Tafuta

Vatican News
Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot anasema, majadiliano ya kidini na kiekumene ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot anasema, majadiliano ya kidini na kiekumene ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa.  (Vatican Media)

Majadiliano ya Kidini na Kiekumene ni Muhimu kwa Utume wa Kanisa

Kardinali Miguel Ángel Ayuso Guixot, hivi karibuni alifanya ziara ya kitume nchini Bulgaria, ambayo inaendelea kujipambanua kuwa ni maabara ya mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene. Kama ilivyokuwa kwa Watakatifu Petro na Paulo, ndivyo ilivyo pia kwa Watakatifu Cyril na Metodi: hawa ni Walimu wa imani na Mitume wanaowaalika waamini kujenga umoja wa kiimani kati yao,

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume na miamba wa imani, Baba Mtakatifu Francisko amesema, safari ya maisha ya Mtakatifu Petro inaweza kuwa ni dira kwa maisha ya waamini, kiasi hata cha kusadaka maisha yao kwa ajili ya Mungu aliye hai! Hija ya maisha ya Mtakatifu Petro hapa ulimwenguni ni mwanga angavu unaoweza kuwaangazia hata waamini katika maisha yao. Mtakatifu Petro alibahatika kupata upendeleo na neema ya pekee kutoka kwa Kristo Yesu, akamwokoa kutoka katika taabu mbali mbali na ndivyo Mwenyezi Mungu anavyofanya kwa kila mwamini. Inasikitisha kuona kwamba, waamini wanamkimbilia Mwenyezi Mungu wanapokuwa katika shida na mahangaiko makubwa. Lakini, Mwenyezi Mungu anaona mbali zaidi, na anawataka waja wake kupiga hatua kubwa zaidi, si tu kwa kutafuta zawadi, neema na baraka zake, bali kumtafuta Mwenyezi Mungu aliye hai.

Waamini wawe na ujasiri wa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, huku wakimtolea shida na matatizo yao mbali mbali ya maisha, ili hatimaye, aweze kuwapatia neema kubwa zaidi ya kuweza kusadaka maisha yao, kwa kuyageuza kuwa ni zawadi kwa ajili ya wengine. Mwenyezi Mungu anawataka waja wake, kukua na kukomaa katika sadaka ya maisha na kwa njia hii, wataweza kukomaa na kuwa watu wazima zaidi. Mtakatifu Petro hakubahatika kuwa shujaa wa imani kwa sababu aliokolewa kutoka gerezani, lakini kwa sababu aliweza kusadaka maisha yake kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Kardinali Miguel Ángel Ayuso Guixot, M.C.C.I, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, hivi karibuni alifanya ziara ya kitume nchini Bulgaria, ambayo kwa sasa inaendelea kujipambanua kuwa ni maabara ya mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene.

Kama ilivyokuwa kwa Watakatifu Petro na Paulo, Mitume, ndivyo ilivyo pia kwa Watakatifu Cyril na Metodi: hawa ni Walimu wa imani na Mitume wanaowaalika waamini kujenga umoja wa kiimani kati yao, wakiendelea kutafakari ushujaa wao wa kiimani na ushuhuda wa maisha yao kwa Kristo Yesu, kwa kutoa changamoto ya kulinda na kudumisha tunu bora za maisha walizorithisha kwa njia ya maneno na matendo yao, katika harakati za kuleta maendeleo fungamani ya binadamu, haki na amani kwa watu wote wenye mapenzi mema. Watakatifu Cyril na Metodi, walikita maisha na utume wao, katika mchakato wa ujenzi wa umoja, udugu wa kibinadamu na mshikamano. Wakazama zaidi katika uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Bado kuna ukakasi na migawanyiko miongoni mwa Wakristo, kumbe ni wajibu wa waamini kuhakikisha kwamba wanavuka vikwazo vyote hivi ili waweze kuwa wamoja, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya Kitume nchini Bulgaria kuanzia tarehe 5-7 Mei 2019 aliwasihi watu wa Mungu nchini Bulgaria kujikita tena katika ujenzi wa umoja hata katika tofauti zao msingi, kama sehemu ya kutajirishana na kukamilishana katika hija ya maisha ya hapa duniani! Majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa Katoliki ili kujenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano kati ya watu wa mataifa na wala si kwa bahati mbaya kwamba, Kanisa katika mikakati na vipaumbele vyake katika mchakato wa uinjilishaji linaendelea kukazia majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani.

Kardinali Miguel Ángel Ayuso Guixot katika hija yake ya kitume nchini Bulgaria, amepata nafasi ya kukutana, kusali na kuzungumza na viongozi wa Kanisa, watawa na waamini walei kwa kukazia umuhimu wa wokovu kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wajibu binafsi katika kukubali mwaliko wa wokovu pamoja na kujibidiisha kukutana na Kristo Yesu katika: Neno, Sakramenti na historia ya watu wanaokutana nao katika maisha na utume wao, kila kukicha! Imekuwa pia ni fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa la Kiorthodox pamoja na viongozi wa Serikali nchini Bulgaria. Kardinali Miguel Ángel Ayuso Guixot amepata fursa pia ya kukutana na Mustafa Hadzi, Mufti mkuu wa waamini wa dini ya Kiislam nchini Bulgaria pamoja na viongozi wa dini ya Wayahudi. Kwa viongozi wote hawa, mkazo umekuwa ni kuendeleza majadiliano ya kidini, ili kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu!

Bulgaria

 

04 July 2020, 14:19