Tafuta

Vatican News
Vatican inasema wahanga wa mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo wanapaswa kupewa ulinzi kamili na kusaidiwa kurejea tena katika maisha ya kawaida. Vatican inasema wahanga wa mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo wanapaswa kupewa ulinzi kamili na kusaidiwa kurejea tena katika maisha ya kawaida. 

Vatican: Mapambano Dhidi ya Utumwa Mamboleo ni Muhimu!

Vatican inasikitisha kuona kwamba, wahanga wa biashara haramu ya binadamu pamoja na utumwa mamboleo, bado wanaendelea kukumbana na unyanyapaa katika jamii, na wakati mwingine wanaadhibiwa. Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuanzisha mikati itakayotoa ulinzi kamili sanjari na kuwasaidia waathirika hatua kwa hatua kuanza tena kurejea katika maisha ya kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa katika ulimwengu mamboleo, inakabiliana na uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu kutokana na: vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kidini na kikabila. Kuna umaskini mkubwa wa hali na kipato; uhalifu unaofanywa na magenge ya kitaifa na kimataifa pamoja na kuendelea kuibuka kwa mifumo mipya ya utumwa mamboleo pamoja na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake. Yote haya ni mambo yanayonyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Biashara ya binadamu na viungo vyake ni donda ndugu katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko ambaye ameendelea kulivalia njuga suala hili na biashara haramu ya binadamu aliwahi kusema kwamba, kuna haja ya kuhakikisha kuwa watu hawa wanapewa haki zao msingi, uhuru na utu wao kama binadamu unaheshimiwa na kuthaminiwa; kwa kuwaonesha ukarimu na kuwapatia hifadhi; ili hatimaye, waweze kurejeshwa tena katika maisha ya kijamii. Watu waoneshe ujasiri wa kuwafichua wale wote wanaojihusisha na biashara haramu ya binadamu na vyombo vya ulinzi, sheria na haki vitekeleze dhamana na wajibu wake pasi na makunjanzi. Inasikitisha kuona kwamba, watu wanatumia umaskini na ujinga wa watu kuwanyanyasa kwa kuwatumbukiza katika biashara haramu ya binadamu na hatimaye, kuwageuza kuwa ni vyombo vya kutosheleza tamaa zao mbovu!

Shirika la Kazi Duniani, ILO linasema kwamba, si rahisi kuweza kupata idadi kamili ya watu wanaotumbukizwa katika utumwa mamboleo. Wanawake na watoto ndio waathirika wakuu wa biashara haramu ya binadamu wanaounda walau asilimia 70% ya zaidi ya watu millioni ishirini na moja. Wengi wao ni wale wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya ngono; asilimia 40% wako katika hali ya utumwa kamili. Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Ivan Jurkovič, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, nchini Uswiss, hivi karibuni, ameshiriki katika mkutano wa 44 wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa “United Nations Human Rights Council, kifupi: UNHRC” kwa kukazia umuhimu wa kuwajengea uwezo wa kiuchumi waathirika wa biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Mwelekeo huu unapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Ujumbe wa Vatican unasema, inasikitisha kuona kwamba, wahanga wa biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na utumwa mamboleo, bado wanaendelea kukumbana na unyanyapaa katika jamii, na wakati mwingine wanaadhibiwa.

Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuanzisha sera na miakati itakayotoa ulinzi kamili sanjari na kuwasaidia waathirika hatua kwa hatua kuanza tena kurejea katika maisha ya kijamii. Mali na fedha inayotaifishwa kutoka kwa wale wote wanaojihusisha na biashara ya binadamu na viungo vyake, isaidie kuwajengea uwezo wa kiuchumi waathirika hawa. Jambo la msingi ni kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasimama kidete kupambana na biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja “kufyekelea mbali” mifumo yote ya utumwa mamboleo, kwani matukio kama haya hayapaswi kuwa na nafasi katika Jumuiya ya Kimataifa. Kumekuwepo na maendeleo makubwa katika mapambano dhdi ya biashara na mifumo ya utumwa mamboleo, lakini matukio yote haya yanaendelea kuwa ni donda ndugu katika maisha ya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Kuna baadhi ya watu ambao wametumia mianya ya vita na ghasia; baa la ujinga, maradhi na magonjwa; rushwa na ufisadi pamoja na janga la Virusi vya Corona, COVID-19 kutaka kuendelea kujinufaisha kwa kujipatia utajiri wa haraka haraka.

Askofu mkuu Ivan Jurkovič, anasikitika kusema kwamba, biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo ni donda ndugu katika ulimwengu mamboleo. Hii ni biashara inayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, kiasi cha kumgeuza binadamu mwingine kuwa kama bidhaa inayoweza kuuzwa na kununuliwa sokoni. Haya ni matokeo kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine. Angalisho limetolewa kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa macho zaidi kutokana na wimbi kubwa la wizi wa watoto wadogo, ambao wakati mwingine wanapotea katika hali na mazingira ya kutatanisha. Kuna mtindo ambao unaendelea kujipanua kwa baadhi ya wanawake kukodisha matumbo yao kwa malipo, ili kuwazalia wanawake wenzao watoto, kwa lugha ya kitaalam mwanamke wa namna hii anaitwa “surrogate mother”. Askofu mkuu Ivan Jurkovič anasema, huu ni uhalifu unaofanywa na magenge ya kitaifa na kimataifa, kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushikamana ili kuweza kung’oa mizizi ya uhalifu huu sehemu mbali mbali za dunia.

Hapa kuna haja ya kujenga dhamiri nyofu na utashi mwema, kwa kutekeleza kwa vitendo  maamuzi yanayotolewa na Jumuiya ya Kimataifa. Kanisa pamoja na Taasisi zake, limeendelea kuwa mstari wa mbele kukabiliana na kashfa hii yenye matatizo na changamoto pevu kwa ujasiri mkubwa, kiasi kwamba, zimegeuka kuwa ni nguzo za matumaini kwa waathirika wa vitendo hivi viovu ndani ya jamii. Ni taasisi ambazo zimejielekeza zaidi, kuzuia, kuokoa na kuwasaidia waathirika kuanza kuandika tena kurasa mpya za maisha yao, kwa kuwawezesha kiuchumi pamoja na kuwapatia ushauri nasaha. Sheria haina budi kushika mkondo wake, ili wale wote wanaojihusisha na vitendo hivi viovu waweze kufikishwa mbele ya sheria ili kujibu tuhuma zinazowakabili. Kuna haja pia ya kukomesha tabia ya kudhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Utumwa Mamboleo
17 July 2020, 13:57