Tafuta

Mwongozo wa Mchakato wa Kesi za Unyanyasaji wa Kijinsia Dhidi ya Watoto Wadogo Ndani ya Kanisa ni "Vademecum" inayopania kutafuta ukweli ili haki iweze kutendeka! Mwongozo wa Mchakato wa Kesi za Unyanyasaji wa Kijinsia Dhidi ya Watoto Wadogo Ndani ya Kanisa ni "Vademecum" inayopania kutafuta ukweli ili haki iweze kutendeka! 

Mwongozo wa Mchakato wa Kesi za Nyanyaso za Kijinsia: Ukweli

Mama Kanisa anapenda kujielekeza zaidi katika njia ya ukweli na haki kama jibu makini katika kukabiliana na kashfa hizi ambazo zimechafua maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Toba, wongofu wa kichungaji; mang’amuzi, malezi na majiundo makini ni kati ya mambo msingi yanayoweza kuganga na kutibu kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, tarehe 17 Julai 2020, limechapisha Mwongozo wa Mchakato wa Kesi za Unyanyasaji wa Kijinsia Dhidi ya Watoto Wadogo Ndani ya Kanisa, “Vademecum” ili ukweli uweze kufahamika na haki kutendeka. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuendeleza Utume wake wa kutaka kudhibiti uhalifu unaoweza kutendwa na waamini; pamoja na kumrekebisha mhalifu; kutenda haki kwa waliokosewa; na kuondoa kashfa. Askofu mkuu Giacomo Morandi, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa katika mahojiano maalum na Vatican News anafafanua kuhusu: Lengo kuu la Mwongozo wa Mchakato wa Kesi za Unyanyasaji wa Kijinsia Dhidi ya Watoto Wadogo Ndani ya Kanisa, “Vademecum”, dhamana na wajibu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa; Kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa; pamoja na wajibu wa Maaskofu mahalia na Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume.

Askofu mkuu Giacomo Morandi, anasema ukweli unapaswa kufahamika na haki kutendeka. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuendeleza utume wake wa kutaka kudhibiti uhalifu unaoweza kutendwa na waamini; pamoja na kumrekebisha mhalifu; kutenda haki kwa waliokosewa; na kuondoa kashfa hii ambayo inachafua maisha na utume wa Kanisa. Kashfa hii haitaweza kuponyeka, ikiwa kama hakuna toba, wongofu wa kichungaji, sera na mikakati makini ya majiundo kwa majandokasisi na wakleri. Mkutano wa Viongozi wa Kanisa uliofanyika kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019, ulipembua dhamana ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa kuwaundia mazingira bora zaidi ya malezi na makuzi yao, changamoto iliyotolewa Baraza la Makardinali Washauri. Mwongozo huu ni matunda ya uzoefu na ukomavu uliojitokeza katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, pamoja na ushirikiano wa dhati ulioneshwa na wataalamu mbali mbali kutoka katika Sekretarieti kuu ya Vatican.

Huu ni mwongozo unaotolewa kwa ajili ya Maaskofu, Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume pamoja na wadau mbali mbali wanaojihusisha na utekelezaji wa sheria na haki jamii. Mwongozo unatoa dira na mwelekeo unaowawezesha wahusika kufuata mambo msingi ili hatimaye, ukweli uweze kufahamika na haki kutendeka. Mwongozo wa Mchakato wa Kesi za Unyanyasaji wa Kijinsia Dhidi ya Watoto Wadogo Ndani ya Kanisa unawaelekeza wahusika tangu wakati tuhuma zinapotolewa hadi hukumu ya kesi hii kutolewa, kwa kuzingatia: sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Mwongozo huu utaendelea kuboreshwa kwa kuzingatia maoni kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, Taasisi za Elimu ya Juu na Vyuo Vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa. Mwongozo huu ni kwa ajili ya huduma ya ukweli na haki katika maisha na utume wa Kanisa.

Kimsingi, Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa limepewa dhamana ya kushughulikia: Kesi za Imani, Sakramenti za Kanisa, Kanuni maadili na utu wema. Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, mnamo mwaka 2001 kwa Barua binafsi “Motu proprio”, yaani “Sacramentorum sanctitatis tutela”, yaani “Ulindaji wa Utakatifu wa Sakramenti”, alitoa taratibu za mchakato wa kuendesha kesi hizo katika Mahakama za Kanisa. Kati ya makosa ya uhalifu, yapo yale ambayo yanatambuliwa kuwa ni makosa makubwa ya uhalifu, yanayojulikana kwa lugha ya kisheria “Delicta graviora”. Sehemu kubwa ya makosa haya ni yale yanayokwenda kinyume cha Amri ya Sita ya Mungu. Watoto wadogo wanaozungumziwa ni wale ambao bado hawajatimiza umri wa miaka 18 na kwamba, nia ni kutaka kufanya nao mahusiano ya kijinsia au kuchezea miili yao kinyume cha maadili na utu wema. Kanisa litaendelea kushughulikia hata zile shutuma za watu wasiojulikana, ili ukweli uweze kufahamika na haki kutendeka na mchakato wa kesi za namna hii unaendeshwa kwa kuzingatia kile kinachoitwa kwa lugha ya sheria: “fumus delicti”.

Askofu mkuu Giacomo Morandi anaendelea kufafanua kwamba, mbele ya sheria, kanuni na taratibu, Kanisa linawaona watu! Hawa wanaweza kuwa: watuhumu, watuhumiwa, waathirika na pale inapowezekana mashuhuda wa vitendo hivi ambavyo ni kinyume cha maadili na utu wema. Kanisa linaonja na kutambua mateso, utu, heshima na haki msingi za watu hawa, ndiyo maana linapania kuhakikisha kwamba, ukweli unafahamika na haki inatendeka. Ndiyo maana Mwongozo wa Mchakato wa Kesi za Unyanyasaji wa Kijinsia Dhidi ya Watoto Wadogo Ndani ya Kanisa “Vademecum” ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia” ni mbinu mkakati wa kichungaji kwa ajili ya kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.

Barua hii inawataka Maaskofu na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kuwajibika barabara katika kushughulikia tuhuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa kwa kutoa taarifa kwa viongozi wanaohusika. Wana wajibu wa kuwalinda watu wote wanaohusika katika sakata hili. Pale ambapo ukweli uko bayana, kesi inaweza kuendeshwa nje ya Mahakama na mtuhumiwa kupata adhabu anayostahili. Lakini, Kanisa linapenda kuhakikisha kwamba, mtuhumiwa anapata nafasi ya kujitetea, ili ukweli uweze kufahamika na haki kutendeka. Kesi za nyanyaso za kijinsia zina utata wake kwa sababu mara nyingi hazina mashuhuda. Lakini, Askofu mkuu Giacomo Morandi anasema, mwendelezo wa matukio, ukubwa wa tendo lililofanywa, uwepo wa nyaraka mbali mbali pamoja na dhamiri nyofu, inawezekana mtuhumiwa kukiri makosa yake mbele ya Mahakama. Katika muktadha kama huu, kuna uwezekano kabisa wa watu kuchafuliwa utu, heshima na sifa zao njema.

Katika mazingira kama haya mtuhumiwa anaweza kutumia kanuni ya “in dubio pro reo” kwa kukiri kwamba, hana hatia! Kwa Mapadre wanaoshutumiwa kujihusisha na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, kwa kuongozwa na dhamiri nyofu, wanaweza kuomba kwa Baba Mtakatifu, ili kuondolewa mamlaka na haki ya kuishi na kuhudumu kama Mapadre, lakini, ikumbukwe kwamba, ile chapa ya Daraja Takatifu ni yakudumu na haiwezi kufutika. Kashfa za nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni udhaifu ambao utaendelea kuliandama Kanisa, lakini kwa miaka ya hivi karibuni, shutuma zimeanza kupungua. Mama Kanisa anapenda kujielekeza zaidi katika njia ya ukweli na haki kama jibu makini katika kukabiliana na kashfa hizi ambazo zimechafua maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Toba, wongofu wa kichungaji; mang’amuzi, malezi na majiundo makini ni kati ya mambo msingi yanayoweza kuganga na kutibu kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa!

Vademecum

 

17 July 2020, 13:35