Tafuta

Vatican News
Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuketi ili kung'oa mizizi ya mifumo mbali mbali ya ubaguzi, ukatili unaofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu! Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuketi ili kung'oa mizizi ya mifumo mbali mbali ya ubaguzi, ukatili unaofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu!  (ANSA)

Vatican: Jumuiya ya Kimataifa Ing'oe Mizizi ya Ubaguzi na Ukatili

Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuketi kitako na kuanza kujadili mizizi ya mifumo ya ubaguzi inayoendelea kukiuka haki msingi za binadamu, ukatili unaofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na uvunjwaji wa haki msingi za waandamanaji! Vatican inakaza kusema, mifumo mbalimbali ya ubaguzi ni mambo ambayo kamwe hayawezi kamwe kuvumiliwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mauaji ya kinyama ya watu wasiokuwa na hatia, yamesababisha hasira kubwa, majonzi, huzuni na wasi wasi mkubwa kutokana na vitendo vya chuki na ubaguzi wa rangi pamoja na maamuzi mbele. Binadamu wote ni sawa kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Amani na haki jamii; umoja, utulivu na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni mambo msingi katika maisha ya jamii yoyote ile. Saratani ya mifumo mbali mbali ya ubaguzi wa rangi ni mateso ambayo yameacha madonda makubwa katika dhamiri za watu, lakini kwa bahati mbaya, hayakupata ufumbuzi wa kudumu ndiyo maana hata wakati huu, yanaendelea kujitokeza na kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Utu, heshima, haki msingi za binadamu; umoja na udugu wa kibinadamu ni tunu msingi zinazopaswa kurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi na kuendelea kupyaishwa, ili tunu hizi msingi zisichafuliwe na dhambi, kiasi cha kusababisha ukosefu wa haki msingi, vurugu na ghasia pamoja na ukandamizaji wa utu na heshima ya binadamu!

Chuki, vita, vurugu na ghasia ni hatari sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini wajielekeze zaidi katika kudumisha misingi ya haki, usawa pamoja na kuendelea kujikita katika utawala wa sheria. Ubaguzi ni dhambi ambayo kamwe haiwezi kufumbiwa macho kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Waamini wawe waaminifu kwa Injili ya Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake! Wasimame kidete kulinda na kudumisha utu, heshima, haki msingi, ustawi na maendeleo ya wote sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu! Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Ivan Jurkovič, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika ofisi za Umoja wa Mataifa ziliko mjini Geneva, Uswiss, hivi karibuni amesema kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuketi kitako na kuanza kujadili mizizi ya mifumo mbali mbali ya ubaguzi inayoendelea kukiuka haki msingi za binadamu, kwa kujikita katika mfumo wa ubaguzi wa rangi, ukatili unaofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na uvunjwaji wa haki msingi za waandamanaji!

Vatican inakaza kusema, mifumo mbalimbali ya ubaguzi ni mambo ambayo kamwe hayawezi kuvumiliwa na Jumuiya ya Kimataifa. Hii inatokana na ukweli kwamba, binadamu wote wanaounda familia kubwa ya binadamu, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wana utu, heshima na haki zao msingi. Serikali mbali mbali zinapaswa kutambua haki hizi, ili kulinda, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Uwezekano wa kuishi pamoja kati ya Mataifa mbali mbali unategemezwa na misingi ileile ambayo ingekuwa ni miongozo ya uhusiano kati ya binadamu yaani: ukweli, haki, mshikamano wa kweli kimatendo na uhuru. Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusu kanuni za kikatiba juu ya jamii ya kimataifa yanasema kwamba, mahusiano kati ya watu na jumuiya za kisiasa yanaratibiwa kimantiki, kihaki, kisheria na kwa maafikiano bila vurugu au vita wala aina yoyote ya ubaguzi, vitisho na udanganyifu. Huu ni mwaliko wa kuondokana na ubaguzi wa rangi na maamuzi mbele kwa kutambua kwamba, kila binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ubaguzi wa aina yoyote ile ni jambo ambalo kamwe haliwezi kuvumiliwa wala kufumbiwa macho kwa kisingizio cha kulinda utakatifu wa maisha. Lakini, pia, watu wanapaswa kutambua kwamba, ghasia na vurugu za hivi karibuni, zimepelekea watu wengi kujeruhiwa pamoja na uharibifu mkubwa wa mali. Mambo mengi yanapotea kutokana na vita pamoja na ghasia.

Ubaguzi Duniani
20 June 2020, 06:56