Tafuta

Vatican News
Bi Bernice King: Kuna umuhimu wa kuheshimu utawala wa sheria unaozingatia: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Bi Bernice King: Kuna umuhimu wa kuheshimu utawala wa sheria unaozingatia: utu, heshima na haki msingi za binadamu.  (AFP or licensors)

Utawala wa Sheria Unaozingatia: Utu, Heshima na Haki Msingi

Kuna ubaguzi mkubwa kwenye masuala ya ajira, elimu na hali ya maisha ya watu. Janga kubwa la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limekuwa na madhara makubwa kwa raia wa Marekani wenye asili ya Kiafrika. Wananchi wa Marekani wanapaswa kushikamana na kuelezea matashi yao mbele ya viongozi wa Serikali, ili yaweze kutekelezwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Bwana George Floyd aliuwawa kikatili tarehe 25 Mei 2020 huko Minneapolis katika jimbo la Minnesota nchini Marekani na kuzikwa tarehe, 9 Juni 2020, huko Houston, mahali alipokulia. Kifo cha George Flyod ni tukio ambalo limeamsha hisia kubwa ndani na nje ya Marekani kuhusu: umuhimu wa kusimama kidete, kulinda, kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni changamoto ya kuondokana na mifumo mbali mbali ya ubaguzi, nyanyaso, ukandamizaji na matumaini makubwa ya nguvu yanayofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama na kwa namna ya pekee na Jeshi la Polisi nchini Marekani. Sehemu mbali mbali za dunia, kulifanyika maandamanio ya amani kulaani ubaguzi wa rangi na matumizi makubwa ya nguvu dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Kiafrika, huku wakiongozwa na kauli mbiu “Black Lives Matter”. Tarehe 19 Juni 2020 Marekani imeadhimisha Kumbukumbu ya kufutwa kwa biashara ya utumwa ulimwenguni, kunako tarehe 19 Juni 1865. Tangu wakati huo, Wamarekani wenye asili ya Kiafrika wanaihesabu kuwa ni Siku ya Uhuru wao. Mwaka huu, tukio hili limeadhimishwa, huku kukiwa na shinikizo la kuitaka Marekani kufanya marekebisho makubwa kwenye Jeshi la Polisi linaloonekana kutumia nguvu kubwa dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Kiafrika.

Bi Bernice Albertine King, Binti ya Martin Luther King, Jr. katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano na Vatican News anasema, nchini Marekani kuna kilio kikubwa cha utawala wa sheria unaozingatia utu, heshima na haki msingi binadamu. Huu ni wakati wa kujizatiti zaidi katika masuala ya haki jamii na usawa kwa watu wote pamoja na kuhakikisha kwamba, huduma za kijamii zinatolewa kwa kuzingatia misingi ya utu wa binadamu. Maandamano makubwa yaliyofanywa na wananchi wa Marekani kupinga vitendo vya ubaguzi wa rangi na matumizi makubwa ya nguvu dhidi ya raia ni jambo ambalo linaweza kusaidia kukoleza mchakato wa uragibishaji wa haki msingi za binadamu ndani na nje ya Marekani. Kuna ubaguzi mkubwa kwenye masuala ya ajira, elimu na hali ya maisha ya watu. Janga kubwa la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limekuwa na madhara makubwa kwa raia wa Marekani wenye asili ya Kiafrika. Wananchi wa Marekani wanapaswa kushikamana na kuelezea matashi yao mbele ya viongozi wa Serikali, ili yaweze kutekelezwa kwa dhati. Huu ni wajibu wa Kikatiba unaopaswa kutekelezwa na viongozi wa Serikali ya Marekani.

Imegota miaka 57 tangu Martin Luther King, Jr alipotoa hotuba kuhusu ndoto yake “I Have a Dream”. Hii ni falsafa inayokita mizizi yake katika majadiliano, ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Lengo ni kuondokana na ghasia, mifumo mbali mbali ya ubaguzi na ukosefu wa haki msingi za binadamu, ili kujenga na kuimarisha maskani ya wote. Huu ni wakati kwa wananchi wa Marekani kubua mbinu mkakati wa kuleta mageuzi katika jamii bila ya kutumia ghasia na vurugu. Watu wenye ushawishi mkubwa katika masuala ya kisiasa, vyombo vya mawasiliano ya jamii, sanaa za maonesho, vyombo vya ulinzi na usalama, sekta ya afya na elimu, wahakikishe kwamba, wanasaidia mchakato wa kuondokana na mifumo mbali mbali ya kibaguzi, ili usawa na haki viweze kutawala na kushamiri nchini Marekani. Wajibu huu unapaswa pia kutekelezwa na viongozi mbali mbali wa kidini, kwa kujenga na kudumisha haki na usawa miongoni mwa waamini wao pamoja na kuhakikisha kwamba, wanajizatiti katika kupambana na mifumo mbali mbali ya ubaguzi. Kuna haja kwa familia ya Mungu nchini Marekani kuendelea kujisadaka bila ya kujibakiza ili kupambana na dhambi ya ubaguzi, umaskini na matumizi ya nguvu!

Baba Mtakatifu Framcisko anasema, ubaguzi wa aina yoyote ile ni jambo ambalo kamwe haliwezi kuvumiliwa wala kufumbiwa macho kwa kisingizio cha kulinda utakatifu wa maisha. Lakini, pia, watu wanapaswa kutambua kwamba, ghasia na vurugu za hivi karibuni, zimepelekea watu wengi kujeruhiwa pamoja na uharibifu mkubwa wa mali. Mambo mengi yanapotea kutokana na vita pamoja na ghasia. Baba Mtakatifu alipenda kuungana na Kanisa la Mtakatifu Paulo na familia ya Mungu mjini Minneapolis pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini Marekani kwa ajili ya kumkumbuka na kuiombea roho ya Marehemu George Floyd pamoja na wale wote waliopoteza maisha kutokana na dhambi ya ubaguzi, ili waweze kupata faraja na maisha ya uzima wa milele. Ameliombea taifa la Marekani liweze kujikita katika upatanisho wa kitaifa, ili hatimaye, amani iweze kutawala tena katika akili na nyoyo za watu. Bi Bernice Albertine King, Binti ya Martin Luther King, Jr. anasema, vurugu, ghasia na vita ni mambo yanayosababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Kumbe, kuna kila sababu ya kuondokana matukio ambayo yanaweza kuweka “Rehani” misingi ya haki, amani na maridhiano.

Bi Bernice Albertine King anaendelea kufafanua kwamba, amani bila vurugu wala ghasia ni jambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo, ili kupyaisha mwelekeo wa kisiasa, kanuni maadili na utu wema. Ni muda muafaka wa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa Jamii ya watu inayowajibika katika kukoleza misingi ya haki na usawa; utu na udugu wa kibinadamu pamoja na heshima kwa kuzingatia amani na utulivu, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki katika mchakato wa mageuzi yanayofumbatwa katika huruma na upendo, ili kujenga na kuimarisha udugu wa kibinadamu. Kauli mbiu kwamba “Black Lives Matter” yaani “Maisha ya Watu Weusi ni ya maana” ni kilio cha watu wanaotaka kupambana na mifumo mbali mbali ya ubaguzi, ili kujenga Jumuiya inayojali utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Hii ni Jumuiya ambayo inasimikwa katika umoja na utofauti; kuna shida, matatizo na changamoto za maisha ambazo zinajadiliwa na kupewa ufumbuzi wa kudumu kwa njia ya amani. Hii ni Jumuiya ambayo: huruma, upendo na msamaha vinatawala, ili kupambana na ujinga, umaskini na baa la njaa; mambo ambayo yanaweza kuchochea vurugu na kinzani za kijamii. Kumbe, kuna haja kwa watu wote kushikamana katika ujenzi wa Jumuiya inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano!

Mahojiano
23 June 2020, 13:46