Tafuta

Kumbukumbu ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Changamoto ni wongofu wa kisiasa na kiutu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ili kukabiliana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Kumbukumbu ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Changamoto ni wongofu wa kisiasa na kiutu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ili kukabiliana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19. 

Kumbukumbu ya Mt. Inyasi wa Loyola: Wongofu wa Kisiasa na Kiutu!

Maisha na utume wa Wayesuit ulimwenguni umebadilika sana kutokana na janga la ugonjwa wa COVID-19. Kumekuwepo na ongezeko la viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanaotawala kibabe, hali ambayo inahatarisha sana, mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Shida na changamoto zote hizi ni fursa ya kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 31 Julai, anaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola, Muasisi wa Shirika la Wayesuit duniani. Wayesuit katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa, wanapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mambo makuu yafuatayo: Kuendeleza mchakato wa mang’amuzi na mafungo ya kiroho; Kushikamana na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; Kuwasindikiza vijana katika safari ya maisha yao; Mwishoni, kutunza mazingira nyumba ya yote. Haya ni mambo ambayo yanabainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika barua aliyomwandikia Padre Arturo Sosa, Mkuu wa Shirika ya Wayesuit kama sehemu ya mpango mkakati wa maisha na utume wao katika kipindi cha miaka kumi yaani kuanzia mwaka 2019-2029. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hivi pia ndivyo vipaumbele vya Kanisa la Kiulimwengu kwa wakati huu! Mambo ambayo yanapaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya Sinodi za Maaskofu na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia.

Padre Arturo Sosa, Mkuu wa Shirika ya Wayesuit, katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola kwa Mwaka 2020, akihojiwa na Vatican News anabainisha kuhusu: Maisha na utume wa Wayesuit ulimwenguni na jinsi ambavyo umebadilika sana kutokana na janga la ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19; kumekuwepo na ongezeko la viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanaotawala kibabe, hali ambayo inahatarisha sana, mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Shida na changamoto zote hizi ni fursa ya kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limesababisha madhara makubwa katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii, kisiasa, kiuchumi, kitamaduni, kifamilia na hata maisha ya kiroho. Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 limebadilisha vipaumbe vya maisha na utume wa Wayesuit sehemu mbali mbali za dunia na kwa sasa wameanza kujikita katika mapambano dhidi ya janga ili, kwa kuhakikisha kwamba, waathirika wanapata mahitaji yao msingi kama kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Hii ni changamoto ya umoja na mshikamano na ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa kutambua kwamba, watu wote wanategemeana na kukamilishana kama inavyojionesha katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Gonjwa hili limegusa na kutikisa misingi ya maisha ya kiroho na hivyo kusababisha ukame wa maadhimisho ya Ibada na Sakramenti za Kanisa. Malengo na vipaumbele vya watu vimebadilika sana, leo hii Wayesuit wanapenda kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwasaidia kutambua hatua ambazo wanapaswa kupiga katika hija ya maisha na utume wao hapa duniani baada ya kuzuka kwa janga la Virusi vya Corona- COVID-19. Kuna umuhimu wa kuleta mabadiliko makubwa katika mifumo ambayo inaendeleza na kudumaza ukosefu wa haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Ni wakati wa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote. Mwishoni, ni kujenga na kuendeleza utamaduni wa kuwasikiliza vijana na kujibu changamoto, shida na matamanio yao halali kwa sasa na kwa siku za usoni.

Janga kubwa la Virusi vya Corona, COVID -19 limesababisha kudumaa kwa demokrasia ya kweli sehemu mbali mbali za dunia, kiasi kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inashuhudia kuibuka kwa viongozi wanaowaongoza wananchi wao kwa ubabe, kiasi hata cha kujikuta wanatumbukia katika uvunjwaji wa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mfano halisi ni kuhusu sera na mikakati ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, hali ambayo inagumisha mchakato wa ujenzi wa dunia ambayo inasimikwa katika misingi ya haki, amani na udugu wa kibinadamu. Nyanyaso na dhuluma dhidi ya wakimbizi na wahamiaji ni hatari sana kwa umoja na mafungamano miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa. Matokeo yake ni kuendelea kukua na kukomaa kwa biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo inayodhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 iwe ni fursa ya kupiga hatua mbele katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika ukarimu, demokrasia ya kweli, haki, amani na udugu wa kibinadamu.

Padre Arturo Sosa, Mkuu wa Shirika ya Wayesuit anakaza kusema, changamoto, matatizo na fursa hizi, zinapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Fumbo la Msalaba, liwe ni kigezo muhimu katika kuchagua vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa. Jumuiya ya Kimataifa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali inapaswa kuhakikisha kwamba, hata maskini wanapata huduma bora ya afya, elimu na mahitaji yao msingi kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Sera na mikakati mbali mbali iwasaidie vijana kupata fursa za ajira, ili waweze kuwa na leo na kesho yenye matumaini zaidi katika maisha na utume wao. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni changamoto changamani inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika umaskini wa hali na kipato, magonjwa na ujinga.

Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Wayesuit sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni mwaliko kwa waamini kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu. Kwa kukutana na kumwambata Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, waamini wanakirimiwa amani, utulivu na uhuru wa ndani, kwa kujiaminisha chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Kumbe, dhamiri nyofu inakuwa ni mahali patakatifu ambamo Mwenyezi Mungu anakutana na kuzungumza na mja wake, tayari kuinafsisha sala katika huduma ya upendo, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Waamini wawe makini kusoma alama za nyakati, huku wakiwa tayari kutambua na kukiri uwepo endelevu wa Mungu katika historia, ili hatimaye, hata wao, waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini wajenge utamaduni wa kuchunguza dhamiri zao kila siku, ili kufanya mlingano kati ya maisha yao ya kiroho na ushuhuda wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake katika maisha ya hadhara.

Padre Arturo Sosa, Mkuu wa Shirika ya Wayesuit anasema, kuna haja kwa Wayesuit kushirikiana kwa karibu sana na waamini walei katika kuadhimisha Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa, ili hatimaye, waamini waweze kutoka kifua mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika maisha yao kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa tunu msingi za maisha ya Kikristo! Huu ni mwaliko wa kuendelea kujikita katika wongofu wa shughuli za kichungaji, tayari kusaidiana na kusindikizana katika maisha ya kiroho, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Mafungo ya kiroho yanayotolewa na Wayesuit sehemu mbali mbali za dunia ni zawadi ya Mungu kwa waja wake.

Padre Arturo Sosa, Mkuu wa Shirika ya Wayesuit anasikitika kusema kwamba, maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 yanaendelea kuleta madhara makubwa sana hasa katika Nchi za Amerika ya Kusini. Hii inatokana na ukweli kwamba, hakuna miundombinu ya kisiasa ambayo imekuwa tayari kukabiliana na dharura ya janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Kuhusu hali ya miito ya Daraja Takatifu ya Upadre anasema, kumekuwepo na upungufu mkubwa wa vijana wanaoingia Shirika la Wayesuit kutoka katika Bara la Ulaya na Marekani ambako kwa miaka mingi walizoea kupokea makundi makubwa ya vijana waliotamani kujiunga na Shirika la Wayesuit. Lakini hata hivyo, ubora umeongezeka na kuimarika zaidi. Kuna makundi makubwa ya vijana kutoka Barani Afrika na Asia wanaoendelea kufundwa usiku na mchana, ili kuweza kutekeleza dhamana, maisha na utume wa Wayesuit, sehemu mbali mbali za dunia.

Padre Arturo Sosa, Mkuu wa Shirika ya Wayesuit  anahitimisha kwa kusema kwamba, haya ni malezi ya awali na endelevu yanayochukua muda mrefu, ili kuweza kuwapika barabara vijana hawa, ili waweze kuwa tayari kupambana na changamoto katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kwa sasa hakuna wazo na kuanzisha Shirika la Watawa wa Kike kwa Wayesuit, lakini kama Shirika litaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na wanawake katika vituo vyao vya tasaufi, maisha ya kijamii na katika taasisi za elimu, ili kutekeza maisha na utume wa Wayesuit sehemu mbali mbali za dunia!

Wayesuit 2020

 

 

 

01 August 2020, 07:46