Tafuta

Vatican News
2020.05.30 Balozi wa Kitume Gianfranco Gallone  na Askofu Moses Hamungole wa Zambia 2020.05.30 Balozi wa Kitume Gianfranco Gallone na Askofu Moses Hamungole wa Zambia 

ZAMBIA#Coronavirus.Papa atoa zawadi ya vifaa vya matibabu kwa Baraza la Maaskofu Zambia!

Msaada wa Papa Francisko unazidi kupanuka kwa ajili ya kufariji watu na mateso ya wengi walio hatarini zaidi ulimwenguni katika dharura ya sasa ya virusi vya covid-19.Kwa njia hiyo Papa ametuma zawadi ya vifaa vya matibabu kwa Baraza la Maaskofu nchini Zambia ambapo mashine tatu za kupumulia zinatumika kwa wagonjwa walio mahututi katika hospitali tatu katoliki.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Kwa mujibu wa taarifa zilizotelewa kwenye Blog ya Shirikisho la Baraza la Maaskofu wa Afrika Mashariki (Amecea), limebainisha juu ya Baraza la Maaskofu katoliki nchini Zambia kupokea msaada kutoka Vatican. Hii ni kudhihirisha wazi juu ya orodha ya msaada kutoka kwa Papa Francisko unavyozidi kupanuka kwa ajili ya kufariji watu na mateso yao zaidi kwa walio hatarini ulimwenguni kote katika dharura ya sasa ya virusi vya corona. Kwa mujibu wa Baraza la Maaskofu Zambia (Zccb) wamepokea mashine tatu na vifaa maalum vya kuzuia maambukizi kwa wauguzi miongoni mwake zikiwemo barakoa. Kwa mujibu wa taarifa hizo msaada huo ulikabidhiwa tarehe 25 Mei na Askofu Mkuu Gianfranco Gallone Balozi wa Kitume nchini Zambia na Malawi.

Hospitali tatu katoliki kupokea mashine za kupumulia

Mashine tatu za kupumulia zimelekwa katika Hospitali ya Kumbu kumbu ya Kardinali Adam huko Lusaka, katika Hospitali ya Kitume huko Chilonga, Wilayani Muchinga, na katika Hospitali ya Mtakatifu Dominiki, Wilaya ya Copperbelt.  Zawadi ya Papa Francisko ni kutaka kuonyesha ukaribu na  mshikamano kwa wale ambao wanateska na hawana nyenzo za kutibu, kwa mujibu wa Askofu Mkuu Gallone, Balozi wa Kitume na kuongeza kusema kwamba,  Papa anao wasiwasi mkubwa hata kwa wale wote ambao wamepoteza kazi zao na wala hawana chakula.

Shukrani kwa Papa kutoka kwa Askofu Hamungule kwa niaba Maaskofu Zambia

Vifaa hivyo vimepokelewa na kukabidhiwa na Askofu Moses Hamungole, Askofu wa jimbo katoliki la Monze, ambaye kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Zambia, amemshukuru Baba Mtakatifu, na kubainisha kwamba mashine za kupumulia zinatumika kwa wagonjwa walio na hali mbaya zaidi katika hospitali tatu katoliki. Hata hivyo wakati wa makabidhiano hayo alikuwapo Katibu wa Kudumu wa Wizara ya Afya nchini Zambia, Bwana Kennedy Malama, ambaye ameonesha utambuzi muhimu wa mchango wa Kanisa mahalia hasa kwa sasa katika dharura ya kiafya.

Kanisa la Zambia na Jumuiya ya Kijesuit

Kanisa la Zambia lilihamasishwa mara moja katika kusaidia mpango wa misaada uliowekwa na serikali ya Lusaka. Kunako Aprili iliyopita Baraza la Maaskofu Zambia walizindua mfuko maalum wa kufadhili  kwa ajili kuzuia na kusaidia wagonjwa, lakini pia kwa wazee, watu wenye ulemavu wa akili na kimwili, watoto yatima na wanao hitajika zaidi. Msaada huo wa mwisho uliotolewa umeongezea ule Msaada wa Covid-19 wa Shirika la Yesu (Jesuit) ambao ni mpango mpya wa misaada uliozinduliwa katika Wilaya ya Zambia na Malawi ili  kusaidia vikundi vya kijamii vilivyo katika mazingira magumu. Kufikia tarehe 29 Mei, kulikuwa na kesi karibu 1,057 katika nchi hiyo pamoja na walipona ni 779 na vifo 7.

30 May 2020, 10:40