Tafuta

Vatican News
Vatican: Palestina na Israeli zinapaswa kudumisha mchakato wa majadiliano ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vatican: Palestina na Israeli zinapaswa kudumisha mchakato wa majadiliano ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.  (Vatican Media)

Vatican: Palestina na Israeli: Wajadiliane Kudumisha Amani!

Vatican inapenda kusisitizia umuhimu wa kuheshimu Sheria za Kimataifa pamoja na Maazimio mbali mbali yaliyofikiwa na Umoja wa Mataifa, ili kuwawezesha watu wa Mataifa haya mawili kuishi kwa amani na utulivu katika mipaka iliyokubaliwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1967. Vatican inaendelea kufuatilia kwa ukaribu zaidi, hali tete huko Palestina ilikudumisha amani na utulivu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chama cha ukombozi wa Wapalestina, PLO kiliundwa kunako mwaka 1964 kuongoza harakati za ukombozi wa Wapalestina kupitia mapambano ya kijeshi. PLO inatambuliwa kama mwakilishi pekee halali wa Watu wa Palestina na mataifa zaidi ya 100, ambayo kina uhusiano nayo wa kidiplomasia, na kimekuwa kikipatiwa hadhi ya Mwanachama Mtazamaji katika Umoja wa Mataifa tangu 1974. PLO ilichukuliwa na Marekani na Israel kuwa kundi la kigaidi hadi mkutano wa Madrid wa mwaka 1991 uliotangua msimamo huu. Kunako Mwaka 1993, PLO ilitambua haki ya Israel kuwepo kwa amani na kukubali maazimio nambari 242 na 338 ya Umoja wa Mataifa na kujiweka mbali na vitendo vya kigaidi na vurugu, na hii iliifanya Israel kukitambua chama hicho kama mwakilishi pekee wa watu wa Palestina.

Hivi karibuni, Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican, alipata nafasi ya kuzungumza kwa njia ya simu na Bwana Saeb Erkat, Katibu mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Wapalestina, PLO na Kiongozi mkuu wa majadiliano. Lengo la mazungumzo haya, lilikuwa ni kuijulisha Vatican kuhusu maendeleo yaliyofikiwa hivi karibuni nchini Palestina na hatari ya Israeli kutaka kuingilia kwa mabavu eneo la Palestina, hali ambayo inahatarisha sana mchakato wa majadiliano ya amani kati ya nchi hizi mbili. Taarifa iliyotolewa na Vatican inaonesha kwamba, Vatican inapenda kusisitizia umuhimu wa kuheshimu Sheria za Kimataifa pamoja na Maazimio mbali mbali yaliyofikiwa na Umoja wa Mataifa, ili kuwawezesha watu wa Mataifa haya mawili kuweza kuishi kwa amani na utulivu katika mipaka iliyokubaliwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1967.

Vatican inaendelea kufuatilia kwa ukaribu zaidi, hali tete huko Palestina, jambo linaloweza kuvuruga mchakato wa majadiliano ya amani. Ni matumaini ya Vatican kwamba, Israeli na Palestina zitaweza kupata muafaka wa kuendeleza majadiliano mubashara, ili hatimaye, kuweza kufikia makubaliano yanayopania ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa pande hizi mbili, kwa msaada kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa. Ni kwa njia ya majadiliano, Wayahudi, Wakristo na Waislam wataweza kuishi kwa amani na utulivu, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi.

Palestina

 

25 May 2020, 13:28