Tafuta

Vatican News
Kardinali Pietro Parolin, tarehe 25 Julai 2020 amemwekwa wakfu Askofu mkuu Muñoz Cardaba, Balozi wa Vatican nchini Sudan na Eritrea. Kardinali Pietro Parolin, tarehe 25 Julai 2020 amemwekwa wakfu Askofu mkuu Muñoz Cardaba, Balozi wa Vatican nchini Sudan na Eritrea. 

Askofu Mkuu Luis Càrdaba: Haki, Amani, Matumaini na Mapendo

Kama Balozi wa Vatican nchini Eritrea na Sudan awe ni chombo na mjenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano. Aendelee kudumisha uhuru wa kidini, utunzaji bora wa mazingira, sera na mikakati ya uchumi fungamani ya binadamu. Lengo kuu ni kutengeneza mazingira ya uchumi shirikishi, unaowakumbatia na kuwaambata wote pasi ya mtu yeyote kubakia nyuma hata kidogo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi, tarehe 25 Julai 2020, Sherehe ya Mtakatifu Yakobo, Mtume, amemweka wakfu Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba, Balozi mpya wa Vatican nchini Sudan na Eritrea. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Toledo, Jimbo kuu la Vallelado, Hispania. Katika Ibada hii ya Misa takatifu ameshiriki pia Askofu mkuu Francisco Cerro Chaves pamoja na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican. Dhamana na wajibu wa Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba kwa sasa ni kusaidia mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu ndani ya Kanisa na kati ya Mataifa. Watu wana kiu ya kutaka kusikiliza ujumbe wa matumaini na hekima inayobubujika kutoka katika Habari Njema ya Wokovu.

Kardinali Parolin, amemkumbusha Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba kwamba, kama Balozi wa Vatican, ni mwakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, anayemtuma kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo. Katika maisha na utume wake, ajitahidi kuwa ni chombo na mjenzi wa umoja wa Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wake. Atakuwa na wajibu wa kuhakikisha kwamba, anawasaidia watu wa Mungu kwa kuwafundisha ili waweze kuyafahamu Mafundisho ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na kuyaweka kuwa ni sehemu ya vipaumbele vya maisha yao, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Asimame imara kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, tangu mtoto anapotungwa tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba atambue kwamba, Mama Kanisa anaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali za maisha. Kama Balozi wa Vatican nchini Sudan na Eritrea, awe ni chombo na mjenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu katika maeneo haya sanjari na kuendelea kudumisha uhuru wa kidini. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, sera na mikakati ya uchumi fungamani wa binadamu ni kati ya mambo ambayo atapaswa kuyaunga mkono, ili kutengeneza mazingira ya uchumi shirikishi, unaowakumbatia na kuwaambata wote pasi ya mtu yeyote kubakia nyuma!

Ni wajibu wa Mabalozi wa Vatican, kutoa taarifa ya mambo muhimu yanayoendelea kujiri katika nchi wanazotekeleza dhamana na utume wao, ili Vatican iweze kushiriki kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Jambo la msingi ni kuonesha vipaumbele vinavyopaswa kuvaliwa njuga! Kwa njia ya wawakilishi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia, Vatican inaweza pia kushiriki kikamilifu katika maisha ya watu hawa, katika shida, changamoto na matumaini yao kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Kama mwakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, atapaswa kuwa pia ni chombo cha majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, kwa kujikita katika ujasiri, utayari, ukweli na uwazi pamoja na kutoa nafasi kwa Injili ya matumaini ili iweze kukita mizizi yake katika maisha ya watu wa Mungu. Aoneshe na kushuhudia imani, matumaini na mapendo kwa watu wa Mungu, ili kwa njia ya maisha na utume wake, watu waweze kuona ufunuo wa Uso wa huruma ya Mungu.

Udhaifu na mapungufu yake ya kibinadamu umkumbushe kwamba, wito wake ambao ni kito cha thamani kubwa, umehifadhiwa katika chombo cha udongo. Anapaswa kuwahudumia watu wa Mungu kwa kufuata na kuiga mfano wa Kristo Mchungaji mwema. Uongozi ndani ya Kanisa ni huduma kwa ajili ya watu wa Mungu. Kwa njia ya karama na mapaji ya Roho Mtakatifu Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba sasa amepata utimilifu wa Daraja Takatifu ya Upadre, kwa kuwekwa wakfu kuwa Askofu mkuu, kielelezo cha huduma kwa watu wa Mungu. Anatumiwa kuhudumia na wala si kutawala. Kumbe, wajibu wake mkuu ni: kupenda na kuhudumia; ushuhuda na sala, nguzo msingi kwa ajili ya utume wa Askofu. Aoneshe ukaribu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa watu wa Mungu nchini Sudan na Eritrea. Lengo kuu ni kukuza na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi.

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba alizaliwa tarehe 25 Agosti 1965 huko Vallelado, nchini Hispania. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 28 Juni 1992 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Alijiendeleza na hatimaye, kubahatika kupata Shahada ya Uzamili katika masomo ya taalimungu, Sheria za Kanisa pamoja na Sheria na Taratibu za Uendeshaji wa Kesi Mahakamani, “Giurisprudenza”. Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba alianza kutoa huduma za Kidiplomasia mjini Vatican hapo tarehe 1 Aprili 2001. Tangu wakati huo ametumwa kwenye Balozi za Vatican nchini Ugiriki, Mexico, Ubelgiji, Italia, Australia, Ufaransa na Uturuki.

Kardinali Parolin: Wakfu
27 July 2020, 09:18