Tafuta

2020.05.30 - Ordo virginum 2020.05.30 - Ordo virginum 

Tarehe 31 Mei ni maadhimisho ya miaka 50 tangu kuundwa kwa Ordo Virginium!

Tarehe 31 Mei ni maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa mtindo mwingine wa Watawa walei(Ordo Virginum).Ni mtindo wa wakfu wa kizamani uliozaliwa ndani ya Jumuiya za Wakristo wa kwanza.Tukio hili lilitokea mara baada ya kupindi cha kupungua kwa watawa ambapo kwa utashi wa Papa Paul VI alizindua kwa mara nyingine tena mtindo huu wa wakfu ambao hadi sasa ni watawa walei 5000 ulimwenguni kote.

Na Sr. Angela Rwezaula- Vatican

Kusifu na kushukuru Bwana, kutafakari pamoja na kujitajirisha kwa njia ya kubadilishana uzoefu, ushuhuda kwa Kanisa na ulimwengu ule uzuri wa wito binafsi na kuimarishwa kwa uthabiti wa Kharifa wa mtume Petro ndiyo yalikuwa ndani ya muktadha wa Mkutano wa Kimataifa kwa ajili ya watawa walei.   Mkutano huo ulikuwa ufanyike kuanzia tarehe 28  hadi 31 Mei Jijini Roma kwa kuandaliwa na Shirika la Kipapa kwa ajili ya Maisha ya Kitawa na vyama vya Kitume sambamba na kuadhimisha Jubilei ya kuzaliwa mtindo mwingine wa Watawa walei (Ordo Virginum) miaka 50 iliyopita.

Tarehe 31 Mei watawa wa Italia, kuungana na watawa wengine wote ulimwenguni watafanya mkesha wa sala

Mkutano wa kimataifa kwa ajili ya Watawa walei hakuweza kufanyika kutokana na janga la virusi vya Corona, ambapo waliokuwa wamejiandikisha kuudhuria walikuwa watawa wa kike zaidi 700 wakiwa na maaskofu mbali mbali na wawakilishi kutoka mataifa 61 duniani. Kila kitu kimesitishwa kwa tarehe nyingine ambayo kwa namna moja au nyingine, hapakukosekana fursa za  mapendekezo mengine ya maombi kwa kupitia  njia ya mtandao ya kijamii. Ili kusheherekea miaka 50 kwa ibada, tarehe 31 Mei kwa mfano watawa wa Italia, kwa kuungana na watawa wengine wote ulimwenguni watafanya mkesha wa sala kwa pamoja.

Mtindo huu wa maisha ulikuwapo tayari katika Jumuiya za kwanza za Kikristo

Ilikuwa ni tarehe 31 Mei 1970, kwa matashi ya Papa  Paul VI, alipotoa agizo la Baraza la Kipapa la Nidhamu na Sakramenti ili kutangaza ibada mpya ya watawa kwa kufanya wafufue ule mtindo wa kizamani ulioshuhudiwa katika jamuiya  za Kikristo tangu nyakati za kitume. Ni wito ambao umekua kwa muda sasa , kiasi kwamba tangu mwaka 1970 hadi leo wapo karibia wanawake waliowekwa wakfu 5,000 katika mabara yote. Wawata hawa wanaopewa wakfu huo, bado wana mizizi katika jimbo lao mahalia, yaani wanamoishi na mahali walipokomaa  kwa dahti ule uchaguzi wao wa kumfuata Kristo katika nyayo zake na mahali walipofanya mchakato wao mafunzo ya malezi yao. Kwa dhati mfumo huu wa wakfu kwa walio wengi katika nchi za utume, bado hawajulikani sana, kwa maana waamini walio wengi walizoea kuona watawa walio mavazi rasmi ya shirika. Na mara nyingi, waamini wengi wamekuwa na maoni tofauti dhidi ya mtindo huu wa wakfu hasa katika nchi za kiutumea. Kwa upande wa Bara la Ulaya na Bara la Amerika lote,  mtindo huu umekuwa na mwamko sana katika miaka ya mwisho na miito ni mingi sana.

Ni maisha na uzoefu wa kuishi ukaribu wa wengine kwa mfano wa Yesu

Mtindo wa maisha ya watawa walei kwa namna hiyo hawana ishara ya nje, isipokuwa pete inayotolewa wakati wa ibada ya kujitoa wakfu kwa Bwana na ambayo inaonyesha agano la ndoa na Kristo, na inataka kuelezea upendo na uaminifu wa Mungu kwa ajili ya ubinadamu. Upendo halisi, wenye msimamo, unaosimikwa katika muktadha wa kihistoria na katika eneo mahalia, kwa kuishi ule ukaribu na wengine. Kwa namna ya pekee wanawake wenye wakfu wanashiriki, kulingana na uwezo wao na talanta zao, upendeleo wa Kanisa kwa maskini, katika mateso na waliotengwa. Kwa kawaida wanajitegemea na kujisaidia wenyewe kiuchumi kwa njia ya taaluma na kazi yao na wanaishi kikamilifu kwa kushirikiana na kazi za ubunifu na za ukombozi wa Mungu, huku wakijitahidi kufikia kiwango cha juu cha taaluma yao katika maisha. Hawa ni watawa ambao wapo karibu kila sekta ya maisha kuanzia ya kiafya hadi kisiasa, kutoka katika maisha ya kijamii hadi taaluma ya kufundisha, uandishi wa habari, wa vitabu na wawakili.  Kwa mifano halisi wauguzi wengi na wafanyakazi wa matibabu katika miezi hii wameweza kufanya kazi kubwa  kwa bidii kuwa karibu na wagonjwa wa virusi vya corona.

Marekebisho ya maisha ya wakfu kwa mujibu wa Papa Paulo VI

Katika Hati ya Papa Paulo VI kuhusu marekebisho ya maisha ya wakfu anadhihirisha kuwa “Maisha ya kitawa ya walei, wanaume au wanawake, ni hali iliyokamilika ya kufunga nadhiri kwa  mashauri ya kiinjili. Mtaguso Mkuu una heshima kubwa kwa maisha haya ya kitawa ya walei kwa sababu yanaleta manufaa makubwa kwa kazi ya kichungaji ya Kanisa katika uwanja wa malezi ya vijana, kwa kuwatunza wagonjwa na wa huduma nyinginezo nyingi. Kwa maana hiyo Mtaguso huu pamoja na kuwathibitisha katika wito wao wanachama wa mtindo wa namna hii ya maisha ya kitawa, unawahimiza pia walinganishe maisha yao na mahitaji ya siku hizi.

Maisha ya kiroho yana nafasi ya kwanza

Wenye kuweka nadhiri za ushauri wa kiinjili, kabla ya yote wamtafute na kumpenda Mungu aliyewapenda kwanza (taz. 1Yoh 4:10), na katika mazingira yote wafanye bidii kulisha uhai uliofichwa pamoja na Kristo katika Mungu (taz. Kol 3:3), ambamo huchimbuka na kukuzwa upendo wa jirani kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu na ujenzi wa Kanisa. Mapendo hayo ni moyo na uongozi wa utekelezaji wa mashauri ya kiinjili. Katika wingi huu wa karama, wale wote wanaoitwa na Mungu kutekeleza mashauri ya kiinjili na kuyatimiza kiaminifu, wanajiweka wakfu kwa Bwana kwa namna ya pekee, kwa kumfuasa Kristo ambaye, akiwa bikira na maskini (taz. Mt 8:20; Lk 9:58), aliwakomboa wanadamu na kuwatakatifuza kwa njia ya utii wake mpaka kufa msalabani (taz. Flp 2:8). Vivyo hivyo nao watu, walihimizwa na pendo ambalo Roho Mtakatifu amemimina mioyoni mwao (taz. Rum 5:5) wanaishi zaidi na zaidi kwa ajili ya Kristo na kwa ajili ya Mwili wake ulio Kanisa (taz. Kol 1:24). Kwa hiyo, kama wanavyojiunga kwa ari na Kristo kwa njia ya kujitolea kwao maisha yote, ni kadiri hiyohiyo maisha ya Kanisa yananufaika na utume wake unazidi kuwa na nguvu za kuleta matunda.

Mtaguso Mkuu unaidhinisha kanuni za kijumla kwa ajili ya upyaisho

Kusudi thamani kuu ya maisha ya wakfu kwa njia ya kufunga nadhiri za mashauri ya kiinjili, pamoja na huduma zake muhimu katika mazingira ya leo, yote hayo yalete manufaa makubwa katika Kanisa. Mtaguso huu Mkuu unaidhinisha kanuni, zihusuzo misingi ya kijumla tu ya upyaisho wa maisha na wa nidhamu unaotakiwa katika mashirika ya kitawa, na vilevile katika jamii za maisha ya pamoja pasipo nadhiri, na katika mashirika ya kilimwengu (secularium), hata ingawa kila taasisi inatakiwa kudumisha tabia yake.  Upyaisho wa maisha ya kitawa unadai kurudi kwa daima kwenye chemchemi za maisha ya kikristo na za roho ya mwanzoni ya mashirika, na wakati huohuo kujilinganisha kwa mashirika yenyewe na mazingira ya nyakati yaliyobadilika. Upyaisho huo, chini ya msukumo wa Roho Mtakatifu na ya uongozi wa Kanisa, unatakiwa utekelezwe kadiri ya kanuni hizi za msingi: Kwa vile kanuni ya msingi ya maisha ya kitawa ni kumfuata Kristo kadiri ya agizo la Injili, basi hiyo inabidi iwe kanuni kuu ya kila shirika.

Mashirika yawe na tabia na huduma ya pekee

Ni faida kwa Kanisa lenyewe kwamba mashirika yawe na tabia na huduma ya pekee. Kwa hiyo inafaa roho na lengo maalum la waanzilishi vifahamike na kuhifadhiwa, hali kadhalika mapokeo yanayofaa, kwa sababu hayo yote ni urithi wa kila shirika. Mashirika yote yashiriki katika maisha ya Kanisa na, kadiri ya tabia yake, yapokee na kuchangia kadiri ya uwezo wake, katika juhudi ya utendaji na malengo ya Kanisa lenyewe, katika mambo mbalimbali, kama vile ya kibiblia, kiliturujia, kidogma, kichungaji, kiekumeni, kimisioni na ya kijamii. Mashirika yawapatie wanashirika wake nafunzo ya kufaa ya kuendana na  nyakati na ya binadamu, kama vile ya mahitaji ya Kanisa, kusudi wenyewe, huku wakiweza kutambua kwa busara hali ya ulimwengu wa leo kadiri ya mwanga wa imani na wakiwaka ari ya kitume waweze kuleta manufaa kwa wengine kwa mafanikio makubwa. Kwa vile awali ya yote maisha ya kitawa yanalenga kuwawezesha wanachama wake wamfuate Kristo na waunganike na Mungu kwa kutimiliza mashauri ya kiinjili, lazima izingatiwe kwamba aina zozote zile za marekebisho, ziwe bora namna gani, hazitafanikisha, kama zisipoongozwa na upyaisho wa rohoni, ambao una nafasi ya kwanza katika kazi mbalimbali za utume wa nje pia.

30 May 2020, 08:30