Tafuta

Papa Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Fabio Salerno kuwa Katibu wake muhtasi kuanzia tarehe 1 Agosti 2020 Papa Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Fabio Salerno kuwa Katibu wake muhtasi kuanzia tarehe 1 Agosti 2020 

Padre Fabio Salerno Ateuliwa Kuwa Katibu Muhtasi wa Papa

Padre Fabio Salerno alizaliwa tarehe 25 Aprili 1979, huko Catanzaro. Tarehe 19 Machi 2011, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre, Jimbo kuu la Catanzaro-Squillace. Padre Salerno anachukua nafasi ya Monsinyo Yoannis Lahzi Gaid ataendelea kuwa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Hati ya Udugu wa Kibinadamu. Mons. Gaidi aliteuliwa na Papa Francisko, Mwezi Aprili 2014. Sasa amemaliza muda wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Jumamosi tarehe 1 Agosti 2020 amebainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, amemteua Mheshimiwa Padre Fabio Salerno kuwa Katibu wake muhtasi. Hadi kuteuliwa kwake, Padre Fabio Salerno alikuwa ni Afisa katika Idara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, Padre Fabio Salerno alizaliwa tarehe 25 Aprili 1979, huko Catanzaro. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 19 Machi 2011, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre, Jimbo kuu la Catanzaro-Squillace, nchini Italia. Baadaye Padre Fabio Salerno alijiendeleza kwa masomo ya juu na hatimaye kujipatia shahada uzamivu katika Sheria na Taratibu za Uendeshaji wa Kesi Mahakamani “Utroque Iure” kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran, kilichoko mjini Roma.

Katika maisha na utume wake katika masuala ya diplomasia ya Kanisa, amebahatika kutoa huduma kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Indonesia, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Baraza la Umoja wa Ulaya, kwenye Makao yake Makuu huko mjini Strasburgy, nchini Ufaransa. Padre Fabio Salerno atashirikiana kwa sasa na Padre Gonzalo Aemilius, kutoka Uruguay aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko mwanzoni mwa Mwezi Januari, 2020 na hivyo kuchukua nafasi iliyokuwa imeachwa wazi na Monsinyo Fabián Pedacchio Leániz. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemshukuru na kumpongeza Monsigno Yoannis Lahzi Gaid, aliyeteuliwa tangu mwezi Aprili 2014 kuwa Katibu muhtasi wa Baba Mtakatifu Francisko. Kwa sasa amemaliza utume wake kama Katibu muhtasi wa Papa.

Lakini Monsigno Yoannis Lahzi Gaid ataendelea kuwa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa sahihi kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Huu ni mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hati ya Udugu wa Kibinadamu inapata chimbuko lake katika mikutano elekezi iliyowasaidia waamini wa dini hizi mbili kushirikishana: furaha, majonzi, matamanio yao halali pamoja na changamoto mamboleo.

Katibu Muhtasi

 

01 August 2020, 14:49