Tafuta

Vatican News
Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha limeanzisha Kampeni ya upendo na mshikamano kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee, kama sehemu ya utekelezaji wa ndoto ya Papa Francisko. Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha limeanzisha Kampeni ya upendo na mshikamano kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee, kama sehemu ya utekelezaji wa ndoto ya Papa Francisko. 

Kampeni ya Mshikamano wa Upendo Kati ya Vijana na Wazee!

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, tarehe 27 Julai 2020 limezindua kampeni inayopambwa na kauli mbiu: “Vijana, Wazee ni Babu na Bibi zenu”: Tumieni kipaji chenu cha ugunduzi wa upendo ili kuwasiliana nao kwa njia ya simu, video pamoja na kuwasikiliza. Lengo ni kusaidia mchakato wa kupunguza upweke unaowasonga wazee hasa kutokana na janga la ugonjwa wa COVID-19

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sikukuu ya Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Julai, ametoa wito na mwaliko kwa vijana kuhakikisha kwamba, wanatenda tendo jema la huruma na mapendo kwa wazee wanaowazunguka. Upendeleo wa pekee utolewe kwa wazee wanaoishi peke yao au kwenye nyumba za kutunzia wazee, ambao kwa muda mrefu uliopita hawajapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na ndugu, jamaa na marafiki zao. Vijana watambue na kuthamini nafasi na dhamana ya wazee katika jamii na kamwe wasiwaache kuelemewa na upweke. Katika maadhimisho ya Sikukuu ya Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria, Baba Mtakatifu Francisko amewataka vijana kutumia uzoefu na mang’amuzi yao ili kuwaonjesha upendo kwa njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii.

Baba Mtakatifu ameyasema hayo mara baada ya tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 26 Julai 2020. Vijana watenge muda wa kuweza kuwasikiliza kwa dhati na pale ambapo inawezekana kwa kuzingatia itifaki ya mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 wawatembelee ili kuwajulia hali. Baba Mtakatifu Francisco anasema, Bwana Luis Bernárdez, Mshairi maarufu kutoka Argentina aliwahi kusema, mti ambao mizizi yake imeng’olewa, hautaweza kukua, kuchanua na hata kutoa matunda. Baba Mtakatifu amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwapongeza wazee kwa uwepo na ushiriki wao katika maisha na utume wa jamii.

Ni katika muktadha huu, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, tarehe 27 Julai 2020 limezindua kampeni inayopambwa na kauli mbiu: “Vijana, Wazee ni Babu na Bibi zenu”: Tumieni kipaji chenu cha ugunduzi wa upendo ili kuwasiliana nao kwa njia ya simu, video pamoja na kuwasikiliza. Lengo ni kusaidia mchakato wa kupunguza upweke unaowasonga wazee hasa kutokana na janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Vijana wanaweza kutekeleza wito huu wa Baba Mtakatifu kwa kuzingatia na kuheshimu itifaki dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Hata kabla ya mlipuko wa Virusi vya Corona, COVID-19, mahusiano na mafungamano kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee yalikuwa yanalega lega sana sehemu mbali mbali za dunia.

Katika siku za hivi karibuni, Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, Vyama na Mashirika ya Kitume pamoja na watu mbali mbali wenye mapenzi mema, wamekuwa wakiendesha kampeni maalum ili kuwahamasisha vijana wa kizazi kipya kuwa karibu zaidi na wazee, ambao kimsingi ni amana na utajiri wa jamii husika. Vijana wengi wameitikia sana mwaliko huu na kwa hakika wametumia vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii kuwaweza kuwafikia wazee wengi zaidi. Upweke hasi ni hatari sana katika maisha ya mwanadamu kwani unaweza kumtumbukiza mtu katika ugonjwa wa sonona au msongo wa mawazo kama unavyofahamika na wengi. Sonona ni ugonjwa wa kawaida wa akili unaohusisha hali endelevu ya huzuni au kukosa shauku au raha inayoambatana na dalili zifuatazo: hali ya kukosa usingizi na hata hamu ya chakula, hisia za mtu kujiona kuwa hafai, uchovu wa kupindukia, umakini hafifu na ugumu katika kufanya maamuzi.

Dalili nyingine ni ukosefu wa utulivu wa mwili, mtu kuongea sana pamoja na kukosa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Sababu zinazoweza kuchangia sonona ni kama hizi zifuatazo: Nyanyaso za kijinsia na utumiaji haramu wa dawa za kulevya. Migogoro ya kifamilia, kijamii na kimahusiano husababisha kwa baadhi ya watu kutumbukia katika ugonjwa wa sonona, ambapo mtu hujiona hana thamani tena baada ya kutengwa na jamii kwa muda mrefu. Kifo au hasara za kikazi, wakati mwingine mtu hujikuta amepata tatizo hili baada ya kupoteza mtu muhimu kwake na jamii kwa ujumla au endapo mtu akapata hasara kubwa kiasi cha kufilisika mali yake, basi mtu huyu hunyong'onyea na kudhohofika afya yake taratibu, asijue wapi pa kuanzia na hatima yake huona jamii yote kwake kuwa ni mbaya na imemtenga kiasi cha kujiona si mali kitu!

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha linawahamasisha vijana kuwatembelea wazee katika Jumuiya zao ndogo ndogo za Kikristo na katika maeneo ya Parokia zao, ili kuwapelekea upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kampeni hii inalenga kufanikisha ndoto ya Baba Mtakatifu Francisko anayetaka kuona ulimwengu ambao unawafumbata na kuwaambata vijana na wazee. #sendyourhug.

Baraza la Kipapa: Mshikamano Vijana na Wazee
28 July 2020, 13:24