Tafuta

Vatican News
Jumuiya ya Umoja wa Ulaya inaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 70 ya Umoja, Amani na Mshikamano wa dhati! Jumuiya ya Umoja wa Ulaya inaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 70 ya Umoja, Amani na Mshikamano wa dhati! 

Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU: Kusaidiana na Kushikamana!

Bi Ursula Von der Leyen, katika Kumbukumbu ya Miaka 70 ya Tamko la R. Schuman, anapenda kukazia ari na mwamko uliotolewa na waasisi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya; kwa kujizatiti katika umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza hasa kutokana na janga kubwa la ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU itajikita katika matumaini ikiwa kama binadamu atapewa kipaumbele cha kwanza katika taasisi zake; kwa kumsikiliza kwa makini; kwa kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia; kwa kuheshimu na kuthamini umoja katika tofauti. Jumuiya ya Umoja wa Ulaya inapaswa kushirikiana na kushikamana katika: kutafuta, kutumia na kugawana rasilimali fedha, vitu na akili. Bara la Ulaya litaweza kupata matumaini kwa kuwekeza katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu sanjari na amani, kwani amani ni jina jipya la maendeleo ya watu! Pasi na amani, maeneo ya pembezoni mwa jamii yataendelea kuwa ni vituo vya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; mahali pa fujo, ghasia na vurugu za kijamii.

Matumaini ya Bara la Ulaya anasema Baba Mtakatifu Francisko yanajikita kwa kuwa wazi kwa mambo yanayokuja mbeleni; kwa kuwajengea watu uwezo wa kuanzisha na kuendeleza familia; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea: utu, heshima na utakatifu wa maisha ya binadamu. Changamoto zote hizi ziwe ni fursa ya kuganga na kutibu mapungufu yaliyojitokeza huko nyuma; kwa kushirikiana na kushikamana kwa pamoja; kwa kuamua na kutenda kwa ujasiri. Bi Ursula Von der Leyen, Rais wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU katika mahojiano maalum na Vatican News, kama sehemu ya maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 70 tangu Tamko la Robert Schuman, Waziri Mkuu wa Ufaransa lilipotolewa kunako tarehe 9 Mei 1950 anapenda kukazia ari na mwamko uliotolewa na waasisi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya; kwa kujizatiti katika umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza hasa kutokana na janga kubwa la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Uchoyo, ubinafsi na utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko ni kati ya mambo yanayoipekenyua Jumuiya ya Umoja wa Ulaya. Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 linapaswa kushughulikiwa Kimataifa. Bi Ursula Von der Leyen anasema, tangu achaguliwe kuwa Rais wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU, miezi miwili iliyopita, amekuwa akitumia muda wake kuangalia madhara yanayoendelea kujitokeza ndani na nje ya Bara la Ulaya; hatua muhimu zinazopaswa kuchukuliwa. Anaguswa na mahangaiko ya familia nyingi zisizokuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi kutokana na madhara ya Virusi vya Corona, COVID-19. Anaendelea kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kupambana kikamilifu na janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Watu wengi bado wako kwenye karantini, hawa wanapaswa kusaidiwa kwa hali na mali!

Vita Kuu ya Pili ya Dunia iliacha madhara makubwa kwa watu na mali zao: Kuanzishwa kwa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, kulimaanisha mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ndoto ya waasisi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya ilikuwa ni amani, ustawi, maendeleo na mafungamano ya kijamii, sanjari na kulinda, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Uhuru unaowajibisha na afya bora ni matunda ya juhudi za waasisi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya. Kwa njia ya umoja na mshikamano wa dhati, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya itaweza kuwa na nguvu. Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 70 ya Tamko la Robert Schuman la tarehe 9 Mei 1950, yameadhimishwa wakati ambapo Jumuiya ya Kimataifa bado inapambana na janga kubwa la Virusi vya Corona, COVID-19. Lakini bado kuna nafasi ya kujenga na kudumisha urafiki, umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya na binadamu wote katika ujumla wao!

Kumbukumbu ya Miaka 70 ya Tamko la Robert Schuman ni nafasi ya kukuza na kudumisha: umoja na mshikamano katika huduma kwa waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19; kwa kuboresha huduma inayotolewa kwa waathirika; kwa kulinda na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuendelea kujikita katika maendeleo ya teknolojia rafiki kwa mazingira, ili kujiandaa kikamilifu kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo kwa sasa na kwa siku za usoni! Ulinzi na usalama wa raia na mali zao unaweza kupata mafanikio makubwa, ikiwa kama Serikali za Jumuiya ya Umoja wa Ulaya zitakuwa zimeungana na kushikamana; kwa kuboresha huduma ya afya kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba, dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa wakati! Jumuiya ya Umoja wa Ulaya haina budi kuendelea kujizatiti ili kulinda nafasi za kazi na ajira hasa kutokana na kuyumba kwa uchumi wa kitaifa na kimataifa kutokana na madhara yanayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Kiasi cha Euro Trilioni tatu kimetengwa kwa ajili ya kuwaunga watu mkono; kuyasaidia makapuni ya uzalishaji na huduma pamoja na kuendeleza juhudi za kufufua uchumi. Kiasi cha bilioni 100 kimetengwa kwa ajili ya wafanyakazi walioathirika kwa Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa sasa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya inaendelea kujizatiti katika mchakato wa kufufua uchumi kwa kutenga bajeti kubwa ili kukabiliana na changamoto mamboleo. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kushikamana kwa dhati, ili kupambana na gonjwa la Corona, COVID-19. Tarehe 4 Mei 2020, viongozi wa Umoja wa Jumuiya ya Ulaya, Mashirika na Makampuni ya Kitaifa na Kimataifa pamoja na watu binafsi, walifanikiwa kuchanga kiasi cha bilioni 7.4 ili kuiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kufanya utafiti; kutafuta chanjo na hatimaye, tiba dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Tukio hili limeonesha mafanikio makubwa kwamba, umoja ni nguvu na utengano ni dhaifu!

Jumuiya ya Umoja wa Ulaya

 

11 May 2020, 14:10