Tafuta

Vatican News
Tarehe 27 Juni 2020 Shirika la Wayesuit limepata Mapadre Wapya 2 na Mashemasi 18 na kati yao kuna umati mkubwa wa Mashemasi kutoka Barani Afrika. Tarehe 27 Juni 2020 Shirika la Wayesuit limepata Mapadre Wapya 2 na Mashemasi 18 na kati yao kuna umati mkubwa wa Mashemasi kutoka Barani Afrika.  (Society of Jesus)

Wayesuit Wapata Mapadre Wapya 2 na Mashemasi Wapya 18! Hadi...!

Kardinali Michael Czerny, SJ., tarehe 27 Juni 2020, kwenye Kanisa Kuu la “Gesù” lililoko Roma, ametoa Daraja Takatifu ya Upadre na Ushemasi. Mashemasi wawili kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati na Poland wamepewa Daraja Takatifu ya Upadre na Majandokasisi 18 kati yao kutoka Barani Afrika ni wale wanaotoka: Rwanda, Burundi; Madagascar na DRC, ambao wamepewa Daraja ya Ushemasi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, kazi ya Mapadre, maadam imeunganika kiundani na Daraja ya Maaskofu, inashiriki mamlaka ya Kristo ambayo kwayo mwenyewe hukuza, hutakasa na kuongoza Mwili wake. Ndiyo sababu ukuhani wa mapadre, ijapo hudai kwanza sakramenti zinazoingiza katika ukristo, lakini hutolewa kwa njia ya ile sakramenti maalum ambayo kwa ajili yake mapadre, kwa mpako wa Roho Mtakatifu, hutiliwa muhuri wa pekee unaowafanya kuwa mfano wa Kristo Kuhani; hivi kwamba wawezeshwe kutenda kwa jina la Kristo na katika nafsi yake aliye kiongozi. Aidha, mapadre wanalishiriki, kwa kadiri yao, jukumu la Mitume; ndiyo maana wanapewa kutoka kwa Mungu neema inayowawezesha kuwa wahudumu wa Yesu Kristo kati ya mataifa kwa njia ya huduma takatifu ya Injili, ili sadaka ya mataifa iwe ya kupendeza, na iliyotakaswa katika Roho Mtakatifu. Maana kwa njia ya tangazo la kitume la Injili kweli Taifa la Mungu linaalikwa na kukusanywa, hivi kwamba wote wanaoshiriki katika Taifa hili, madhali wanatakaswa kwa Roho Mtakatifu, waweze kujitoa wenyewe wawe “hostia iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu” (Rum 12:1).

Tena kwa njia ya huduma ya mapadre dhabihu ya kiroho ya waamini kweli inakamilishwa, kwa kuwa inaunganishwa na dhabihu ya Kristo aliye Mshenga pekee; maana kwa mikono ya mapadre na kwa jina la Kanisa zima dhabihu hii hutolewa katika Ekaristi pasipo kumwaga damu na kwa mtindo wa kisakramenti, hadi Bwana mwenyewe atakapofika. Napo ndipo inapolenga huduma ya mapadre na kupewa kipeo chake. Maana utumishi wao unaoanza kwa tangazo la Injili, hupewa nguvu yake na matunda yake kutoka katika dhabihu ya Kristo; na madhumuni yake ndiyo kwamba “mji mzima uliokombolewa, yaani kusanyiko na jamii ya watakatifu, ujitoe kwa Mungu uwe dhabihu ya kilimwengu (universale sacrificium) kwa njia ya Kuhani Mkuu, ambaye pia alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu katika mateso yake, ili kutufanyiza tuwe mwili wa Kichwa kitukufu namna hii.”

Hivyo, shabaha wanayolenga mapadre kwa huduma na maisha yao ndiyo utukufu wa Mungu Baba wanaopaswa kuutafuta katika Kristo. Nao utukufu u kwamba wanadamu wapokee kwa utambuzi, kwa hiari na kwa moyo wa shukrani kazi timilifu ya Mungu iliyotendeka katika Kristo na kuidhihirisha katika maisha yao yote. Kwa sababu hiyo, mapadre, wawe wanajitolea katika sala, ibada na liturujia ya Kanisa, wawe wanalihubiri Neno la Mungu, wawe tena wanatoa dhabihu ya Ekaristi na kutoa Sakramenti nyingine, ama wanatekeleza huduma nyingine kwa kuwahudumia watu, basi wanachangia katika kuukuza utukufu wa Mungu na wakati huohuo kuwaendeleza watu katika uzima wa kimungu. Na mambo hayo yote ambayo hububujika katika Pasaka ya Kristo yatapata utimilifu kamili katika ujio mtukufu wa Bwana mwenyewe, pindi atakapompa Mungu Baba Ufalme wake. (Rej. Presbyterorum Ordinis n. 2.).

Ni katika muktadha huu, Kardinali Michael Czerny, SJ., Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu, Jumamosi, tarehe 27 Juni 2020, kwenye Kanisa Kuu la “Gesù” lililoko Jimbo kuu la Roma, Italia, ametoa Daraja Takatifu ya Upadre na Ushemasi.  Mashemasi wawili kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati na Poland wamepewa Daraja Takatifu ya Upadre na Majandokasisi 18 kati yao kutoka Barani Afrika ni wale wanaotoka: Rwanda, Burundi; Madagascar na DRC, ambao wamepewa Daraja ya Ushemasi. Sehemu kubwa ya waamini wameshiriki kwa njia ya mitandao ya kijamii kutokana na hofu ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Kardinali Michael Czerny, SJ., anasema, hofu hii ni sawa ni ile iliyowakumba wanafunzi wa Yesu, hadi Siku ile ya kwanza ya Juma Yesu alipowatokea na kuwaambia “Amani kwenu” akawaonesha mikono yake na ubavu wake. Akawapatia Roho Mtakatifu na kuwatuma kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Mapadre na Mashemasi wapya wamewekwa wakfu kwa ajili ya huduma kwa Shirika ya Wayesuit na Kanisa katika ujumla wake. Mapadre na Mashemasi hawa wanatumwa kuwahubiri maskini Habari Njema ya Wokovu. Kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa!

Ni viongozi wa Kanisa wanaopaswa daima kusoma alama za nyakati, kwa kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na waamini walei wanaoshiriki pia: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Ni wakati wa kutoka huko Sakristia, ambako Mapadre na Mashemasi “wamejichimbia kwa raha zao wenyewe” ili kupambana na matatizo na changamoto za walimwengu kwa mwanga wa Injili ya Kristo Mfufuka. Wanapaswa kuwa ni mashuhuda jasiri wa Kristo, huku wakiungwa mkono na ndugu, jamaa na marafiki zao kwa hali na mali. Mang’amuzi ya miito ni dhamana na wajibu wa Kanisa zima anasema Kardinali Michael Czerny, SJ. Huduma hii haipaswi kubinafsishwa na wakleri katika maisha na utume, bali wajitahidi kuwashirikisha pia waamini walei, kwa kufikiri na kutenda kama timu, jambo linalohitaji fadhila ya unyenyekevu, ujasiri pamoja na kutambua mipaka ya kila mmoja wao.

Katika mazingira ya hofu na taharuki kubwa mintarafu janga kubwa la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, waamini wawe na ujasiri wa kumwomba Mwenyezi Mungu awasaidie kuuona ulimwengu kwa jicho la Kristo Yesu. Janga la Corona, COVID-19 limeonesha matatizo, changamoto na masuala mtambuka katika mifumo mbali mbali ya kijamii na kiuchumi. Pengo kubwa kati ya maskini na matajiri katika huduma ya afya limejionesha sana, kiasi cha baadhi ya watu ndani ya jamii kujisikia kuwa wametengwa na kusahauliwa katika vipaumbele vya huduma ya afya kitaifa na kimataifa. Kanisa linapaswa kuwa ni mwanga wa ukweli wa Injili, lisaidie kusikiliza kilio cha Mama Dunia na maskini na hatimaye, kukukipatia majibu muafaka, kwa ajili ya kulinda na kudumisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mapadre na Mashemasi wapya wawe ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili; wafurahi na kushangalia, utukufu wa Mungu unaojidhihirisha kati ya watu wa Mungu. Wawe faraja na furaha kwa watu wa Mungu wanapotekeleza dhamana yao ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Mapadre na Mashemasi, SJ.
30 June 2020, 14:09