Tafuta

Vatican News
Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka Mkuu wa Kipapa, hivi karibuni amefanya hija ya upendo na mshikamano na wananchi wa Ukraine. Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka Mkuu wa Kipapa, hivi karibuni amefanya hija ya upendo na mshikamano na wananchi wa Ukraine.   (AFP or licensors)

Mshikamano wa Huruma na Mapendo na Wananchi wa Ukraine

Kardinali Konrad Krajewski akiwa nchini Ukraine, ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Monasteri ya Masista wa Shirika la Albertin, ujenzi wa nyumba ya wanawake wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Ametabaruku Kanisa la Mtakatifu Yohane Paulo II, kama kumbukumbu endelevu ya miaka 100 tangu alipozaliwa. Amesali na kuzungumza na viongozi wa Ukraine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka Mkuu wa Kipapa, hivi karibuni amefanya hija ya kichungaji nchini Ukraine, kuanzia tarehe 18 – 19 Julai 2020 kwa mwaliko wa Askofu mkuu Mieczyslav Mokshitsky wa Jimbo kuu la Leopoli, kama kielelezo makini cha uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu Francisko kwa familia ya Mungu nchini Ukraine. Akiwa nchini Ukraine, ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Monasteri ya Masista wa Shirika la Albertin, ujenzi wa nyumba ya wanawake wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; pamoja na wanawake wanaoishi peke wakiwa na dhamana ya kuwatunza watoto wao. Kardinali Konrad Krajewski ametabaruku Kanisa la Mtakatifu Yohane Paulo II, kama kumbukumbu endelevu ya miaka 100 tangu alipozaliwa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Yohane Paulo II amekuwa ni zawadi ya pekee kabisa kwa Kanisa na Poland katika ujumla wake.

Mtakatifu Yohane Paulo II, alianza hija yake ya maisha ya hapa duniani tarehe 18 Mei 1920 huko Wavowice, akaendeleza sehemu ya maisha yake mjini Roma kwa muda wa miaka 15. Tangu awali ni kiongozi aliyejipambanua kuwa ni mtetezi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; aliguswa kwa namna ya pekee na Fumbo la Mungu, Kazi ya Uumbaji na Utakatifu wa maisha ya mwanadamu. Ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu. Adhimisho la Jumapili ya huruma ya Mungu, linapata chimbuko lake wakati wa adhimisho la Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo. Huruma ya Mungu inakita mizizi yake katika Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo! Mtakatifu Maria Faustina Kowalska ni kati ya watu waliotangaza, wakashuhudia na hatimaye, kueneza Ibada ya huruma ya Mungu kwa watu wa Mataifa. Mtakatifu Yohane Paulo II kwa mwanga wa upendo wa Mungu wenye huruma, alipata mang’amuzi ya pekee kuhusu uzuri na utakatifu wa wito wa watu wa Mungu; akatambua umuhimu wa watoto katika jamii, vijana sanjari na watu wazima. Aliangalia muktadha wa hali za kitamaduni na kijamii.

Askofu mkuu Mieczyslav Mokshitsky wa Jimbo kuu la Leopoli, Ukraine anasema, Kanisa nchini Ukraine linaadhimisha Mwaka wa Miito Mitakatifu. Uwepo wa Kardinali Konrad Krajewski, kati yao ni alama muhimu sana ya uwepo endelevu wa Baba Mtakatifu Francisko katika maisha ya watu wa Mungu nchini Ukraine. Hawa ni watu ambao wamejaribiwa na kupepetwa kutokana na vita, hali ambayo pia imegumishwa kwa uwepo wa janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Madhabahu ya Berdychiv ni mahali ambapo panakuza na kudumisha ari na moyo wa Sala ya Kanisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kama sehemu ya kazi ya ukombozi. Ni mahali pa shuhuda za imani, matumaini na mapendo, kielelezo cha Kanisa linalokesha na kusali daima! Madhabahu ya Berdychiv ni mahali pa ukimya unaobubujika kutoka katika undani wa mahujaji, tayari kuomba: neema na rehema pamoja na kudumisha upendo kwa Mungu na jirani!

Hapa ni mahali pa kuonja huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu. Kwa njia ya sala na sadaka ya Misa Takatifu, waamini wanatambua na kukiri uwepo endelevu wa Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Kanisa Katoliki nchini Ukraine linaendelea kutoa huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi kama kielelezo cha upendo wa Kanisa kwa watu wa Mungu nchini humo!

Kardinali Konrad

 

24 July 2020, 07:57