Tafuta

Vatican News
Kardinali De Donatis amezindua Mwongozo wa Shughuli za Kichungaji Jimbo kuu la Roma kwa mwaka 2020 hadi mwaka 2021 Kardinali De Donatis amezindua Mwongozo wa Shughuli za Kichungaji Jimbo kuu la Roma kwa mwaka 2020 hadi mwaka 2021  (Vatican Media)

Mwongozo wa Shughuli za Kichungaji Jimbo Kuu la Roma: 2020-2021

KardinaliDe Donatis, katika tafakari yake amegusia kwa kina na mapana mambo makuu yafuatayo: Haki ya matumaini baada ya janga la COVID-19 katika mwanga wa Pasaka; Umuhimu wa kutoka ili kukutana na kukumbatiana na watu; mageuzi makubwa yaliyojitokeza katika kipindi hiki katika maisha na utume wa familia; mahusiano na mafungamano ya watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji, tarehe 24 Juni 2020, Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu mkuu Jimbo kuu la Roma, ameongoza masifu ya jioni pamoja na kuwakabidhi Maparoko pamoja na wawakilishi wa waamini walei Mwongozo wa Shughuli za Kichungaji Jimbo kuu la Roma kwa mwaka 2020-2021. Imekuwa ni fursa ya kuwapongeza Mapadre wanaokumbukia Jubilei ya Miaka 25, 50 na 60 tangu walipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mwongozo huu ni mwaliko wa kufanya tafakari ya kina kuhusu maisha na utume wa Mama Kanisa baada ya waamini kupapaswa na kutikiswa na janga kubwa la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Imekuwa ni fursa ya kumwimbia tena Mwenyezi Mungu, utenzi wa sifa na shukrani kwa wema, ukarimu na tunza yake ya Kibaba.

Familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma inataka kuendelea kumtumikia Mungu kadiri inavyowezekana, ikiwa imeungana na mchungaji wake mkuu, yaani, Baba Mtakatifu Francisko. Wameomba ulinzi na tunza ya Bikira Maria katika kipindi hiki cha malezi na majiundo endelevu kwa watu wa Mungu, Jimbo kuu la Roma. Itakumbukwa kwamba, Mwongozo wa Shughuli za Kichungaji Jimbo Kuu la Roma kwa Mwaka 2019, ulikuwa ni mwaliko wa kusikiliza kwa moyo na kujibu kilio cha watu wa Mungu. Kardinali Angelo De Donatis, katika tafakari yake amegusia kwa kina na mapana mambo makuu yafuatayo: Haki ya matumaini baada ya janga la Corona, COVID-19 katika mwanga wa Pasaka; Umuhimu wa kutoka ili kukutana na kukumbatiana na watu; mageuzi makubwa yaliyojitokeza katika kipindi hiki katika maisha na utume wa familia; mahusiano na mafungamano ya watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma.

Kardinali Angelo De Donatis anasema, hiki ni kipindi cha kukuza na kudumisha matumaini mapya na yaliyo hai kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ni muweza wa yote, kiasi kwamba, anaweza kuwafufua wafu kutoka makaburini, kama alivyosema Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Kesha la Pasaka kwa mwaka 2020. Huu ni wakati wa kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa baada ya kupitia vipindi vya giza, ukimya na majaribu makubwa. Lakini mbegu ya Neno la Mungu imeendelea kumea na kukua wasivyojua wao, kadiri ya mpango wa Mungu. Rej. Mk. 4:27. Huu ni wakati wa kusoma alama za nyakati, kwa kupembua na kuona vipaumbele katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni wakati wa toba na wongofu wa ndani, Kairos, ili kuweza kutembea kwa umoja na mshikamano. Ni muda wa kuvuka Bahari ya Shamu kama ilivyokuwa kwa Waisraeli. Lengo ni kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na watu wa Mungu; kwa kusikiliza kwa moyo na kujibu kilio chao cha ndani mintarafu Maandiko Matakatifu.

Kanisa ni matunda ya Fumbo la Pasaka. Ugonjwa wa Corona, COVID-19 umesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Roho Mtakatifu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kwa kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu. Ni wakati wa kujizatiti zaidi katika mchakato wa uinjilishaji wa marika ya watu, yaani: vijana na wazee, ili kujenga mahusiano na mafungamano kati ya watu, katika imani na matumaini, ili kutekeleza utume wa Kanisa wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Roho Mtakatifu anapaswa kuwa ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa, tayari kuchangamkia matunda ya imani, matumaini na mapendo, yaliyopandikizwa na Roho Mtakatifu katika nyoyo za waamini. Ni wakati wa kujenga na kuimarisha madaraja ya kukutana, kukumbatiana na kujadiliana na wengine, ili kuendelea kusoma alama za nyakati. Ni muda muafaka wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika ubunifu wa shughuli za kichungaji, ili kumpatia nafasi Roho Mtakatifu “kupindua meza” za vipaumbele vyao vya shughuli za kichungaji!

Kardinali Angelo De Donatis anawataka watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma, kutoka kifua mbele tayari kukutana na kukumbatiana na wenzi wa safari ya maisha yao. Lengo ni kuimarisha imani, matumaini na mapendo, kwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa watu wa Mungu. Watu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kumbe, umoja na mshikamano ni kielelezo cha Fumbo la Utatu Mtakatifu. Huu ni wakati wa kutoka kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, ili kuwashirikisha wengine amana na utajiri wa zawadi ya Mungu. Katika kipindi cha kuwekwa karantini, mambo mengi yamebadilika, hii ikiwa ni pamoja na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Imekuwa ni fursa ya kujenga na kudumisha familia kama Kanisa dogo la nyumani. Wanandoa wamegundua mambo msingi yanayowaunganisha na udhaifu katika mahusiano yao. Malezi ya vijana kwa wazazi wa upande mmoja yamekuwa ni changamoto pevu sana. Kuna baadhi ya familia zimekumbwa na upweke hasi kutokana na watoto au wazazi kuishi na kufanya kazi mbali na familia zao. Umoja na mafungamano ya kifamilia yameguswa na kutikiswa sana.

Kipindi hiki, waamini wengi wamejenga na kuimarisha upendo na mshikamano; urafiki na ujirani mwema kwa kusaidiana kwa hali na mali. Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, ni matunda ya mwanga wa Neno la Mungu unaozingatia ukweli na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo. Unatoa mwelekeo wa Kristo Yesu katika kukuza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuzijengea familia uwezo wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Ni wosia unaokazia upendo thabiti ndani ya familia; upendo unaogeuka kuwa ni chemchemi na asili ya maisha. Baba Mtakatifu anatoa mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji mintarafu utume wa maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu anawataka wazazi na walezi kuimarisha elimu na makuzi ya watoto wao, ili waweze kuwajibika kikamilifu katika maisha yao. Ni wajibu wa Kanisa kuwasindikiza, kung’amua na kuwasaidia wanafamilia wanaolegalega katika maisha na wito wao wa ndoa na familia.

Huu ni wakati wa kuwekeza zaidi katika utume wa familia kwa kujenga na kuimarisha Liturujia ya Familia; umoja na mafungamano ya dhati; kwa kukazia umuhimu wa kupokea Sakramenti za Kanisa. Familia iwe ni kitovu na hatima ya uinjilishaji. Ni wakati pia wa kupambana na umaskini wa hali na kipato; kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema. Kardinali Angelo De Donatis anasema, kumekuwepo na mabadiliko makubwa ya mahusiano na mafungamano kati ya watu wa Mungu. Mapadre wameonesha uwepo wao wa karibu kwa waamini katika raha na shida; wakawa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu. Wamejenga na kuimarisha mawasiliano na waamini wao kwa njia mbali mbali. Kumbe, kuna mambo mengi yakuendelea kujifunga baada ya waamini kuzuiliwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Ibada na Liturujia ya Kanisa. Kipindi hiki kiwe ni muda wa kuwahudumia kwa moyo wa huruma na mapendo, maskini, wagonjwa na wazee. Waamini waendelee kujenga utamaduni wa kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa familia na Kanisa katika ujumla wake, inapaswa kukuzwa na kudumishwa!

Jimbo Kuu la Roma
25 June 2020, 14:20