  (AFP or licensors)

Parokia ni Kitovu cha Wongofu na Utume Wa Uinjilishaji Kanisani

Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa” unapania kupyaisha ari na mwamko wa wito na utume wa kimisionari. Parokia ni kitovu cha uinjilishaji na ni mahali ambapo maisha ya Kisakramenti yanapewa uzito wa pekee sanjari na ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, tarehe 29 Juni 2020 limechapisha Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa”. “Instruction: The pastoral conversion of the Parish community in the service of the evangelising mission of the Church.” Waraka huu, umegawanyika katika Sura 11, lakini unaweza kufupishwa na kugawanywa katika sehemu kuu mbili yaani: Sura ya Kwanza hadi Sura ya sita. Hapa, Waraka  unajadili kuhusu wongofu wa kichungaji, maana ya umisionari na tunu msingi za maisha ya Parokia katika ulimwengu mamboleo. Sehemu ya Pili ni kuanzia Sura ya Saba hadi Sura ya Kumi na moja. Hapa Waraka unajikita katika mchakato wa mgawanyo wa Parokia, dhamana na nyajibu mbali mbali ndani ya Parokia na jinsi ya kutekeleza sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Mama Kanisa. Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Wakleri katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa” unapania kupyaisha ari na mwamko wa wito na utume wa kimisionari katika maisha na utume wa Kanisa na umuhimu wa Parokia kama kitovu cha uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Parokia, ni mahali ambapo maisha ya Kisakramenti yanapewa uzito wa pekee sanjari na ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha imani tendaji. Parokia ni mahali ambapo, utamaduni wa watu kukutana unapaswa kujengwa na kudumishwa, ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene; mshikamano pamoja na kuendelea kuwa wazi kwa ajili ya watu wote. Jumuiya ya Kiparokia inapaswa kuwa ni wasanii wa utamaduni wa ujirani mwema, kama kielelezo na ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa kwa namna ya pekee katika Injili ya huduma. Pamoja na ukweli huu, Mama Kanisa anatambua kwamba, kuna uhaba mkubwa wa miito ya Kipadre katika baadhi ya maeneo, kiasi kwamba, mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache katika shamba la Bwana. Kumbe, kuna haja ya kuwa na mwelekeo na utambuzi mpya wa “dhana ya Parokia”.

Kardinali Beniamino Stella, anakaza kusema, huu ndio mchakato wa mageuzi na upyaishaji wa Parokia unaoendelea katika maisha na utume wa Kanisa, sehemu mbali mbali za dunia. Mchakato huu, hauna budi kuratibiwa na Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati. Katika muktadha huu, upyaisho huu unapaswa kuliangalia Kanisa zima si tu kama Kanisa mahalia! Upyaisho wa huduma Parokiani hauna budi kujikita katika miundombinu ya kimisionari iliyoko Parokiani. Huu ni mwaliko wa kujikita zaidi katika masuala ya maisha ya kiroho na wongofu wa kichungaji unaokita mizizi yake katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Parokia inapaswa kuwa ni Jumuiya ya waamini inayoinjilisha na kuinjilishwa. Hii ni Jumuiya inayotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji!

Ni mahali muafaka pa waamini kukutana, ili hatimaye, kuweza kuutafakari Uso wa huruma ya Mungu katika kina na mapana yake. Ni mahali muafaka pa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Parokia ni mahali pa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kurithisha imani, ili kuziwezesha familia kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Kardinali Beniamino Stella anafafanua zaidi kwa kusema kwamba, upyaisho wa kimisionari unalenga kuwahamasisha wabatizwa wote kutambua uzuri wa imani na furaha ya Injili, tayari kuwashirikisha watu wengine, mang’amuzi haya ya maisha ya kiroho baada ya kukutana na Kristo Mfufuka. Ni nafasi ya kuendeleza mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, ili hata wale waliokuwa wamesahau “mlango wa Kanisa” waweze kurejea tena na kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu anataka kutembea na kuambatana nao katika safari ya maisha yao ya kila siku! Huu ni mpango mkakati wa shughuli za kichungaji ambao ni shirikishi, kwa sababu waamini wote katika umoja na tofauti zao, wameitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Kardinali Beniamino Stella anasema, huu ni wakati muafaka kwa waamini kuwaendea jirani zao, huko “vijiweni” ili kuwatangazia na kuwashuhudia ile furaha ya Injili, kwa wale ambao bado wanatafuta fursa ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao. Mapadre, watawa, mashemasi na waamini walei kwa pamoja, wanapaswa kujifunga kibwebwe kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ni wakati wa kutumia rasilimali muda na uwepo kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Kwa kuthamini familia kama shule ya kwanza ya uinjilishaji, huruma na upendo. Hapa ni mahali ambapo wanafamilia wanapaswa kujisikia kuwa wako salama salimini. Kuna haja ya Parokia kuendelea kushirikiana na kushikamana, ili kujenga Jumuiya kubwa zaidi ya watu wanaoinjilisha na kuinjilishwa. Katika mchakato huu, Paroko anapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa na watu wa Mungu katika mchakato wa uinjilishaji mpya. Wote wanaitwa na wanahamasishwa kushiriki katika safari hii ya imani, chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani unaofumbatwa katika ari na mwamko wa kimisionari!

Parokia 2020
13 August 2020, 07:19