Tafuta

Vatican News
Jubilei ya Miaka 100 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II: Kiongozi aliyejitahidi kuhakikisha kwamba, anamwilisha Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Jubilei ya Miaka 100 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II: Kiongozi aliyejitahidi kuhakikisha kwamba, anamwilisha Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.  (Vatican Media) Tahariri

TAHARIRI: Jubilei ya Miaka 100 ya Kuzaliwa: Mt. Yohane Paulo II

Mtakatifu Yohane Paulo II, anasema ni kiongozi ambaye maisha na utume wake ulikita mizizi katika mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Akajitahidi kusoma alama za nyakati na hivyo kufungua mikakati mipya ya maisha na utume wa Kanisa. Ilikuwa ni tarehe 27 Oktoba 1986, Jumuiya ya Kimataifa ilipokuwa imegubikwa na hofu na mashaka juu ya kuzuka kwa Vita ya Nyuklia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake kuhusu Jubilei ya Miaka 100 tangu Kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II, anasema, huyu ni kiongozi ambaye maisha na utume wake ulikita mizizi katika mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Akajitahidi kusoma alama za nyakati na hivyo kufungua mikakati mipya ya maisha na utume wa Kanisa. Ilikuwa ni tarehe 27 Oktoba 1986, Jumuiya ya Kimataifa ilipokuwa imegubikwa na hofu na mashaka juu ya kuzuka kwa Vita ya Nyuklia! Mtakatifu Yohane Paulo II, kwa kusoma alama za nyakati, huku akiongozwa na ushupavu wa kichungaji, kiasi hata cha kuvuka vikwazo vilivyojitokeza ndani na nje ya Kanisa, akafanikiwa kuwakusanya viongozi mbali mbali wa dini na madhehebu ya Kikristo, ili kusali, kwa ajili ya kuombea amani duniani!

Huu ni mtindo mpya ambao unapania kulinda na kudumisha amani hata kama si matunda ya majadiliano na muafaka unaofikiwa na wanasiasa au wachumi! Matokeo ya sala hii iliyoadhimishwa katika umoja na utofauti wake kwa misingi ya kidini na madhehebu ya Kikristo, ilionesha muungano kati ya binadamu na nguvu kubwa zaidi, inayozidi uwezo wa binadamu peke yake. Mtakatifu Yohane Paulo II alisema, uwepo wao ni kutokana na uhakika kwamba, wanahitaji sala madhubuti inayofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu; sala yenye matumaini, ikiwa kama watu hatimaye, wanataka ulimwengu unaosimikwa katika amani ya kweli na yakudumu. Tarehe 18 Mei 2020, Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II.

Ni kiongozi aliyetoka masafa ya mbali na katika utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ameliongoza Kanisa kuweza kuingia katika Mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Katika maisha yake, amefanikiwa kuona Ukuta wa Berlin, uliotenganisha Ulaya ya Mashariki na Maghariki ukaporomoka Akatumaini kuona mapambazuko mapya yanayosimikwa kwenye misingi ya amani. Katika uzee na ugonjwa wake, akajikuta anaanza kupambana tena na mifumo mipya ya vita pamoja na vitendo vya kigaidi; kwa baadhi ya waamini wenye misimamo mikali ya kidini, kutumia jina la Mwenyezi Mungu kupandikiza utamaduni wa kifo na uharibifu wa mali za watu! Ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo, kunako mwezi Januari 2002, Mtakatifu Yohane Paulo II akaitisha tena mkutano wa Sala kwa ajili ya viongozi wa dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo.

Mtakatifu Yohane Paulo II alipenda kukazia umuhimu wa kusimama kidete katika misingi ya amani bila kutumbukia katika kinzani za kiitikadi na kitamaduni, kwa kujielekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana katika misingi ya kitamaduni na kidini. Katika maisha yake, ameshuhudia imani thabiti iliyojengeka kwenye mwamba imara, akaonesha utajiri wa maisha yake ya kiroho na utu wema. Aliweza kujenga utamaduni wa kuzungumza na watu wote na wala hakutoa mwanya hata kidogo kuzuka tena kwa Vita na kinzani kati ya watu. Akajielekeza zaidi katika kipindi cha mpito, ili kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani. Alibahatika kutembelea sehemu mbali mbali za dunia, ili kukutana na watu wa Mungu, ili hatimaye, kuwatangazia na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Akajipambanua kama mlinzi na mtetezi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Akajielekeza zaidi katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa kutembelea Sinagogi la Roma, akiwa ni Papa wa kwanza katika historia kutembelea eneo hili. Alibahatika pia kutembelea Msikiti mkubwa wa Roma. Kwa hakika, Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake, alijitahidi kunafsisha Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Akafanikiwa kujielekeza zaidi katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa tayari, katika majadiliano ya kiekumene kuangalia nafasi na dhamana na Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili kujenga na kuimarisha umoja wa Wakristo. Ushuhuda wa maisha na utume wake, ni endelevu hata katika ulimwengu mamboleo!

Tahariri: Jubilei Maka 100 JPII

 

18 May 2020, 14:23