Tafuta

Vatican News
Familia ni kitovu cha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa kwa ajili ya Utume wa Familia. Familia ni kitovu cha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa kwa ajili ya Utume wa Familia.  (Vatican Media)

Vatican: Familia ni Kitovu cha Sera na Mikakati ya Uinjilishaji! Inalipa!

Mbele ya maisha ya wanandoa wanaoteseka kutokana na madonda ya maisha ya ndoa Kanisa kama ilivyokuwa katika historia yake, halina budi kuonesha moyo wa upendo na mshikamano; kwa kuonja magumu wanayokabiliana nayo, ili hatimaye, kuwawezesha kuzima kiu ya amani, utulivu na furaha ya kweli kama mtu binafsi na kama wanandoa katika ujumla wao. Utume wa Familia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia kuanzia tarehe 6 hadi tarehe 8 Julai 2020 limeadhimisha Mkutano wake wa 110 uliopambwa na kauli mbiu: “Kwa ajili ya Huduma ya Injili, Matumaini ya Colombia”. Kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, mkutano huu umeadhimishwa kwa njia ya mitandao ya kijamii. Mama Gabriella Gambino, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, kwa kuchota katika uzoefu na mang’amuzi yake kama mwanandoa na mama wa familia, amewaonesha Maaskofu wa Colombia vipaumbele na malengo ya utume wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia, kwa kuwakumbusha kwamba, katika kipindi hiki cha kipeo cha janga la Corona, COVID-19, familia imeonesha: umuhimu, amana na utajiri wake katika jamii.

Mbele ya maisha ya wanandoa wanaoteseka kutokana na madonda ya maisha ya ndoa na familia, Kanisa kama ilivyokuwa katika historia yake, halina budi kuonesha moyo wa upendo na mshikamano; kwa kuonja shida na magumu wanayokabiliana nayo, ili hatimaye, kuwawezesha kuzima kiu ya amani, utulivu na furaha ya kweli kama mtu binafsi na kama wanandoa katika ujumla wao. Mipasuko na majeraha ya maisha ya ndoa na familia ni matokeo ya sababu mbali mbali katika maisha. Kwa mfano haya ni masuala: kisaikolojia, kimwili, kimazingira na kitamaduni na wakati mwingine ni matokeo ya binadamu kujifungia katika ubinafsi wake na kushindwa kupokea zawadi ya upendo. Mama Gabriella Gambino anasema, katika shida na changamoto zote hizi, kipaumbele cha kwanza ni kuwasindikiza wanandoa na familia.

Lengo ni kuwasaidia wanandoa na familia kutambua na kuthamini: amana, utajiri na tunu msingi zinazobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ndoa, kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu katika maisha yao. Wanandoa watambue kwamba, wamepewa dhamana na jukumu la malezi na elimu bora kwa watoto wao. Katika mapambano dhidi ya janga la Virusi vya Corona, COVID-19, familia sehemu mbali mbali za dunia, imekuwa ni kimbilio na nguvu iliyowawezesha watu wengi kusimama imara; kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; kwa kusaidiana kwa hali na mali, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja, wanasaidiana na kukamilishana katika hija ya maisha yao hapa duniani. Familia imara na thabiti, zimeendelea kuwa ni kichochea kikubwa cha mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu katika masuala ya uchumi, jamii na elimu.

Ni katika muktadha huu, Mama Gabriella Gambino, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, Kanisa halina budi kusimama kidete kwa kushikamana na familia, ili kuweza kuzisindikiza katika maisha na utume wake. Familia ni kitovu cha tunu msingi za maisha ya Kikristo na elimu ya uraia mwema. Maisha ya ndoa na familia ni kielelezo cha: Ukuu, uzuri, utakatifu na ushuhuda wa Injili ya familia unaobubujika kutoka katika sura na mfano wa Mungu. Ndani ya familia kuna matatizo na changamoto zake, lakini waamini wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Huu ndio ushuhuda wanaopaswa kuoneshwa vijana wa kizazi kipya kwamba, matatizo na changamoto ni sehemu ya maisha ya ndoa na familia, lakini pia familia ni kisima cha furaha ni wito na njia inayomwelekeza mtu furaha ya kweli katika maisha.

Wanandoa watambue kwamba, kimsingi wao kama familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Huu ndio mwelekeo wa pekee uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto inayovaliwa njuga na Baba Mtakatifu Francisko, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii. Wanandoa wanapaswa kuwa ni walimu wa kwanza na viongozi wa tunu msingi za maisha ya Kikristo.

Ni wajibu na dhamana ya Mama Kanisa kuwasaidia wanandoa katika safari ya maisha yao kutambua uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati pamoja nao. Lakini, familia katika ulimwengu mamboleo inakabiliwa na changamoto pevu kama zilivyoainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa. Mama Gabriella Gambino anaendelea kufafanua kwamba, ni kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa, wanandoa wanaweza kuendelea kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa.

Maaskofu wawe mstari wa mbele kuwasaidia na kuwasindikiza wanandoa kukabiliana kwa imani na matumaini: matatizo na changamoto za maisha ya ndoa na familia. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi ya mawasiliano ya jamii, vijana wengi wanajikuta wakijenga mahusiano ya kimtandao yasiyogusa hali halisi ya maisha ya watu. Kuna umati mkubwa wa vijana unaoshindwa kutambua mahusiano na mafungamano ya kweli katika maisha; wanashindwa kuelewa umuhimu wa mwili wa mwanadamu na wanandoa wenyewe kujisadaka bila ya kujiachilia kwa ajili ya ndoa na familia. Hapa kuna umuhimu wa pekee kwa Maaskofu kupitia na kuangalia tena: jinsi ya kuwaandaa wanandoa watarajiwa; mambo msingi yanayopewa kipaumbele katika semina kwa wanandoa na kwamba, kuna haja ya kuendelea kuwapatia vijana wa kizazi kipya katekesi ya kina kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Wazazi na walezi wajengewe uwezo wa kulea familia zao, kwa kupenda na kuhudumia. Utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya hauna budi kwenda sanjari na utume wa familia. Baba Mtakatifu Francisko anasema, maisha ya ndoa na familia ni wito kwa waamini wengi ndani ya Kanisa. Yataka moyo kwa mwamini kuamua kufunga ndoa na kuwa tayari kupata watoto. Huu ni wito na jibu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kuwapatia wanandoa katekesi endelevu. Wanandoa wanapopata watoto, mtindo wa maisha, dhamana na majukumu yao yanabadilika sana. Familia pia zinapaswa kuwaangalia, kuwatunza na kuwathamini wazee pamoja na watu wenye udhaifu ndani ya familia. Hawa ni sehemu muhimu sana ya familia ya watu wa Mungu, wasaidiwe kutambua na kuthamini mchango wao katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao.

Waamini watambue kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wanashiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo, hivyo wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Wazee wahakikishe kwamba wanashirikisha vyema karama na mapaji yao kwa vijana wa kizazi kipya. Wazee waendelee kuimarisha tasaufi ya maisha ya kiroho bila kuwatenga. Maaskofu wanayo dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, kwa kusimama kidete kutekeleza vyema utume wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia kwa kuonesha na kushuhudia kwamba, kwa hakika familia ni wito na njia inayoelekea kwenye utakatifu wa maisha!

Utume wa Familia: Colombia

 

14 July 2020, 08:29