Tafuta

Askofu Mario Grech anafafanua umuhimu wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa kifamilia, kikanisa na kijamii katika ujumla wake. Askofu Mario Grech anafafanua umuhimu wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa kifamilia, kikanisa na kijamii katika ujumla wake. 

Dhana ya Sinodi Katika Maisha ya Kifamilia, Kikanisa na Kijamii!

Dhana ya Sinodi inapaswa kumwilishwa si tu katika maisha na utume wa Kanisa bali hata katika jamii, kama kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu, ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha! Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na COVID-19 limegusa na kutikisa misingi ya maisha ya watu: kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata kiimani! Sinodi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa: Sinodi ya XVI ya Maaskofu itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba 2022 itaongozwa na kauli mbiu “Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, ushiriki na utume”. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kuhusu umuhimu wa kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kukazia umuhimu wa watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Mambo yanayopaswa kuzingatiwa ni: Ufahamu wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani; ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Haya ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya katika ulimwengu mamboleo. Dhana ya Sinodi ni wazo lililotolewa na Mtakatifu Paulo VI, linaloihusisha Familia ya Mungu katika ujumla wake.

Sinodi ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa wa kutaka kutembea kwa pamoja chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, kama sehemu ya mchakato wa utambulisho wa Kanisa na uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ndio ufafanuzi wa kina uliotolewa na Mtakatifu Paulo VI, Muasisi wa maadhimisho ya Sinodi za Kanisa, mara baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Sinodi ni chombo cha uinjilishaji unaolisaidia Kanisa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, baada ya kutembea kwa pamoja katika sala, tafakari na mang’amuzi mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa. Askofu Mario Grech, Katibu Mwambata wa Sinodi za Maaskofu katika mahojiano maalum na vyombo vya mawasiliano ya jamii mjini Vatican anasema, dhana ya Sinodi inapaswa kumwilishwa si tu katika maisha na utume wa Kanisa bali hata katika jamii, kama kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu, ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha!

Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limegusa na kutikisa misingi ya maisha ya watu: kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata kiimani. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, anawaalika waamini kuanza mchakato wa wongofu wa shughuli za kichungaji, ili kugundua na kutambua njia mbali mbali za kuweza kuutafakari Uso wa Kristo, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Katika kipindi cha karantini, mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu, viongozi mbali mbali wa Kanisa wameibuka kutoka “Sakristia” walikokuwa wamejichimbia na kuanza kutumia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii ili kuwashirikisha waamini wao: Tafakari ya Neno la Mungu, Sala, Liturujia na mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa.

Hii ni changamoto kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anaendelea kusoma alama za nyakati kwa kukaza uzi na kamwe asibweteke na kutaka kurejea tena kwenye mazoea ya zamani. Imani inapaswa kuwa ni chachu ya mabadiliko katika maisha ya waamini. Huu ni wakati muafaka wa kutangaza na kushuhudia familia kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, “Domus ecclesiae” linalojengwa na kuimarishwa na wanandoa wenyewe katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku kwa kutambua kwamba, Kristo Bwana, yuko daima pamoja nao! Ni muda wa kufanya mazoezi na kumwilisha Injili ya huruma, upendo na msamaha. Ni wakati wa kukaa pamoja na wanafamilia ili kukazia malezi bora na utu wema. Ni muda muafaka wa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kusikilizana, kuheshimiana na kuthaminiana.

Ni muda wa kuratibu vyema rasilimali muda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia. Umefika wakati kwa wanandoa kuangaliana usoni bila kupepesa pepesa macho ili kujenga na kuimarisha upendo na urafiki wao wa dhati, daima wakimwachia nafasi Kristo Yesu. Mazoezi haya yasaidie kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu. Ni muda wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni wakati uliokubalika wa kusali na kutafakari pamoja Neno la Mungu, ili janga la Virusi vya Corona, COVID-19 litakapopita na waamini kurejea tena Kanisani, wawe na ari na mwamko mpya. Askofu Mario Grech anasema, adhimisho la  Fumbo la Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa ni kiini cha Parokia. Kimsingi, Fumbo la Ekaristi Takatifu linaadhimishwa siku ya Bwana; Jumuiya ya waamini inapopata nafasi ya kusikiliza, kutafakari Neno la Mungu na hatimaye, kutumwa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao, kama kielelezo cha imani ntendaji!

Neno Parokia, linapata asili yake kutoka katika lugha ya Kigiriki yaani “παρоικια” maana yake “Ujirani”. Kumbe, kwa maneno machache, Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa, mahali pa kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, tayari kutoka kifua mbele kutangaza furaha ya Injili; huruma na upendo wa Mungu. Waamini wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huduma ya upendo kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina. Waamini wawe ni washiriki waaminifu wa Sakramenti za Kanisa. Wajenge na kukuza moyo wa kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kanisa liendelee kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa sababu hawa ni amana na utajiri wa Kanisa. Pia ni walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu.

Majiundo makini na endelevu ya Katekesi yaendelee kupewa msukumo wa pekee katika maisha ya waamini; kwa kusikiliza kilio cha Mama Dunia pamoja na kilio cha maskini, tayari kusikiliza na kutoa majibu muafaka. Mama Kanisa hana budi kuendelea kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Watu watambue umuhimu na uwepo wa Mungu katika maisha yao wakati wa raha na shida.

Dhana ya Sinodi

 

18 June 2020, 08:02