Tafuta

Vatican News
Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali amempongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa ushupavu wa kichungaji wakati wa janga la Corona, COVID-19. Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali amempongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa ushupavu wa kichungaji wakati wa janga la Corona, COVID-19.  (Vatican Media)

Dekano wa Baraza la Makardinali Amshukuru Papa Francisko!

Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, kwa niaba ya Makardinali amemshukuru Papa Francisko katika kipindi cha janga kubwa la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Baba Mtakatifu ameonesha uwepo na ukaribu wake kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wake wa upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali kwa niaba ya Maaskofu wakuu walioteuliwa katika kipindi cha Mwaka 2019 hadi Juni 2020, kabla ya Ibada ya Misa Takatifu, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa moyo wake wa ujasiri, nguvu na faraja kwa watu wa Mungu. Katika kipindi cha janga kubwa la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Baba Mtakatifu Francisko ameonesha uwepo na ukaribu wake kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wake wa upendo. Watu wengi wamebahatika kumsikiliza na kumwona Baba Mtakatifu Francisko akiadhimisha Ibada ya Misa Takatifu mubashara kutoka kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, zilizokuwa zinarushwa na vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii, ili kuwapatia watu wa Mungu, neno la faraja, imani na matumaini.

Baba Mtakatifu ametolea nia za Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mahitaji ya watu mbali mbali, kwa wagonjwa, madaktari, wauguzi, wanafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na makundi na marika ya watu waliokuwa wanahitaji msaada na faraja ya pekee kwa njia ya sala. Hii imekuwa ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maadhimisho ya Juma Kuu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, katika ukimya na utupu, ni picha ambazo zimeacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za watu wengi sehemu mbali mbali za dunia. Tafakari za Sala ya Malkia wa Mbingu na Malaika wa Bwana wakati wa Jumapili pamoja na Katekesi, kila Jumatano, ni matukio ambayo yamemwezesha Baba Mtakatifu Francisko kuingia katika nyumba na familia za watu mbali mbali duniani, ili kuwapatia faraja na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Katika kipindi hiki cha mateso na mahangaiko makubwa ya watu, Mama Kanisa ameendelea kujipambanua kuwa rafiki wa maskini na wale wote wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali za maisha. Mshikamano wa huruma na upendo, umeliwezesha Kanisa kuanzisha Mfuko wa Mshikamano ujulikanao kama “Yesu, Mfanyakazi” kwa ajili ya mji wa Roma, ili kuwasaidia watu wa Mungu walioguswa na kutikiswa na janga la Corona, COVID-19, walau waweze kupata mahitaji yao msingi. Umoja, upendo na mshikamano katika Jumuiya ya Kimataifa ni changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu kwa kuwakumbusha watu wa Mungu kwamba, binadamu wote wanaunda familia kubwa ya watu wa Mungu, kumbe, wanapaswa kusaidiana kwa hali na mali na kwamba, haiwezekani kuwageuzia maskini kisogo. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu; kwa kuimarisha imani, matumaini na mapendo kwa Mungu aliye hai.

Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, kwa mara nyingine tena amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa yale yote aliyotenda, anayoendelea kutenda kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Maaskofu wakuu wapya wanapenda kurudia tena kiri ya imani kwa kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Khalifa wa Mtakatifu Petro ni msingi thabiti wa umoja wa Kanisa.

Kardinali Re: Dekano
30 June 2020, 06:49