Tafuta

Vatican News
Padre Federico Lombardi anasema mapambano dhidi ya janga la COVID-19 yanahitaji toba na wongofu wa ndani! Padre Federico Lombardi anasema mapambano dhidi ya janga la COVID-19 yanahitaji toba na wongofu wa ndani! 

Janga la Virusi vya Corona, COVID-19: Toba na Wongofu wa ndani!

Mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19: Kuna haja kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia, kujikita katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kuongoa roho za watu, tayari kuambata huruma, haki jamii na amani na utulivu wa ndani ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha mwanadamu! Ni mapema mno kusahau Corona!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika kipindi hiki cha janga kubwa la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kuna haja kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia, kujikita katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kuongoa roho za watu, tayari kuambata huruma, haki jamii na amani na utulivu wa ndani ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha mwanadamu! Padre Federico Lombardi katika makala yake inayojulikana kama “Shajara ya Kipeo cha Corona, COVID-19 anasema, watu wengi wamekwisha kuonja adha ya kuugua au kuuguza wapendwa wao. Leo hii, watu wengi wameingia taharuki ya maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona. Lakini, hali hii pia inaweza kuwa na mwelekeo chanya katika maisha ya watu wa Mungu.

Sera, mikakati, miradi na vipaumbele mbali mbali vimebadilika kutokana na maambukizi ya Corona, COVID-19. Hii inaonesha udhaifu wa maisha ya mwanadamu mbele ya Fumbo kuu la Mwenyezi Mungu. Mwanadamu amegundua kwamba, hatima ya maisha yake haiko mikononi mwake mwenyewe, hata kama kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi ya tiba ya mwanadamu. Ni katika muktadha huu, binadamu amekuwa “mdogo kuliko hata kidonge ya pilton”, hali ambayo imemfanya kuwa mnyenyekevu kuliko kawaida yake. Watu wameguswa na kutikiswa kutoka katika undani wa maisha yao na kuanza pole pole kujenga na kudumisha umoja na mafungamano ya kijamii! Wamegundua uwepo wa jirani na umuhimu wao kiroho na kimwili! Lakini kadiri siku zinavyozidi kuyoyoma, kama kawaida yake, mwanadamu anaanza kusahau na kutaka kurejea tena katika maisha yake ya kale, kurejea katika mazoea.

Binadamu anaanza kujiwekea sera, mikakati na miradi ili kwa haraka iwezekanavyo aweze kuzima kiu yake. Pole pole, sala inaanza kusahalika tena, kwa kudhani kwamba, katika kipindi cha kuwekwa karantini, huo ndio ulikuwa ni muda wa sala, lakini sasa “mwanadamu ponda mali, eti kufa kwaja”. Maajabu yaliyoje, kwamba, mwanadamu anaanza tena kumsahau Mungu aliyekuwa anampigia magoti usiku na mchana, akiomba amwondolee janga la Corona, COVID-19! Huu ni ugonjwa ambao unasambaa kwa haraka na kuwaambukiza wengine. Hapa binadamu amejifunza kuona udhaifu wake kwa sababu gonjwa hili limeleta changamoto kubwa katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Limesababisha maafa makubwa katika maisha ya watu wengi na kwamba, madhara yake, si rahisi sana kuweza kusahaulika kwa siku za usoni!

Padre Lombardi anaangalia sehemu ya pili ya shilingi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 na kusema, hapa kuna haja ya kuangalia yale mazuri yanayobubujika kutokana na ugonjwa wa Corona. Yohane Mbatizaji katika mahubiri yake, alikazia toba na wongofu wa ndani! Hili ni neno muhimu sana katika Kipindi cha Kwaresima ambayo kwa mwaka 2020, waamini wamekiadhimisha kwa uwepo wa gonjwa la Corona, COVID-19. Hili ni jambo la kushangaza sana katika maisha ya waamini. Toba na wongofu wa ndani ni maneno yaliyokuwa yanabubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu, yaani waamini walikuwa wanahimizwa kuanza mchakato wa kumrudia tena Mwenyezi Mungu. Maafa makubwa yaliyosababishwa na Corona, COVID-19 yasidhaniwe hata mara moja kwamba, ni kielelezo cha hasira ya Mungu kama baadhi ya watu wanavyotaka kuwasadikisha wengine!

Ikumbukwe kwamba, tangu mwanzo wa kuumbwa kwambe, mwanadamu amejikuta akiogelea katika dimbwi la dhambi! Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Ugonjwa wa Corona, hatimaye utapita, lakini utakuwa umeacha madhara makubwa katika maisha ya watu, lakini watu hawana budi kuanza tena upya, ili kusonga mbele kwa imani na matumaini sanjari na kuendelea kujikita katika upendo na mshikamano. Matumaini haya yanapaswa kusimikwa katika upendo kama kielelezo cha imani tendaji! Jambo la msingi ni toba na wongofu wa ndani, kwa kutambua kwamba, binadamu ni kiumbe dhaifu, lakini amepewa kazi ya uumbaji ili kulinda na kuitawa kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Laudato si”.

Hiki ni kipindi cha kujikita katika fadhila ya unyenyekevu. Ni wakati wa kufanya upembezi yakinifu kuhusu mfumo wa afya na elimu; kuhusu umuhimu na matumizi ya maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano ya jamii. Ni matumaini ya watu wa Mungu kwamba, hata sayansi ya tiba ya mwanadamu itabidi kupiga hatua mbele. Mwanadamu anapofikiri kutoa majibu ya kisayansi, ili kuboresha tija na uwezo wake wa kufikiri na kutenda kuna haja pia ya kujielekeza zaidi katika maisha ya kiroho! Kuna umuhimu wa kufanya toba na wongofu wa maisha ya kiroho! Hii ni kwa sababu, mwanadamu ataendelea kuwa ni kiumbe mbele ya Mwenyezi Mungu. Kumbe, ni muhimu kujenga na kudumisha amani na kila kiumbe; amani na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani, ili kweli maisha yaweze kupata maana halisi yanahitaji kufumbatwa katika toba na wongofu wa ndani!

Wongofu

 

 

 

03 June 2020, 07:10